Sasa ni kipofu, adai serikali imemtelekeza
Na Richard Konga, Arusha
TINDIKALI inaweza kuwa silaha hatari sana na haifai hata kidogo katika jamii, wanaokutwa nayo ingefaa wafungwe kifungo cha maisha kwani wanapoitumia vibaya huleta madhara yasiyoelezeka.

Kuthibitisha hayo tunawaletea maelezo ya Elisha Kombe aliyekuwa Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Kitengo cha Upelelezi mkoani Mwanza, aliyemwagiwa tindikali akiwa katika majukumu ya kikazi mkoani humo.
Miaka 15 iliyopita alikuwa mchapakazi na tena mtanashati na nadhifu mwenye viungo kamili na alikuwa akifanya kazi yake kwa umakini mkubwa lakini leo, anaililia serikali kwa kile alichodai kumtelekeza baada ya kumwachisha kazi kutokana na tukio hilo lililomfanya awe kipofu.
Kombe alikutana na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha ambapo anaishi na kaka yake, George Kombe baada ya kunusurika kifo kutokana na kumwagiwa tindikali wakati alipokuwa Mwanza kwa shughuli maalumu za kikazi.
Akisimulia mkasa huo wa kumwagiwa tindikali, Kombe alisema: “Nilipata uhamisho kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania Dar es Saalam (TRA)  Septemba, 1997 kwenda mkoani Mwanza kwa ajili ya kazi maalumu ya ukaguzi na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa mapato na magendo kwa baadhi ya wafanya biashara wasio waaminifu.
“Nikiwa Mwanza nilishuhudia mianya hiyo ya ukwepaji wa mapato kwa baadhi ya wafanya biashara waliokuwa wakitumia usafiri wa majini na baadhi ya meli na boti zilikuwa zikisafirisha bidhaa kwa njia isiyo halali sambamba na magari yaliyokuwa yakitumika nchi kavu.
“Pamoja na upinzani niliokuwa naupata vikiwemo vishawishi mbalimbali ili niweze kupunguza kasi ya utendaji niliokuwanao lakini nilikuwa na msimamo wa kutekeleza majukumu yangu ya kikazi kwa haki kama nilivyoagizwa na viongozi wangu,” alisema Kombe.Aliongeza kuwa hali hiyo iliashiria kujengeka kwa hali ya chuki kwa baadhi ya mitandao ya wafanya biashara mkoani humo waliokuwa wakijishughulisha na biashara mbalimbali zikiwemo za mafuta, sabuni, bati na nyinginezo  huku wakibainika kukwepa kulipa mapato ya serikali.
Aliendelea kusema kuwa katika mamlaka hiyo aliitumikia zaidi ya miaka 11 akiwa ameitumikia serikali kwa uaminifu hadi Februari, 1998 alipomwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akigonga katika geti la nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Kirumba jijini Mwanza.
ANAIKUMBUKA SIKU HIYO YA BALAA
“Ilikuwa ni majira ya saa nne ya usiku nikiwa katika hali ya matembezi ya kawaida ambapo katika matembezi hayo walijitokeza baadhi ya wafanyabiashara ambao walinisalimia ndipo baada ya kuachana nao nilielekea nyumbani kwangu, nilipofika kwenye geti nilianza kugonga ili mlinzi aje afungue ghafla niliitwa jina langu na mtu niliyehisi alikuwa nyuma yangu, nilipogeuka, ghafla nilimwagiwa tindikali kichwani,” alisema Kombe.
Akaongeza kuwa tukio hilo lililoashiria kupangwa lilimletea maumivu makali ya kichwa ambapo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza na baadaye akahamishiwa KCMC. Baada ya kushindikana katika hospitali hizo alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Leeds iliyopo nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi ambapo baada ya miezi minane alipata nafuu na kurudi nchini.
Kombe ameshangazwa na hatua ya serikali kumlipa shilingi milioni 12 kama mafao yake huku ikiwa imemtelekeza kwa kumwachisha kazi wakati ana familia ya watoto wanne  wanaomtegemea na kwamba fedha hizo hazimtoshi kutokana na majeraha aliyoyapata katika eneo la kichwa na maeneo mengine ya mwili wake.
“Naiomba serikali inipatie kazi kwani ulemavu wangu hauwezi kunizuia kufanya kazi katika idara yoyote au katika mamlaka hiyo hata kama ni kitengo cha huduma kwa wateja, mawasiliano na nyinginezo ili  niweze kujipatia kipato cha kuniwezesha kuishi na familia yangu na kunisaidia katika matibabu.”
Yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia mpiganaji huyu wa uchumi wa nchi hii kwa simu namba 0787 926549 Kutoa ni moyo.