Mahakama moja nchini Ufaransa imeamuru kuachiliwa kwa aliyekuwa Kanali wa jeshi la Rwanda , anayesakwa na taifa hilo kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo.
Rwanda iliwasilisha ombi la kutaka Kanali huyo Laurent Serubuga, wa kabila la Hutu, na ambaye alihudumu kama naibu mkuu wa majeshi kurejeshwa nchini humo.Kanali Serubuga mwenye umri wa miaka 77, alikamatwa mwezi Julai Kaskazini mwa Ufaransa baada ya Rwanda kutoa kibali cha kumkamata.

Takriban watu 800,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi, waliuawa na wahutu ambao ni wengi kwa idadi nchini Rwanda mnamo mwaka 1994.
Mwanawe Serubuga alikuwa mahakamani kushuhudia kesi hiyo. Wakati jaji akitoa uamuzi wake, alisema kuwa wameridhishwa na uamuzi wa kumwachilia huru babake.
"tulirajaria kesi ya kisiasa. Uongo wa Rwanda haujasikika mbele ya mahakama hii," alinukuliwa akisema na shirika la habari la AFP .
Mahakama iligundua kuwa wakati wa mauaji ya kimbari, uhalifu wa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu haungeweza kuadhibiwa chini ya sheria ya Rwanda, kwa hivyo, bwana Serubuga hangeweza kuchukuliwa hatua zozote kwa makosa ambayo hayakuwa na adhabu.
Sheria za Ufaransa, haziruhusu mshukiwa au mhalifu kurejeshwa kwao hasa ambapo mshukiwa ana wasiwasi ikiwa haki zake zinaweza kulindwa, alisema wakili wa Bwana Serubuga.
Wakili aliyekuwa anatetea maslahi ya Rwanda alisema kuwa hakushangazwa na uamuzi huo kwani Ufaransa mara kwa mara imekataa kuwarejesha washukiwa wa mauaji hayo nchini Rwanda ili wakabiliwe na sheria.