Watu watatu wamezuiliwa nchini Afrika Kusini kuhusiana na mauaji ya watoto wawili ambayo yalizua ghasia katika mtaa wa Diepsloot.
Kwa mujibu taarifa ya polisi, miili ya wasichana wawili walio na umri wa miaka miwili na mitatu ilipatikana imetpwa kwenye choo cha umma siku ya Jumanne baada ya wawili hao kupotea siku ya Jumamosi.

Ghasia zilizuka huku wenyeji wakiwatuhumu polisi kwa kukosa kulinda jamii ipasavyo.

Rais Jacob Zuma aliwasihi wasichukue sheria mikononi mwao.

"kitendo hiki cha unyama dhidi ya watoto wetu, sio kitu ambacho kinapaswa kufanywa katika jamii hii ambayo daima tunajitahidi kuiunda,'' alinukuliwa akisema Rais Zuma kwenye jarida moja la mtaani Soweto.

''Tunalaani vikali mauaji haya.''

Luteni kanali Lungelo Dlamini, alisema kuwa watu watatu wanahojiwa na polisi na kuwa wangali wanamsaka mtu wa nne anayeshuiwa kuhusika na kitendo hicho.

Alisema kuwa pia wanachunguza kuwepo uhusiano kati ya mauaji hayo na yale ya mtoto mwenye umri wa miaka mitano aliyepatikana amefariki katika eneo hilo hilo, mwezi Septemba.

Kulingana na jarida la Star wenyeji wa Diepsloot, jamii masikini Kaskazini kwa Johannesburg, waliweka vizuizi barabarani na kuchoma magurudumu ya magari.

Maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni, yaliporwa huku waandishi wa habari wakishambuliwa.

Wasichana haio walikuwa na uhusiano wa kifamilia , na walipotea Jumamosi nyumbani kwao wakiwa wanacheza na marafiki zao.