AU inajadili swala hili baada ya ICC kupuuza ombi la kutaka kuhamisha kesi za
Kenyatta na Ruto
Mawaziri wa mambo ya nje Afrika wanakutana mjini Addis Ababa
nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara la Afrika na mahakama ya kimataifa ya
jinai ICC.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia Tedros Adhanom Ghebreyesus ameilaani
mahakama ya ICC kwa kusema ina mapendeleo sana na hicho sio kitu kinachokubalika
na kuwa ina uonevu kwa nchi za Afrika.
Waziri huyo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao maalum cha AU kuhusu
mahakama ya ICC.
Kikao hicho kinafuatia ombi la serikali ya kenya.
Umoja wa Afrika unaishtumu mahakama ya ICC kwa kuwalenga viongozi wa bara
hilo huku ikipuuzilia mbali uhalifu mwengine dhidi ya binadamu unaotekelezwa
katika maeneo mengine ulimwenguni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho waziri wa maswala ya kigeni
kutoka Ethiopia Tedros Adhanom ameishtumu mahakama hiyo kwa kukataa kuheshimu
uwezo wa marais wa bara Afrika na kukitaka kikao hicho kushutumu mahakama
hiyo.
Aidha amekitaka kikao hicho kuwasilisha ombi la kuahirisha kesi
zinazowakabili Rais wa kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake Wiliam Ruto kusikizwa
katika mahakama hiyo.
Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC kukataa ombi la wanachama 34 wa
Muungano wa Afrika kurejesha kesi za Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto
nyumbani.
Miongoni mwa yatakayozungumziwa ni hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama
hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya ICC na AU, viongozi wa Afrika
wanakutana katika makao makuu ya AU katika kile kinachosemekana ni kutafakari
upya uhusiano wa bara hilo na mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa kushughulikia ombi
lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za Kenya. AU inasema kuwa ICC ina
njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi
za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mahakama hiyo.
Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008
ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.
Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa mrengo wa Jubilee
unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya kuondoa Kenya kutoka katika mahakama
ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza nchi za Afrika kujadili hoja
ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na majirani zake kama Uganda na
Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni
zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU isikubali kwa ujumla kujiondoa
ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa
ICC. |
0 Comments