Hata hivyo, aliwataka wananchi kuunganisha nguvu zao kupitia vikundi vya Polisi jamii kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua watu wanaotaka kuchafua sifa ya Zanzibar.
Alisema kazi ya kulinda amani ya nchi ni jukumu la kila mwananchi kuahidi Serikali itaendelea kuwasaka wahusika wa vitendo hivyo na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria.
Dk Shein alisema kuwa,Serikali itaendelea kutekeleze dira ya Maendeleo ya 2020 pamoja na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini kwa wananchi wake (MKUZA) na tayari ufanisi wa mipango hiyo umeanza kuonekana licha ya kuwapo changamoto.
“Uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 7.0 kutoka 6.7 kwa mwaka 2011 tofauti na ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.3 katika Bara la Afrika,”alisema Dk Shein.
Bakwata wamempongeza Rais Kikwete siku moja baada ya Rais Kikwete kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema,Cuf,NCCR-Mageuzi,TLP na UDP,Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limepongeza hatua hiyo na kuita yenye manufaa kwa taifa.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi,Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila akitoa salamu za Baraza la Idd jana katika Msikiti wa Al Farouk uliopo Makao Makuu ya Baraza hilo, Kinondoni Dar es Salaam,alisema uamuzi wa Rais Kikwete una lengo la kuhakikisha mchakato wa Katiba unaoendelea unamalizika kwa amani.
Naye Mgeni rasmi kwenye baraza hilo, Waziri wa Maji,Profesa Jumanne Maghembe, aliwataka Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini na kuepuka ushabiki wenye lengo la kuhatarisha mustakabali wa amani nchini.
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Ibrahim Yamola na Pamela Chilongola.
0 Comments