Operesheni Kimbunga awamu ya Pili
iliyoanza tarehe 21 Septemba, hadi kufikia
tarehe 01 Oktoba, 2013 imekamata watuhumiwa wa ujambazi wa kutumia
silaha 88. Kati ya hawa, 27 walikamatwa mkoani Kigoma, 43 mkoani Geita na 18
mkoani Kagera.  Watuhumiwa hawa wanaendelea
kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi ili hatimaye wafikishwe kwenye vyombo vya
sheria.


Wakati huo huo, Operesheni hii
imefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhamiaji haramu 425, kati yao 166
walikamatwa mkoani Kigoma, 50 mkoani Geita na 209 mkoani Kagera.


Wengine waliokamatwa ni watuhumiwa wa
ujangili 11, kati yao sita mkoani Kigoma na watano mkoani Geita, na watuhumiwa watano
kwa kuhifadhi au kutorosha wahamiaji haramu  kati yao wane kutoka mkoa wa Kigoma na mmoja,
mkoa wa Geita.


Vitu vingine vilivyokamatwa katika
Operesheni hii ni SMG 3, Pistol 2 mkoani Kigoma na Gobole 18, moja mkoani
Kigoma na 17 mkoani Geita. Vingine ni risasi 471 za (SMG/SAR), Star Pistol 13,
Magazine za SMG 2, Sare 1 ya Jeshi la Burundi na Shati moja, vyote katika mkoa
wa Kigoma.


Vingine ni bomu  moja la kurushwa kwa mkono mkoani Kigoma,
ngombe 2220 katika Hifadhi ya Taifa ya Biharamulo mkoani Kagera, gunia 100 za
mkaa mkoani Geita, gongo lita 271, mkoani Kigoma 11 na 260 mkoani Geita.  Nyara za Serikali zilizokamatwa ni ngozi ya
mbweha moja na meno matatu ya Kiboko mkoani Geita.  Bangi kilo tatu na nyavu haramu za uvuvi
(makokoro) 12 pia zilikamatwa mkoani Geita.


Akizungumza katika Mkutano na
Waandishi wa habari mjini Bukoba leo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Simon
Sirro, kwa niaba ya Operesheni Kamanda wa Operesheni Kimbunga, alisema
haieleweki ni vipi watendaji wa Vijiji, Kata na Tarafa wanashindwa kutoa
taarifa kuhusu wahalifu katika maeneo yao, wakiwepo wahamiaji haramu, na kuwa
viongozi hawa wanawajibika na uhalifu unaotokea katika maeneo yao.  


Alisema ni imani ya watendaji
wa Operesheni Kimbunga kuwa Watendaji hawa wataanza kuwajibika ili kukomesha
matukio ya uhalifu hapa nchini.

IMEANDALIWA NA TIMU YA HABARI 

– OPERESHENI KIMBUNGA