Dar es Salaam.
 Seleman Rajab (17) anaugua ugonjwa ambao mpaka sasa wazazi wake wanasema hawaufahamu. Licha ya kuwa na maumivu na uvimbe kuongezeka, mara ya mwisho kupelekwa hospitali ilikuwa mwaka 2010, zaidi amekuwa akipewa vidonge vya kutuliza maumivu.
Mama yake anayemlea Khadija Ahmed anasimulia kuwa, alielezwa kwamba Rajab alizaliwa akiwa na uvimbe kwenye unyayo.
Akiwa na umri wa miaka miwili hakuweza kutembea, akapelekwa hospitali kufanyishwa mazoezi ya viungo na alipotimiza umri wa miaka sita, uvimbe huo ukaanza kututumka kidogo kidogo.
“Alikuwa akiishi na mama yake ambaye alifariki Agosti mwaka jana, hakutuambia hospitalini aliambiwa mtoto anaugua nini, lakini mara ya mwisho kumpeleka hospitali ya CCBRT ilikuwa mwaka 2010 na kwa sababu ilipendekezwa akatwe mguu, mama yake hakumrejesha tena,” mama Seleman

Anasema tangu waanze kuishi na mtoto huyo, mwaka jana hawajampeleka hospitali yoyote kutokana na kukosa fedha ya kugharamia vitu mbalimbali ikiwamo kukodi gari la kumpeleka hospitali na kumrejesha nyumbani.

Baba Selemani anafanya kazi ya kutunza bustani kwenye kiwanda cha Kamal Steel, kinachotengeneza nondo  na mama yake ni mama wa nyumbani ambapo familia yake ni yenye watoto watano, wa kike mmoja wa kiume.Wadogo zake wanasoma shule.
Selemani anasema, “Naomba nisaidiwe angalau na mimi niwe na uwezo wa kutoka nje au kujihudumia mwenyewe badala ya sasa ambapo ninaogeshwa, nikitaka kutoka nje mpaka baba na mama waniweke kwenye blanketi, wanibebe mmoja huku mwingine kule, inaniuma sana.”

Anasema huwa anapata maumivu mara moja, kwamba huhisi viungo hususan mguu uliovimba kama vile ndani yake kuna moto unawaka na kwamba inapotokea hali hiyo, hupewa vidonge vya kutuliza maumivu; mara nyingi humsaidia kupunguza maumivu.

Tangu mwaka jana, mguu wa kushoto nao umeanza kuvimba. Hata sikio linaonekana kuanza kuvimba. Pamoja na matatizo yote yanayomkabili tangu utoto, Seleman anaweza kusoma na kuandika majina yake na ya wazazi wake.

Anasema alikuwa akifundishwa na marehemu mama yake, kwamba alinunua ubao mdogo ambao alikuwa akiutumia kumfundishia kusoma na kuandika.

Hakuwahi kuingia darasani na anasema ikitokea Mungu akamponya, atasoma  sana ili awe mwalimu au daktari.Baba Seleman anasema katika familia yao hakuwahi kutokea mtu kuugua ugonjwa wa aina hiyo, ila baba mzazi wa mama yake mguu wake mmoja una ugonjwa wa tende, umevimba sana lakini anasema yeye hutembea na kufanya shughuli zake kama kawaida.
Lakini ninapotazama sura ya Baba Selemani (Rajab) kwenye kidevu upande wa kushoto ana uvimbe mkubwa kidogo, anasema umekuwapo kitambo sasa na kwamba alienda hospitali ya Amana akaandikiwa dawa za kutumia na kwamba huwa anazitumia ingawa haoni mabadiliko,“Hiki kipo siku nyingi tu, wala hakiumi.”

Maisha ya Seleman

Baba yake anasema huwa anaoga mara moja kwa siku. Hii inatokana na ukweli kwamba ni lazima amuogeshe mwenyewe (baba) na inatakiwa iwe usiku kwa sababu kutokana na mazingira ya familia hiyo, ambayo inaishi katika vyumba viwili yenye choo cha nje na cha shimo; anaogea nje- uwanjani.
“Umri wa miaka 17 siyo mdogo, ameishajitambua,  hivyo siyo rahisi tumuogeshee nje mchana, huwa tunasubiri giza liingie, tunamuweka kwenye blanketi mimi nashika huku mama yake kule tunamtoa nje, tunatandika turubai, namuogesha,” anaeleza baba Seleman

Anasema hata anapotaka kujisaidia, wanamtengea kifaa na kumsaidia kuunyanyua mguu uliyojaa ili aweze kukaa vizuri kwenye chombo na kujisaidia.

Hawezi kujihudumia kwa kitu chochote. Kuhusu kula inaelezwa na mama yake kuwa anakula kila kitu isipokuwa viazi mviringo na uji wa ulezi; vinamvuruga tumbo.

Wazazi hao wanaomba msaada ili mtoto huyu apelekwe hospitalini, afanyiwe uchunguzi na ikiwezekana atibiwe, ili naye aishi kama watoto wengine.
Kwa atakayeguswa na mateso yake na kufikia uamuzi wa kumsaidia awasiliane na gazeti hili, Mhariri wa Dawati la Ndani ya Habari (Dismas Lyassa) kwa mpesa 0754498972 au  tigo pesa 0712183282. Kutoa ni moyo na huongeza baraka katika maisha, ni furaha ya Mungu kuona wanadamu wanajaliana hasa wakati wa shida, ndivyo yanavyosema maandiko matakatifu.

Je, ugonjwa huu hutokana na  nini? Usikose toleo la jumatatu ili kuufahamu kwa kina na kujua namna ya ili hata wewe usiupate, kwani utafiti wa awali unaonyesha mtu yeyote anaweza kuupata.