Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa mahakamani leo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro leo imetupilia mbali ombi la kufutiwa shitaka moja kati ya matatu yanayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda. Ponda anakabiliwa na mashitaka matatu; ambayo ni kutokutii amri halali, kuharibu imani za dini na kushawishi kutenda kosa. Ombi la kufutiwa shitaka moja liliwakilishwa na Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro, mahakamani hapo Septemba 17, mwaka huu, akitaka shitaka la kwanza la kutotii amri halali linalomkabili mteja wake lifutwe. Wakili Nassoro alidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza shitaka hilo, vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Kesi hiyo imeahiriswa mpaka Novemba 7 mwaka huu ambapo mahakama itaanza kusikiliza mashahidi wa kesi hiyo. Sheikh Ponda amerudishwa rumande.