Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Kigoma.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewahimiza viongozi wa Kanisa la Morovian Jimbo la Ziwa Tanganyika kuwekeza zaidi kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
 Pinda alisema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Kigoma waliohudhuria Sherehe za Uzinduzi wa Jimbo la Ziwa Tanganyika Kanisa la Moravian Kigoma.

 Waziri mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, alimuomba Askofu Dk Isack Nicodemo wa Kanisa la Moravian Tabora ambaye ndiye mlezi wa jimbo hilo jipya, kuhakikisha anawapeleka vijana wa kanisa hilo kwenye Chuo cha Kilimo cha Mubondo kilichopo wilayani Kasulu, Kigoma ambacho kinatoa mafunzo ya kilimo kwa vijana katika ngazi za Astashahada na Stashahada ya Kilimo.
  ìWakati nikiwa vijijini, nimeona licha ya Mkoa wa Kigoma kuwa na ardhi nzuri na ya kutosha, wananchi wengi wanalima bila ya kutumia kanuni bora za kilimo. Hivyo, niliuelekeza uongozi wa chuo hicho kuweka kozi maalumu kwa watu wasiohitaji cheti kwaajili ya kuajiriwa, wapatiwe kozi maalumu kwa lengo la kuwawezesha kutumia mafunzo hayo kubadili kilimo walichonacho na kukifanya kuwa na tija zaidi,îaliongeza.
 Ã¬Nitoe wito kwa kanisa kuendeleza miradi hii ya kilimo kwa vijana kwa njia ya vikundi, muwasaidie kwa kuwaelekeza ili vikundi hivi visajiliwe na  vijana hao wakopesheke kwa lengo la kupata misaada ya aina mbalimbali. Pia, muwawezeshe kuzalisha kitaalamu, kuyaongezea thamani mazao yao kabla ya kuyauza, kupata nembo za ubora kwa ajili ya bidhaa zao,î alisema.
  Amesema kanisa na wakazi wa Kigoma wana fursa ya kukitumia Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi Nyamidoho kilichopo wilayani Kasulu kinachojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la World Vision ambacho lengo lake ni kutoa mafunzo ya kuongezea vijana wa mkoa huu stadi mbalimbali za kazi.
 Ã¬Nilipata fursa ya kuweka jiwe la msingi katika hicho ambacho nimesema kipandishwe hadhi na kuwa chuo cha Wilaya . Nawasihi waumini wa jimbo hili kuvitumia vyuo hivyo kikamilifu kwa kuwajengea stadi za kazi vijana wetu ili wawe chachu ya mabadiliko katika vijiji,mkoa huu na Taifa kwa  ujumla,î alisisitiza.
  Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa jimbo hilo kwa juhudi zake za kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha Jamii kuwa na mazoea ya kupanda miti.
  ìNawasihi wana-Jimbo na wananchi wote kwa ujumla kupitia hadhara hii, kuendelea kutunza mazingira yetu ili nayo yatutunze. Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema: ìUmaskini na uharibifu wa mazingira ni watoto pacha na mama yao ni ujingaî. Hivyo, tunalo jukumu la kuhifadhi mazingira kwa kutunza misitu iliyopo, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi udongo na uoto wa asili. Tujue kwamba uharibifu wa mazingira unaleta umaskini,î alisema.
  Aliwataka waangalie namna ya kuweka taratibu mahsusi za kuishi pamoja na wafugaji kwenye maeneo yao ili wasiharibu vyanzo vya maji.
  Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Hawa Ghasia, Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandishi Christoher Chiza, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu,Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge pamoja na Naibu Waziri Nishati na Madini, George Simbachawene.