Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete wakipata maelezo ya kiwanda kipya cha chai cha Ikanga, Njombe, baada ya kukizindua ikiwa ni sehemu ya sherehe za uzinduzi rasmi wa mkoa mpya wa Njombe Ijumaa Oktoba 18, 2013.PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Oktoba 18, 2013, amezindua rasmi Kiwanda cha Kusindika Chai cha Ikanga, Tarafa ya Lupembe, Wilaya ya Njombe katika Mkoa Mpya wa Njombe.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa asilimia 25 na wakulima wa chai wa Lupembe ni ukombozi mkubwa wa wakulima wa Tarafa ya Lupembe ambao wamekuwa wanakabiliwa na ukosefu wa sehemu ya kuuza chai yao.
Ufunguzi wa kiwanda hicho cha Ikanga Tea Factory kinachomilikiwa na Kampuni ya Ikanga Tea Factory Limited ni utekelezaji wa ahadi ya Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati anafanya kampeni ya Urais katika Tarafa ya Lupembe mwaka 2010. Ni kiwanda kipya zaidi na bora zaidi cha kusindika chai katika Tanzania.
Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwishoni mwa mwaka 2010 baada ya Serikali ya Rais Kikwete Mei mwaka huo huo kuiomba Kampuni ya Mufindi Tea and Coffee Limited (MTC) kujenga kiwanda cha kusindika chai ya wakulima ambayo sehemu yake kubwa ilikuwa inapotea na kuoza kwa sababu ya ukosefu wa kiwanda.
Ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho, MTC iliunda kampuni mpya ya Ikanga Tea Company Limited Septemba 2010. Kampuni hiyo ni ubia kati ya MTC na wakulima wa chai wa Lupembe ambao wanamiliki asilimia 25 za hisa za kiwanda hicho kupitia umoja wao wa Lupembe Tea Farmers Trust.
Uzinduzi wa leo ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanda hicho. Chini ya awamu hiyo ya kwanza yenye uwezo wa kusindika tani 1,800 za chai kwa mwaka kwa kutumia njia moja ya uzalishaji iliyokamilika Juni mwaka jana kwa gharama ya Sh. bilioni 3.75.
Awamu ya pili ambayo inaendelea kujengwa, itagharimu Sh. bilioni 1.48 na ikikamilika kiwanda kitakuwa na uwezo wa kusindika tani 3,500 na awamu ya tatu na ya mwisho itagharimu Sh.bilioni 1.5 na kukamilika kwa awamu hiyo kutakiwezesha kiwanda kusindika tani 5,000 za chai kwa mwaka.
Chini ya uendeshaji wa Kiwanda hicho, chai yote ya wakulima inanunuliwa kwenye vituo maalum na kusafirishwa kwenda kiwandani na magari ya Kiwanda. Wakulima pia wanapewa mbolea kwa mkopo na wakulima wote wa chai inayochukuliwa na kiwanda hulipwa kila mwezi kwa bei iliyopangwa na Bodi ya Chai Tanzania.
Miongoni mwa mipango ya Kampuni ya Chai ya Ikanga ni kununua angalau hekta 600 za ardhi ili nayo ianze kulima chai ili kuongeza kiwango cha chai kinachozalishwa katika eneo la Lupembe na ukamilishaji wa shule kwa ajili ya watoto wa wakulima wa eneo la Lupembe.
Rais Kikwete amezindua Kiwanda hicho ikiwa ni shughuli ya kwanza katika shughuli nyingi ambazo atazifanya wakati wa ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Njombe kuzindua na kukagua shughuli za maendeleo. Miongoni mwa shughuli hizo itakuwa ni kuuzindua rasmi
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Oktoba, 2013
|
0 Comments