Dar es Salaam. Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania, (TRL) umeunda tume kuchunguza chanzo cha ajali zilizotokea Urambo na Usoke mkoani Tabora.
Tume hiyo inajumuisha wafanyakazi wa Idara za Usafirishaji, Fundi mitambo, Ujenzi na Usalama wa Reli.
Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake, Msemaji wa kampuni hiyo, Midladjy Maez, alisema treni hiyo ya mizigo ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Kigoma.
Kwa mujibu wa Maez, ilianguka ikiwa na mabehewa 10 ya mafuta na manne kati ya hayo yalianza kuvuja.
Alisema hasara iliyotokana na kumwagika kwa mafuta hayo yaliyokuwa mali ya Kampuni ya GBP, TRL itafahamika baada ya tume hiyo kumaliza kazi yake.
Maez alisema hakuna abiria aliyeathiriwa na ajali hiyo na kwamba jana jioni treni ilitarajiwa kuendelea na safari yake.
Wakati hayo yakitokea, Serikali imetangaza mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta ya Uchukuzi na Ujenzi kwa kununua mabehewa 123 na vichwa 21 vya treni ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta hizo.
Serikali pia ipo katika hatua ya kupunguza vituo vya ukaguzi wa mizigo kutoka vituo 15 hadi kufikia vituo vitatu na kufunga mitambo ya kisasa ya kupima mizigo wakati gari inapotembea barabarani ili kurahisisha upekuzi wa mizigo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alipokuwa akifungua mkutano wa saba wa mwaka wa wadau wa sekta ya usafiri, uchukuzi na ujenzi.
Dk Mwakyembe alisema “Serikali kwa sasa imeanza kufufua miundombinu ya reli ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.”
|
0 Comments