Wanafunzi wa Shule ya Viziwi Dongobesh  wakiimba wimbo wa Taifa shuleni hapo mkoani Manyara. Kukosekana kwa walimu wa kufundisha lugha ya alama, imesababisha wanafunzi 39 kati ya 40 wenye ulemavu wa kutosikia waliomaliza elimu ya sekondari mwaka jana kupata daraja la sifuri. PICHA |MAKTABA
Dar es Salaam.
 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jasmine-Angellah Kairuki, amesema kukosekana kwa walimu wa kufundisha lugha ya alama, imesababisha wanafunzi 39 kati ya 40 wenye ulemavu wa kutosikia  waliomaliza elimu ya sekondari mwaka jana kupata daraja la sifuri.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kairuki alisema changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu huo kwa elimu ni kutokuwa na fursa sawa ya kutumia lugha wanayomudu.
Alisema utoaji elimu kwa watu wenye ulemavu huo, hauridhishi kutokana na walimu waliopo kuwa wachache ndiyo maana wanafunzi 39 walifeli na mmoja kupata daraja la nne.
“Tatizo hili linatokana na walimu  wanaofundisha lugha ya alama kuwa wachahe, hivyo nakuagiza Kamishna wa Idara ya Ustawi wa Jamii kutembelea shule za wanafunzi wasiosikia kuangalia elimu yao inatolewaje ili tupunguze  tatizo lililopo,” alisema Kairuki.
Kaiuiki alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataendelea kuelimisha jamii, ili kupata haki haki zao wanazostahili ikiwamo fursa ya kutumia lugha ya alama kuanzia  shule ya msingi hadi sekondari.
Ofisa Uhusiano wa Umoja wa Miradi Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita), Tungi Mwanjalu, alisema hali hiyo inatokana na kukosekana kwa walimu wenye ujuzi wa kutumia lugha ya alama na kubuni nyezo rahisi za kufundishia viziwi.
Mwanjalu alisema kutokana na tatizo hilo, viziwi nchini hawana ajira na kushindwa kudai haki zao za msingi ndani ya jamii inayowazunguka na kuonekana ni mzigo kwa taifa.