Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.

MUNGU ni mwema sana kwangu na kwako, lakini jambo kubwa la kuzingatia hapa ni kuzidi kumuomba ili nchi ipate Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayowafaa hata wajukuu na watukuu wetu wa vizazi vijavyo.Jambo hili la katiba mpya ya nchi linafaa kujadiliwa na wananchi bila kuchoka kwa sababu ndiyo ‘moyo’ wa nchi na kamwe asiwepo wa kufanya kuwa hilo ni jukumu la kundi fulani pekee. Hivi sasa rasimu ya katiba mpya inasumbua watu hasa viongozi wa vyama vya siasa.
Kwanza watu wanapaswa kujua maana ya rasimu; Ni andiko la awali la kitu chochote.

Wakati wananchi wengi tukiomba lipite salama, kuna baadhi ya wanasiasa wanaonesha wazi kuwa wanataka kulifanya jambo hilo lao pekee na kujaribu kuingiza itikadi za chama, kitu ambacho ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba ameliona hilo na wiki iliyopita amevionya vyama vya siasa; Chama Cha Mapinduzi na vyama vya upinzani, kutoweka masilahi ya vyama vyao kwenye katiba mpya ya nchi badala yake visaidie kupatikana iliyo bora.
 Hakuna siri kwamba tangu Rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania ilipozinduliwa, baadhi ya vyombo vya habari vimechapisha na kutangaza vifungu nyeti vilivyomo katika rasimu hiyo.
 Lengo limekuwa siyo tu kuwafahamisha wananchi kuhusu vipengele vilivyomo katika rasimu hiyo, bali pia kuanzisha mjadala wa kitaifa ili hatimaye ipatikane katiba bora ya nchi inayotokana na wananchi wenyewe na siyo viongozi au vyama vya siasa.
Kwa mfano; kuna kasoro katika sheria ya kuunda tume ya katiba, inasema tume ivunjwe mara baada ya kukabidhi rasimu lakini sheria hiyohiyo inaitaka tume itoe elimu kwa wananchi kabla ya kura za maoni kupigwa, jambo ambalo hata Rais Jakaya Kikwete ameliunga mkono mwishoni mwa wiki katika hotuba yake.
Kwa jinsi malalamiko yalivyo mengi kuhusu rasimu hiyo kuna dhana ya upotoshaji kwamba mchakato wa kupata umeisha, hivyo baadhi ya wananchi wanaweza kupumbazika kwamba zoezi hilo sasa limefikia tamati.
Jaji Warioba kafafanua kuwa kwa sasa tume yake inaendelea kuchambua maoni ya mabaraza ya katiba na baada ya kukamilisha kazi hiyo itaandaa ripoti na rasimu ya katiba ambayo wataiwasilisha kwa Rais Dk. Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kama sheria inavyosema.
Upo ukweli kwamba baadhi ya wanasiasa na viongozi katika ngazi mbalimbali nchini wamekumbwa na kiwewe na mfadhaiko mkubwa kwa hofu kwamba rasimu ikija kuwa katiba ya nchi itakuwa ni kiama chao cha kupoteza nafasi za uongozi.
Ieleweke kwamba bado kuna mijadala baadaye ambapo kutakuwa na kura ya maoni na hatimaye Bunge la Katiba litaundwa kuamua.
Hata hivyo, jambo kubwa linalojitokeza hapa ni kwamba wananchi, baadhi ya wanasiasa na viongozi katika ngazi mbalimbali wanauona mjadala wa rasimu hiyo kuwa muhimu zaidi pengine kuliko hatua nyingine za mchakato huo zilizobaki.
Hapana shaka kwamba rasimu hiyo ndiyo dira inayoonyesha njia, mbali na ukweli kwamba wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliotayarisha dira hiyo ni watu waadilifu.
Nasema hivyo kwa sababu wengi wao wakiwa na rekodi ya utumishi uliotukuka, mbali na majina yao kuonekana katika jamii kama taasisi, hatuna shaka nao na hawawezi kupendelea kundi la watu fulani. Wapendelee kundi moja ili iweje?
Hatujawahi kutilia shaka uadilifu na uzalendo wa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Warioba, wajumbe wake kama Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, Mwanadiplomasia wa siku nyingi, Dk Salim Ahmed Salim na wajumbe wengine wa tume waliotayarisha rasimu hiyo.
Nisisitize kwamba ninapotoa maoni haya sina maana kwamba rasimu hiyo isikosolewe na kwamba ni sahihi na kamili kwa asilimia mia moja au kupendelea jinsi mchakato unavyokwenda hadi sasa, ninachoshauri ni kwamba wananchi wote wasikilizwe na asiwepo wa kupuuzwa anapokuwa na hoja.
Mimi najua kwamba kwa kitu kizito kama hicho ni lazima kuwepo na upungufu wa hapa na pale na tayari baadhi umeainishwa na kujadiliwa na wananchi, lakini kama wapo ambao hawajapewa nafasi kuujadili kuna ugumu gani kuwapa nafasi?
Ukichunguza kwa undani utagundua kuwa katika mijadala ya rasimu hiyo inayoendelea, jambo kubwa linalojitokeza ni hofu kubwa inayotokana na baadhi ya wanasiasa kutojua mustakabali wao baada ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakapozinduliwa.
Ukizungumza na wananchi wengi utawasikia wakilalamikia kitendo cha wabunge wa chama kimoja kuwa wengi katika Bunge la Katiba, wengine wanalalamikia Zanzibar kutokushirikishwa katika utoaji wa maoni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wanasema hizo ni kasoro kubwa zilizoibuliwa na wanasiasa lakini zikapuuzwa.
Hakuna asiyejua kuwa viongozi nchini wamechaguliwa kwa neema ya Mungu, hivyo wasitumie nafasi zao kuamua kila jambo hata kama halina masilahi kwa nchi na wananchi wanaowaongoza na inawezekana kabisa kuwa madai ya wabunge wa CUF yana msingi, kwa nini wasisikilizwe?
Wapo viongozi wanaojipendelea katika jambo hili nyeti, hivyo basi wameelekeza nguvu zao katika kupinga baadhi ya vifungu vya rasimu ya katiba mpya vinavyogusa masilahi yao, vikiwamo kuanzishwa kwa serikali tatu, mgombea binafsi hadi ngazi ya urais, kushinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 50, kufutwa kwa viti maalumu bungeni  na kadhalika.
Wanasiasa wengi katika kundi hilo hawataki mabadiliko yatakayogusa nafasi zao au kukubali ukweli kwamba katiba mpya lazima iweke mfumo mpya utakaoleta mabadiliko ambayo wananchi wanayataka. Natoa wito, tujadili rasimu ya katiba na tusijadili watu.
Naamini kuwa iwapo tutapiga vita hofu na ubinafsi, Watanzania tutapata katiba bora itakayotuongoza kwa miaka mingi ijayo. MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.