Rais Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua vitalu vya gesi. Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Joyce Kisamo. Picha ya   Maktaba. 

Rasilimali hapa nchini zipo kedekede, isipokuwa mgawanyo wake ndio umekuwa tatizo, huku wazawa wakiamini kuwa wageni wanapendelewa na kujengewa mazingira mazuri zaidi ya kuzifaidi.
Dar es Salaam. Tanzania ni nchi iliyojaliwa rasilimali nyingi na za kila aina.
Ina ardhi kubwa yenye rutuba, misitu , wanyamapori, madini mengi yakiwamo vito vya thamani na hata vyanzo vingi vya maji.
Hata hivyo, miaka 51 tangu ipate uhuru wake na ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 45, Tanzania bado ni miongoni mwa nchi maskini duniani.
Licha ya Serikali kubadilisha mfumo kutoka sera yake asili ya ujamaa na kujitegemea ambayo iliiwezesha kumiliki rasilimali zote hadi miaka ya 1980 na kuhamia kwenye mfumo wa soko huria, bado rasilimali zake hazijawanufaisha Watanzania.
Katika mfumo huria, kumekuwa na sera za uwekezaji ambazo zimewezesha watu wengi wenye mitaji  kutoka nje ya nchi kupewa rasilimali , kuzitumia kwa uzalishaji.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 1990, kumekuwa na uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya madini ambapo kampuni kubwa za madini duniani  zimemilikishwa migodi ya madini, hasa dhahabu.
Hata hivyo, kutokana na kasoro za hapa na pale, Tanzania bado haijafaidika na madini hayo huku maeneo mengi yanakochimbwa madini hayo yakikithiri kwa migogoro na umaskini mkubwa.
Kumekuwapo pia na uwekezaji katika sekta ya kilimo ambapo wawekezaji kutoka nje wamepewa maeneo makubwa ili kuendesha kilimo cha kisasa cha mashamba makubwa.
Kilimo hiki nacho hakijaifikisha nchi mahali pa kujivunia huku wakulima wengi wakiendelea na kile cha jembe la mkono.
Gesi na mafuta: Wapi tuendako
Hivi karibuni baada ya serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) imekuwa ikiainisha maeneo inakopatikana gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara.Miradi mikubwa ambayo inaendelea na kazi hadi sasa ni ile ya Songosongo ulioko Lindi na Mnazi Bay wa Mtwara ambapo serikali inajenga bomba  la gesi katika mikoa hiyo mwili na kuileta jijini Dar es Salaam.
Hatua ya ujenzi wa bomba la Mtwara- Dar es Salaam  imezua mjadala na maandamano makubwa kwa wananchi hasa wa Mtwara tangu mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu wakipinga kusafirishwa kwa gesi hiyo ili hali mkoa huo ukiwa kati ya mikoa maskini nchini.
Wakati gesi hiyo ikiendelea kunguruma, serikali imefanya uzinduzi wa kihistoria wa uuzwaji wa vitalu vya utafutaji na uchimbaji gesi katika Bahari ya Hindi na Kaskazini  mwa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma, uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyefanya uzinduzi huo huku akisisitiza kuwa Serikali yake haitapata hasara kwa kualika wawekezaji wa nje.
“Kumekuwa na maneno mengi na mabishano katika jamii yanayojenga taswira kuwa mfumo wa sasa wa utoaji leseni ya utafutaji na uchimbaji wa gesi ni kama vile Tanzania inapata hasara na Watanzania hawafaidiki.
Hii tafsiri siyo sahihi,” anasema Rais Kikwete na kuongeza:
“Sheria iliyopo sasa, mkataba wa uzalishaji  unaiwezesha TPDC kuingia mkataba na kampuni binafsi. Kwanza, kampuni hiyo inapewa leseni na wakishapewa wao ndiyo wanaogharimia uzalishaji na kazi hiyo ina gharama kubwa.”
Ameitaka sekta binafsi kuchagua ama kuingia kwenye nafasi ya TPDC kwa kuuza hisa au kuingia kwenye uwekezaji wa kutafuta na kuchimba mafuta ambao ni ghali, kisha wakubali kuilipa Serikali gawio la asilimia 65 au 75 baada ya kupata gesi.
“Hiyo ndiyo sera, kwamba badala ya TPDC iende sekta binafsi…Ninachojua ni kwamba, kama sekta binafsi wakitaka kuwekeza, watafanya kwa masharti haya haya ya asilimia 75 na 65. Lakini, ni shughuli ghali, kisima kimoja ni Dola 100 milioni, nani kati yetu ataweza? Benki gani itakubali kutoa mkopo?”
Kuhusu ugawanaji wa faida, Kikwete alisema mwekezaji akianza kutoa gesi anakuwa na ruksa ya kulipa gharama zake, kisha kuna kuwa na utaratibu wa kulipa gawio la serikali.
“Utaratibu ni ama wanapata asilimia 35, sisi asilimia 65 ama wanapata asilimia 25 nasi 75 zilizobaki. Asilimia 65 ama 75 inashikiliwa na TPDC,” alisema.
Anasistiza Rais Kikwete kuwa kwa mfumo uliopo, Serikali haipati hasara badala yake masilahi ya  taifa yamezingatiwa.“Kwa hiyo, kwa mfumo huu, nataka kuwaeleza Watanzania kwamba, hatupati hasara na anayesema hivyo hasemi ukweli, na kama anaujua anapotosha watu,” anasema.
Amewataka wadau wa sekta binafsi kuzungumza na serikali badala ya kulaumu. Njia nyingine aliyoshauri kwa sekta binafsi ni kuungana na kampuni kubwa za nje zenye mitaji katika utafutaji na uchimbaji ili itakapopatikana gesi wagawane.
Kuhusu wazo la kuwatengea maeneo, Rais Kikwete anasema linaweza kuzua lawama kama sekta binafsi itakosa gesi pale ilipopangiwa.
“Hakuna mwenye uhakika kama kule mtakakopangiwa mtapata. Tunaweza kuwapangia maeneo, halafu akienda kule akakosa, Mswahili (Mtanzania) atasema wametupangia kusiko na gesi. Tutapata lawama,” alisema na Kikwete kuongeza:
“Natambua kabisa umuhimu wa wenzetu wa sekta binafsi kufadikika, sasa haya tukae tuzungumze kwa utaratibu, tusilaumiane.”
Mbali na kusema  serikali inapata faida, Rais Kikwete anasema kwa sasa wanajipanga katika kufanya ukaguzi wa faida inayopatikana kwenye  kampuni hayo ili faida isipotee.
Wazawa na umiliki wa rasilimali
Kabla ya uzinduzi huo kulikuwa na kongamano la wadau wa gesi na mafuta ambao walitoa sauti zao wakitaka nao wakumbukwe katika uwekezaji huo.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi ametaka wazawa wapewe kipaumbele kwenye uvunaji wa mafuta na gesi:
“Tunaambiwa sisi hatuna hela, eti hela zetu ni kwa ajili ya kufanyia biashara ya matunda. Hata hivyo, tunayo ardhi, Tanzania siyo nchi maskini, gesi ni mtaji wetu, tuweke mkakati wa kugawa,” anasema Mengi na kuongeza:
“Huku ni kuwa maskini wa fikra na tutakuja kuulizwa na Mwenyezi Mungu. Kama serikali haina sera itauzaje rasilimali zetu kwa wageni? Tusingependa kuyazungumza haya hadharani lakini tunasema tu. Mtu mwenye hekima pale wizarani wa kutusikiliza ni Maswi pekee yake.”
Wasiwasi kuhusu kodi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Jamidu Katima anaonyesha wasiwasi kuhusu eneo la kodi kwa wawekezaji wa nje.
“Wasiwasi wangu ni nataka kujua, mmejipangaje ili kuhakikisha mfumo wa utozaji kodi ni unafanya kazi kabla ya kuanza uzalishaji wa gesi?” alihoji Profesa Katima.
Mchungaji William Mwamalanga anasisitiza haja ya Watanzania kumilikishwa rasilimali zao.
“Naishauri serikali tuwe na utaratibu wa mazungumzo yetu sisi wenyewe…lakini sijasikia suala la kodi. Mwenyekiti yoyote ili tuwe na nchi yenye nguvu na kujivunia ni lazima tuwe na sheria nzuri, mbinu nzuri na mkakati mkubwa juu ya kulinda rasilimali zetu. Kama hatujajiandaa kwenye kodi, inanishangaza sana, ina maana tutaendelea kupiga kelele,” anasema Mwamalanga.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amepangua hoja hizo akisema kuwa serikali haijawapuuza wazawa.
“Katika andiko letu tumeandika, nawahimiza mkalinunue, tumewagusia wazawa ambao watahusishwa katika ununuzi wa vitalu. Hakuna aliyesema kuwa sekta binafsi haitashirikishwa,” anasema Maswi.
Aliukosoa pia mtindo wa uwekezaji wa Nigeria ambao Mengi ameupendekeza:
“Mengi, kaka yangu, nakwambia mtindo wa Nigeria siyo mzuri… Huwezi kuwapa watu wachache rasilimali wakati wengi wakiwa kwenye umaskini. Nigeria imejaa vurugu na hatuwezi kuichukulia kama mfano mzuri,” anasema.
Akijibu hoja ya viongozi wa dini iliyotolewa na Mchungaji  Mwamalanga, Maswi amewataka viongozi hao kushirikiana na serikali badala ya kuinyooshea kidole.
 “Tatizo la nchi yetu, watu ni kulalamika tu, fanyeni kazi... Mkitusaidia maaskofu, tutatoka hapa tulipo, siyo kutunyooshea tu vidole. Maaskofu wenyewe wanakula rushwa, wanafanya vitu vya ajabu, mbona sisi hatuwanyooshei vidole?
Au tuwataje? Kwa sababu msione tu serikali ni watu wabaya, no, let’s work as a team.”(Njooni, tufanye kazi kama timu.)