Watoto hawa ni miongoni mwa watoto wengi wanaofanya kazi za kugonga kokoto na kuchonga matofali kisiwani Pemba. Watoto wengi wanatumikishwa katika ajira hiyo ngumu, huku wakikosa haki yao ya kupata elimu. Picha na Talib Ussi. Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto, zaidi ya watoto 15,000 wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitimiza miaka 50 tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyojenga mazingira mazuri ya maendeleo, visiwa vya Unguja na Pemba vimeathirika na ajira ngumu zinazowahusisha watoto.
Hicho ni kikwazo kinachoweza kuifanya Zanzibar ishindwe kuyafikia Malengo ya Milenia, ambayo yanataka hadi kufikia mwaka 2015 watoto wote wapate fursa na haki za msingi za elimu.
Vichocheo vya ajira kwa watoto
Kwa Zanzibar sababu ni nyingi, ikiwamo wazazi kutokuwa na mwamko wa kuwasomesha watoto wao na kutamalaki kwa umaskini katika familia nyingi.
Hata hivyo, wapo wazazi walioamua tu kuwatumikisha watoto wao katika ajira ngumu, huku wakisingizia kuwa wanafanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto, zaidi ya watoto 15,000 wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) ambacho ni sehemu ya washiriki wa mradi, Sheha Haji Dau, anasema waliwatembelea watoto zaidi ya 264 na kubaini 80 wanaishi katika mazingira hatarishi kwa kujishughulisha na ajira ngumu.
Baada ya kuwabaini anasema wamekuwa wakihakikisha wanarudi shule kama anavyosema: “Kijiji cha Charawe pekee watoto 16 wamerudishwa shule. Wanaendelea vizuri na masomo, huku tukitoa elimu kwa wazazi wafuatilie maendeleo yao. ‘’
Kisiwa cha Pemba kinatajwa kuathirika zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hata ndani ya familia zao.
Mratibu wa asasi ya kiraia inayoshughulikia mapambano ya ajira ngumu za watoto katika Mkoa wa Kaskazini Pemba (Kukhawa), Mgeni Hamad Othman anasema ajira za watoto zimerudisha nyuma maendeleo ya sekta ya elimu katika kisiwa cha Pemba. ‘Mkoa wa Kaskazini ambapo naufanyia kazi, ajira mbaya za watoto zimetawala na kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu kwa maendeleo ya Taifa,’’ anasema.
Hata hivyo, anashukuru kuwa kupitia mradi huo wa miaka mitatu, wamefanikiwa kuwarudisha shule watoto 106 wanaosoma katika shule mbalimbali.
Akitoa mfano wa watoto katika maeneo ya Mwambe, vitongoji na Micheweni, anasema watoto wamekuwa wakifanya kazi za kugonga kokoto na uchongaji wa matofali.
Mkazi wa Mwamba, Mcha Makame Bahani anawasimamia watoto wapatao saba anaosema, asubuhi wanafanya kazi ya kugonga kokoto ili wapata fedha za matumizi, kisha baadaye wanakwenda shule.
‘Ni kweli ajira za watoto kugonga kokoto zipo Mwamba kwa wingi, lakini sababu kubwa tunakabiliwa na umaskini uliokithiri. Hatuna ajira na Serikali haijaweka mikakati ya kutuwezesha miradi midogo midogo,’’ anasema.
Naye mtoto Mariam Daud Hamad (16), anakiri kuwa kugonga kokoto ndiyo kazi yake ya kila siku kuanzia asubuhi hadi jioni. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa Mariam hakuwahi kupelekwa shule na wazazi.
‘Kwa siku nzima napata madebe 12 ambapo debe moja linauzwa kwa Sh150 mimi sijapelekwa shule lakini nikipelekwa nipo tayari kusoma,’’anaeleza.
Kwa upande wake mchuuzi katika soko la Wesha, lililopo Chakechake, Kai Kombo Omar anasema iliwachukua miezi sita kuwapiga marufuku wanafunzi wa shule 27 waliokuwa sokoni hapo kuparua samaki.
‘Sisi katika soko la Wesha tumefanikiwa na kukomesha ajira mbaya kwa watoto, kama unavyoona hakuna mtoto hapa anayefanya kazi za kuparua samaki na kuchukuwa mizigo,’’ anaeleza.
Mratibu wa Kukhawa anasema katika utafiti walioufanya katika Shehia moja tu ya Mwambe, watoto 280 wamebainika kufanya kazi ngumu, ambapo asasi yake imo mbioni kuwasaidia na kuwarudisha shule.
‘Ajira za watoto ni changamoto kubwa Pemba kutokana na familia kukabiliwa na hali ngumu ya maisha, sasa sijuwi itakuwaje mradi huu utakapomaliza muda wake,’’anasema.Ofisa Mwandamizi wa asasi ya Piro, inayojihusisha na watoto walio kwenye ajira mbaya katika Wilaya ya Micheweni, Sada Hamad Mbarouk anasema wilaya hiyo imeathirika kwa kiasi kikubwa.
‘Wilaya ya Micheweni Pemba imeathirika na ajira mbaya za watoto, ambapo tayari tumewafikia zaidi ya watoto 562 ambao wamerudi shule,’’ anasema.
Watoto wanaorudishwa shule wamekuwa wakisaidiwa madaftari,viatu pamoja na vifaa vyote vya kujifunzia.
Ali Musa anafurahi kurudi shule baada ya kipindi kirefu cha kukacha masomo na kwenda kufanya kazi. Anasema: “Nimerudi shule zaidi ya miezi sita sasa baada ya kutoroka, ambapo nimepokelewa vizuri na walimu na kupata ushirikiano mkubwa.’’
Waziri wa Uwezeshaji Wananchi, Wanawake, Vijana na Watoto, Zainab Omar Mohamed , anakiri kuwepo kwa watoto wanaotumikishwa katika ajira ngumu.
Hata hivyo, anaeleza kuwa sheria za Zanzibar na mikataba ya kimataifa inapiga marufuku ajira hizo, ambapo wazazi wanaobainika huchukuliwa hatua za kisheria.
‘’Serikali inapiga marufuku ajira mbaya za watoto zenye madhara, ambazo husababisha wakose fursa mbali mbali ikiwemo elimu. Tupo katika mikakati ya kupinga ajira hizo,’’ anasema Waziri Mohamed.
|
0 Comments