Dar es Salaam.Dereva wa Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC), Ramadhani Gize ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam akiwa njiani kwenda kuchukua wafanyakazi kuwapeleka kazini.
Ramadhani alipigwa risasi wakati akienda nyumbani kwa mtangazaji wa kituo hicho,Shaaban Kisu aliyekuwa zamu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni,Camillus Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa 3:45 juzi usiku baada ya majambazi manne wakiwa na silaha kuvamia duka la Namanga
Shopping lililopo Ubungo na kumlazimisha mmiliki wa duka hilo, Amdan Rajab kutoa fedha.
Alisema majambazi hao walipora fedha kiasi ambacho hakikufahamika pamoja na vocha za mitandao mbalimbali ya simu zenye thamani ya Sh400,000.
“Wakati tukio likiendelea,Mwagize alikuwa amepaki gari karibu na duka hilo na alipokuwa akitaka kuondoka mmoja wa majambazi alimfyatulia risasi zilizompata kichwani na alipoteza maisha akiwa njiani kuwahishwa hospitali,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema wakati majambazi hayo yakifanya tukio hilo waliliona gari la TBC likiwa eneo hilo na inawezekana walihofia kupigwa picha ndipo walichukua uamuzi huo wa kupiga risasi kioo cha mbele cha gari hilo na kumpata kwenye kichwa dereva huyo,” alisema Wambura.
Alisema risasi hizo pia zilimpata na kumjeruhi mtu mwingine,Mharami Rajabu (25) aliyekuwa anataka kuegesha gari lake karibu na eneo la tukio aliyewahishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili anakoendelea na matibabu.
Kamanda Wambura alisema, polisi wanaendesha msako mkali kuwasaka wahusika na kusisitiza wananchi kushirikiana katika kuwafichua wahalifu.
Baba mzazi alonga
Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwa marehemu,baba mzazi wa dereva huyo, Athumani Mwagize alisema mwili wa marehemu utasafirishwa leo kwenda kijijini kwao Mgole, wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwa maziko.
Naye Mkurugenzi wa TBC, Clement Mshana aliiambia Mwananchi: “Nimeshtushwa na tukio hili lakini ninaamini polisi watafanya kazi yao na wote waliohusika watakamatwa.”
0 Comments