Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma Kikwete wakiongea na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue mara baada ya kuwasili jijini Colombo, Sri Lanka, leo Novemba 14, 2013 tayari kwa mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya ya madola (CHOGM).PICHA NA IKULU Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Colombo, Sri Lanka, leo, Alhamisi, Novemba 14, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Rais Kikwete ambaye anaandamana na Mama Salma Kikwete amewasili mjini Colombo, mji mkuu wa Sri Lanka, asubuhi ya leo, akitokea Dubai ambako aliwasili usiku wa jana akitokea nyumbani.
Mkutano huo wa siku tatu unaanza kesho, Ijumaa, Novemba 15, 2013, kwenye Ukumbi wa Mahinda Rajapaska Theatre katika eneo la Nelum Pokuna mjini Colombo, mji mkuu wa Sri Lanka.
Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Prince Charles, mtoto wa Malkia wa Uingereza, kwa niaba ya mama yake, Malkia Elizabeth ambaye ndiye kiongozi wa Jumuiya ya Madola, ambaye hata hivyo, hataweza kuhudhuria mkutano wa mwaka huu.
Mara baada sherehe za ufunguzi, Rais Kikwete ataungana na viongozi wenzake kwa ajili ya vikao rasmi vya mkutano huo vitakavyofanyika kwenye Kituo cha Maonyesho ya Kumbukumbu cha Sirimavo Bandaranaike.
Miongoni mwa shughuli kubwa za kesho ni vikao viwili rasmi vya kwanza vya viongozi wa Jumuiya hiyo na majadiliano kati ya viongozi hao na viongozi wa vijana kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Aidha, viongozi hao wa Jumuiya ya Madola akiwamo Rais Kikwete watahudhuria hafla rasmi ya makaribisho itakayoandaliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Kamalesh Sharma katika Ukumbi wa Bandaranaike Memorial International Conference Hall (BMICH).
Baadaye leo, Rais Kikwete na Mama Salma, watahudhuria Hafla ya Chakula cha Usiku kitakachoandaliwa na Prince Charles na mkewe, The Duchess of Corwall, kwenye Hoteli ya Cinnamon Lakeside.
Jumuiya ya Madola ni umoja wa nchi zilizokuwa chini ya ukoloni na himaya ya Uingereza na nchi nyingine ambazo zenyewe ziliomba na kukubaliwa kujiunga na Jumuiya hiyo ikiwamo Mozambique na Rwanda.
Jumuiya ya Madola ina jumla ya nchi wanachama 53, zikiwamo nchi 18 za Afrika ambalo ni Bara lenye wanachama wengi zaidi katika Jumuiya hiyo, nchi nane za Asia, nchi 13 za Marekani na Caribbean, nchi tatu za Ulaya na nchi 11 za Pacific.
Jumuiya hiyo pia ina mchanganyiko wa nchi kubwa na ndogo, nchi 32 kati ya hizo zilihesabiwa kama nchi ndogo kwa maana ya kuwa idadi ya watu milioni 1.5 ama chini ya hapo.
Sri Lanka ambayo mpaka mwaka 1972 ilijulikana kwa jina la Ceylon, inajulikama rasmi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka. Ni nchi kisiwa kilichoko kaskazini mwa Bahari ya India na Kusini mwa pwani ya nchi ya India. Ni nchi yenye mipaka ya maji na India na Maldives.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Novemba, 2013 |
0 Comments