Watu wakikatiza mbele ya vifusi na mabaki ya majengo yaliyobomolewa na kimbunga kwenye Kisiwa cha Leyte jana, siku tatu baada ya kimbunga Haiyan kulikumba eneo hilo.
Leyte, Ufilipino.Zaidi ya watu 10,000 wamepoteza maisha Ufilipino katika kisiwa kimoja kati ya vitatu vya nchi hii kutokana na kimbuga kikali.
Licha ya kwamba tayari idadi hiyo inalifanya janga hilo kuwa la kihistoria, idadi hiyo inaweza kuongezeka hasa kutokana na ukweli kwamba visiwa vingine havijafikiwa na kufanyiwa tathmini.
Pamoja na vifo hivyo, zaidi ya watu 800,000 wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya kutolewa kwa tahadhari ya kukabiliana na kimbunga hicho cha Haiyan.
Mabaki ya miili ya watu waliofariki dunia kutokana na kimbunga hicho imetapakaa kila mahali, ikiwamo juu ya miti na kwenye magofu ya majengo na vifaa vingine vilivyoharibiwa kwenye mji wa Leyte.
Licha ya zahama hiyo, wahalifu wameripotiwa kutumia mwanya wa gharika hiyo kuvamia maduka, baa na vituo vya mafuta wakitafuta vyakula, mafuta na maji.
Katika Mji wa Talcoban imeripotiwa kwamba zaidi ya watu 200,000 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula na maji na hiyo ndiyo sababu ya walionusurika kufanya uporaji.
Tayari vikosi vya ulinzi na usalama vimeshatawanya katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kuzuia uharibifu na uhalifu huo ambao umeanza kushika kasi. Kimbunga hicho kilianzia Mashariki na kuelekea Magharibi mwa Ufilipino.
Baadhi ya picha za video zinaonyesha jinsi watu walivyokuwa wakivamia, kuvunja na kuiba kwenye baa, maduka ya vyakula na mashine za kuhifadhia fedha kwenye mji huo ambao hadi jana, haukuwa na uhakika wa usalama.
Katika hospitali moja pekee iliyonusurika kwenye mji huo, madaktari walishindwa kupokea majeruhi kutokana na wingi huku wengi walioumia wakiwa wametelekezwa kwenye maeneo yanayozunguka hospitali hiyo.
Kimbunga hicho kilichoanza kuyakumba maeneo kadhaa nchini humo Ijumaa iliyopita kilisababishwa na upepo mkali wa baharini uliofanya maji ya bahari kukimbilia nchi kavu.
Japokuwa nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na majanga ya kiasili ikiwamo milipuko ya volkano, matetemeko ya ardhi na vimbunga mara kadhaa, kimbunga Haiyan ndicho kilichovunja rekodi kwa kusababisha uharibifu mkubwa na vifo vingi kuwahi kutokea katika historia.
“Nikiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege nilishuhudia miili mingi ya watu waliokufa ikiwa imetapakaa barabarani. Ilikuwa imezagaa kwenye eneo lenye mabaki ya mapaa ya nyumba, mabaki ya kuta na miti iliyong’oka.