Stori:  Jelard Lucas
 Sikia, kama ulikuwa hujui ni kwamba msanii mkongwe katika filamu za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’ ameibuka na kueleza mengi ikiwemo kutoa mimba ya mpenzi wake wa siku nyingi, Vincent Kigosi, tulia hapohapo.Mbali na uhusiano wao huo uliokuwa ukifanywa siri, Mainda ameeleza kwa machungu jinsi Ray alivyomtesa kwa kumchanganya na wasanii wenzake, Blandina Chagula ‘Johari’ na Chuchu Hans ambaye ni mke wa mtu.
Risasi Mchanganyiko lilipata wasaa wa kufanya naye mahojiano ‘exculusive’ kwa saa moja na dakika tano, wikiendi iliyopita, makao makuu ya gazeti hili, Mwenge – Bamaga, jijini Dar.
Hata hivyo, alisema uhusiano wao kwa sasa umevunjika rasmi huku akibainisha jinsi alivyonyooshewa vidole na watu wakiamini kwamba aliambukizwa Ukimwi na aliyekuwa mpenzi wake kabla ya Ray, marehemu Said Maulid Banda  ‘Maxi’.
Soma mwenyewe mahojiano yalivyokuwa mstari kwa mstari, neno kwa neno:Risasi: Baada ya kifo cha Maxi, Ray alijitokeza na kukutongoza au siyo?
Mainda: Hapana, nakumbuka ilikuwa Siku ya Valentine’s Day mwaka 2004...sikumbuki kama tulitongozana ama vipi lakini ilitokea tukajikuta kwenye uhusiano.

Risasi: Umedumu kwa muda gani katika uhusiano wako na Ray?
Mainda: Miaka tisa, nilimpenda sana hata yeye alikuwa akinipenda na kuniheshimu sana.
Risasi: Kwa nini mmeachana?
Mainda: Hajaniacha wala hatujaachana. Miye ndiye nimemwacha.Risasi: Jeuri ya kumuacha Ray umeitoa wapi?
Mainda: Siyo jeuri, ni kujiamini na kujitambua tu.
Risasi: Chanzo cha kumuacha nini labda?
Mainda: Nilipojihakikishia kwamba anatoka na Chuchu Hans na Johari, nikafanya uamuzi.
Risasi: Lini ulipata uhakika huo?
Mainda: Ni hivi karibuni. Niliumia sana (analia).
Risasi: Pole sana, jikaze tafadhali. Siku zote ulikuwa hujui?
Mainda: Nilikuwa nasikia tu maneno, lakini nilipothibitisha nikaamua kukaa pembeni.
Risasi: Uhusiano wako na Ray ulifikia hatua gani?Mainda: Mwaka 2009 miye na Ray tulienda kanisani kwa ajili ya kutaka kufunga ndoa. Kwa sababu  mwenzangu ni Mkatoliki ilibidi aokoke na kunifuata kwenye wokovu ili tuweze kufunga ndoa yetu, nashangaa amebadilika tena.
Risasi: Ulibadili dini kwa ajili yake?
Mainda: Big no! (Hapana kabisa) ulikuwa ni uamuzi wangu binafsi.
Risasi: Mipango yenu ya ndoa ilikuwaje?
Mainda: Tulipanga kufanya private wedding (ndoa ya siri).
Risasi: Unauzungumziaje uhusiano wako na Ray? Namaanisha ni nini hasa ambacho hakitaweza kufutika kirahisi katika kumbukumbu zako?
Mainda: Daah! (anavuta pumzi ndefu kisha anazishusha) Nilimpenda sana Ray. Ilifikia hatua nikapata mimba yake. Mapenzi yetu yakaongezeka lakini kwa bahati mbaya ilitunga nje ya kizazi na ilinitesa sana, tena kwa kuwa ilikuwa ni mimba ya kwanza sikuwa nimejitambua mapema. Madaktari wakashauri niitoe, nikakubaliana nao.
Risasi: Ilikuwa ni mwaka gani?
Mainda: Sikumbuki, ila ni kipindi tulipokuwa tukirekodi filamu iitwayo Johari (kwa kumbukumbu za Risasi ni mwaka 2005).
Risasi: Kuna madai kwamba wewe hukubaliki kwa mama yake Ray, ambaye anadaiwa anamkubali zaidi Johari, ni kweli?
Mainda: Siwezi kumsema vibaya yule mama, namheshimu sana lakini inawezekana kuna maneno ya uongo ambayo ameambiwa na watu.
Risasi: Kama yapi?
Mainda: Kuhusu miye kuwa na Ukimwi. Ngoja nikuambie kitu kaka’ngu, baada ya kifo cha Maxi, watu wengi walininyooshea vidole kwa kuamini kuwa Maxi amekufa kwa ugonjwa huo jambo ambalo siyo la kweli. Nakumbuka mwaka 2003, nilienda na Maxi Mwananyamala (Hospitali), alitolewa vipimo vingi (kikiwemo cha VVU), akabainika kuwa na kansa ya damu.
Akatakiwa kwenda Ocean Road (Hospitali) ambako walipendekeza akatwe mguu uliokuwa umeathirika na ugonjwa huo lakini alikataa. Alisema ni heri afe kwa ugonjwa huo kuliko kuzikwa akiwa na upungufu wa viungo mwilini mwake.
Risasi: Kuna tiba alishaanza kuitumia Ocean Road kabla ya kifo chake?
Mainda: Yeah! Alikuwa akichomwa mionzi, hadi kifo kilipomfika.
Risasi: Pole sana.
Mainda: Ahsante... ila baada ya kifo chake, watu wengi walihisi amekufa kwa Ukimwi na wakaamini nami pia ni mwathirika... hiyo hali ilinitesa sana (anaangua kilio).
Risasi: Pole sana, usilie...jikaze tafadhali.
Mainda: Kama kweli Maxi angekuwa amekufa kwa Ukimwi, Ray asingekubali kuwa na mimi kwa sababu  alikuwa rafiki yake na alishiriki kumuuguza kwa kiasi kikubwa.
Risasi: Kwa hiyo unaamini kwamba mama Ray alipandikizwa sumu hiyo?
Mainda: Binafsi nilikuwa simfuatilii ila mwanaye alijitahidi kuniweka karibu na mama yake.
Risasi: Kivipi?
Mainda: Mara kadhaa Ray alikuwa akinipigia simu na kunitaka niongee na mama yake au ndugu zake, aliniweka karibu sana na familia yake.
Risasi: Umewahi kupima Ukimwi?
Mainda: Siyo mara moja, baada ya maneno hayo,  mwanzo nilipima kwa hofu kwa kuhisi labda wale madaktari wa Mwananyamala walinidanganya kwa vile nilikuwa mdogo.
Risasi: Majibu yako yanasomekaje?
Mainda: Namshukuru Mungu, nipo negative (hana uambukizo).
Risasi: Ulijisikiaje ulipogundua kuwa Ray anatembea na Johari na Chuchu?
Mainda: Awali sikujua na kila nilipomuuliza Ray alinikatalia.
Risasi: Kwa hiyo ulimwamini Ray?
Mainda: Sana, tena nilipokuwa naye alikuwa akiwapigia na kuweka loud speaker kisha kuwauliza kama walikuwa wapenzi, walikataa.
Risasi: Unawachukuliaje Johari na Chuchu?
Mainda: Kwangu nawaona wapumbavu na wasiojiamini katika mapenzi. Mfano kama Ray angenipigia simu na kuniuliza kama natembea naye, ningekubali bila ya wasiwasi. Walikuwa wakijua kama miye natembea na Ray lakini kwa nini wao walifanya mapenzi yao na Ray kuwa ya siri? Mfano Chuchu alikuwa akiniita first lady na aliniambia kuwa Ray ananipenda sana, kumbe kuna kitu alikuwa akinificha.
Risasi: Chuchu alikuwa rafiki yako?
Mainda: Hapana ila alikuwa akipenda kunipigia simu na kujiaminisha kwangu kwamba alikuwa na Ray na hakuna kibaya kitakachotokea.
Risasi: Ulijuaje kama Ray anatambea na Chuchu?
Mainda: Inasikitisha kwa kweli, kwanza Chuchu ni mke wa mtu, (jina la mume kapuni) kisha amezaa na mumewe mtoto mmoja lakini anatangaza mtoto huyo ni wa Ray. Anamuweka kwenye mitandao, unadhani baba yake wa kweli anajisikiaje?
Halafu inasemekana walipokwenda Mbeya na Bongo Muvi, Chuchu alilala chumba kimoja na Ray.
Risasi: Uliambiwa na nani?
Mainda: Kuna msanii mmoja anaitwa (jina kapuni) ambaye naye alikuwa akitembea na Chuchu, ndiye aliyeshuhudia Chuchu akiingia chumbani kwa Ray. Pia ndiye aliyemfumania Chuchu na Ray Msasani hivi karibuni.
Risasi: Inadaiwa siku Ray na Chuchu walipofumaniwa, ulikuwepo na ukapandisha mashetani, ni kweli?
Mainda: Siyo kweli, sikuwepo ila siku hiyo (anamtaja jina huyo jamaa) aliniletea simu za Chuchu ambazo zilikuwa na meseji alizokuwa akichati na Ray. Halafu Chuchu ndiye mwenye tabia ya kupandisha mashetani.
Risasi: Meseji za Ray kwa Chuchu zilikuwa zinasemaje?
Mainda: Mambo ya mapenzi tu, tangu hapo niliamini kwamba Ray alikuwa akitembea na Chuchu. Nikaamua rasmi kumuacha Ray aendelee na Chura wake!
Risasi: Kwa nini unamwita Chuchu Chura?
Mainda: Wenyewe ndivyo wanavyojiita yaani ni kifupi cha Chuchu (Chu) na Ray (Ra) badala ya RJ (Ray na Johari).
Risasi: Ray alijiteteaje kwako?
Mainda: Alidai kwamba simu yake ilikuwa ikitumika na rafiki yake mwingine ambaye ni mume wa mtu (jina tunalo) akidai kwamba ndiye aliyekuwa akitembea na Chuchu lakini si kweli.
Risasi: Kama leo hii Ray akikufuata na kukuomba radhi utakubali kurudiana naye?
Mainda: Ameshaomba radhi sana, hata Chuchu alishaniomba radhi na kudai kutorudia lakini mambo ni yaleyale.
Risasi: Hebu fafanua?
Mainda: Ninaujua msururu mrefu wa wanawake wa Ray, (akaanza kuwataja majina - wamo wanenguaji na wasanii wa filamu na wengine), mmoja kwa sasa ni mke wa mtu huyo sitakutajia jina lake.
Risasi: Jambo jingine?
Mainda: Sijui kama ulisikia, Ray alipata ajali na Chura wake hivi karibuni?
Risasi: Nilisikia!
Mainda: Hiyo nayo inatosha kuthibitisha ninachokisema. Hizi zote ni laana, tukio lingine ni lile la Johari kumfumania Ray akiwa na Chura.
Risasi: Hata hilo nililisikia na liliripotiwa, vipi kuhusu Johari?
Mainda: Johari naye alikuwa akinifuatilia nyendo zangu, kuna wakati nilivaa pete ya uchumba, alihaha kutaka kujua nimevalishwa na nani?
Risasi: Alijua Ray amekuvisha?
Mainda: Nadhani!
Risasi: Ni kweli?
Mainda: Tuyaache hayo.
Risasi: Kwa nini?
Mainda: (Akionesha msisitizo) tafadhali hilo tuliache kaka.
Risasi: Uliwahi kumsaliti Ray?
Mainda: Katika maisha yangu miye ndiye huumizwa kila siku. Baada ya kuwa na Maxi mwanaume mwingine ni Ray, sikuwahi kuwa na mwingine kabla na baada ya kuwa na uhusiano naye.
Risasi: Mwanaume gani alikuingiza katika dunia ya mapenzi?
Mainda: Aaah! Sitapenda kumtaja ilikuwa kabla sijakutana na Maxi.
Risasi: Unazungumza vizuri na Johari na Chuchu?
Mainda: Sina ugomvi nao, ila sikupenda kitendo cha kuchanganywa nao kwa mwanaume mmoja. Imeniuma sana, kwa kweli sipendi kuishi mitala.
Risasi: Unaionaje Bongo Muvi baada ya miaka mitano?
Mainda: Kwanza naomba Mungu aiangamize... unafiki mwingi sana. Kuna siku nilimuuliza Ray kama yeye ndiye mwenyekiti anafanya uchafu kama huu, anaweza kumkemea msanii mwingine? Hakunijibu kitu. Mengi mabaya yanayosemwa kuhusu Bongo Muvi  ni ya kweli, tena uongozi umeoza kuanzia juu mpaka chini.
Risasi: Baada ya kuachana na Ray una mwanaume mwingine?
Mainda: Wengi wamenipigia simu kunitongoza nikawachomolea wakiwemo wasanii waliokuwa wakijua uhusiano wangu na Ray.
Risasi: Kwa nini?
Mainda: Miye huwa sitongozwi kwenye simu.
Risasi: Unatongozwaje?
Mainda: (kicheko), sikia ninaye mtu wangu lakini hatujafikia hatua ya kufanya mapenzi, tunachunguzana ili kujuana tabia kwanza.
Risasi: Ni msanii wa filamu au?
Mainda: Siyo msanii, ni mtu anayejiheshimu.
Risasi: Mara yako ya mwisho kufanya mapenzi ilikuwa lini?
Mainda: Siku chache baada ya msiba wa Albert Mangweah (msanii wa Bongo Fleva).
Risasi: Unaamini iko siku utaolewa?
Mainda: Yeah! Tena nitajifungua watoto.
Risasi: Kitu gani ambacho huwezi kukisahau maishani mwako?
Mainda: Kifo cha Kanumba na marehemu Maxi  (anaangua kilio…) vifo vyao viliniuma sana na vimeshindwa kuondoka akilini mwangu kirahisi.
Risasi: Ahsante sana kwa ushirikiano wako Mainda. Karibu tena Global Publishers.
Mainda: Nashukuru sana lakini nasema hivi; kama  Ray, Johari na Chuchu watakanusha haya niliyoyasema, nipo tayari nikutanishwe nao tena hapahapa ofisini kwenu nitazungumza mbele yao. Naahidi nitaongea mengi zaidi.
Risasi: Sawa, nashukuru sana Mainda.
Mainda: Nanyi pia… ndiyo maana nayapenda magazeti yenu.
Risasi: Kwa nini unasema hivyo?
Mainda: (Kicheko).