Rais Benjamini Mkapa akizungumza wakati wa mkutano wa kujadili Uwezeshwaji wa Afrika katika umiliki wa uchumi wake ambao uliandaliwa na Taasisi ya Tanzania Professional Forum (Tanpro) na kufanyika Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Jaji Mstaafu, Raymond Mwaikasu. Phicha na Joseph Zablon
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amesema kufa kwa Azimio la Arusha kwa sehemu kubwa ndiko kulikosababisha kuporomoka kwa maadili na kushamiri kwa rushwa.
Mkapa aliyasema hayo jana kwenye Mkutano wa marais wastaafu ulioandaliwa na Uongozi Institute, na kusema rushwa imekuwa tatizo kwa maendeleo na kwamba hakuna kinachofanyika bila rushwa.
Alisema, sehemu kubwa ya viongozi wanashindwa kuwajibika huku wakikimbilia kujilimbikizia mali na utajiri wa haraka na zaidi ni utajiri wa rushwa.
Mkapa alionya watu wajitume kuleta maendeleo ya kiuchumi badala ya kutumia muda mwingi kwenye siasa.
Akizungumzia suala la rushwa, Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo alisema alipokuwa madarakani alitumia muda mwingi kupambana na rushwa.
Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana alisema, rushwa kamwe haiwezi kwisha kwa kuwa viongozi, wanaorithi hufuata njia zilezile zisizofaa.
Wataka katiba ziheshimiwe
Mkapa alisema baadhi ya viongozi wa Afrika hawaheshimu katiba zilizowekwa kisheria kwa sababu wanazozijua wao.
Obasanjo alisema Katiba ya Nigeria inaheshimika na inalipa Bunge mamlaka ya kuhoji utendaji usio wa uadilifu wa Rais. Akizungumzia hayo, Rais Mogae alisema, Katiba ya Botswana iko wazi katika madaraka kuanzia ya urais na rasilimali za nchi ni kwa ajili ya wananchi na mapato yote ni kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Mogae kwa upande wake alisema, alipomaliza muda wake kikatiba, aling’atuka na hakutaka tena kuendelea na majukumu hayo ya kuitumikia nchi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa chama na Serikali, wakurugenzi na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi mbalimbali, wabunge na watu mashuhuri kutoka taasisi za kitaifa na kimataifa.
|
0 Comments