Mbunge wa Mfenesini (CCM), Suleiman Nassib Omar akiweka saini baada ya Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangala (kushoto) kuanza kukusanya saini za wabunge kwenye ukumbi wa bunge jana akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI
Dodoma:
 Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.
“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.
“Lazima walete maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema.Kadhalika alizungumzia suala la wabunge wengine kuteuliwa kuingia kwenye kamati ambazo si zao ambapo alisema, suala hilo pia ni la kawaida kwani hata katika mjadala unaoendelea wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ameongeza wajumbe wa ziada.
“Ninafanya hivyo kupanua wigo wa mjadala na mara nyingi kwa mfano kwenye kamati yetu ya Katiba nimeongeza wabunge wenye uelewa wa masuala ya sheria ili watusadie kufanya uchambuzi, maana unaweza kukuta kwenye kamati, watu wenye utaalamu kuhusu suala husika ni wachache. Kwa hiyo siyo kosa kwa mujibu wa Kanuni zetu,” alisema Makinda.

Ukusanyaji saini
Kwa upande wake Dk. Kingwangalla jana alikuwa akiendelea na ukusanyaji wa saini za wabunge huku akisema kuwa amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kupeleka bungeni hoja yake.
Ukusanyaji wa saini ulifanywa kwa kupitia fomu maalumu na kutoa taarifa kwamba wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi, wote wameshasaini katika fomu hizo.
Akizungumza jana katika viwanja vya Bunge, Dk Kigwangallah, alisema wabunge wa Chadema, walimweleza kuwa watafanya hivyo baada ya kukutana katika kikao cha pamoja.
Hata hivyo Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikiri kusikia taarifa hizo lakini akasema walikuwa bado hawajaketi kama kambi ili kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.
Jana asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Dk. Kingwangalla alionekana akipita katika baadhi ya meza za wabunge akiwashawishi kusaini fomu za kumuunga mkono.
Hadi jana mchana wabunge wa CCM, na CUF wapatao 30 tayari walikuwa wamesaini fomu hizo, wakimuunga mkono mbunge huyo.
Alipoulizwa ulazima wa kukusanya saini za wabunge wakati kanuni hazimtaki kufanya hivyo alisema, hilo linamwezesha kujua nguvu aliyonayo katika kumuunga mkono kuhusiana na suala hilo.
Hoja zake Katika taarifa ya kusudio lake ambalo Mwananchi imebahatika kuliona, Dk. Kingwangalla alisema uteuzi wa Serukamba ni kinyume na masharti ya kanuni ya 116(3) na (4).
Alisema Juni 27, 2013, wakati wa kutunga sheria ya fedha, Spika aliagiza kwa mabavu kuwa wabunge wote wenye majedwali ya mabadiliko waende kwenye kamati ya bajeti.
“Uamuzi huu wa Spika ni wa kidikteta na unapingana na masharti ya kanuni ya 88 ya kanuni za kudumu za Bunge ambapo kwa ufupi ni kwamba majedwali ya mabadiliko hujadiliwa bungeni wakati wa kamati ya Bunge zima na huamuliwa kukubaliwa ama kukataliwa na Bunge zima na si kamati yoyote ya Bunge,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya kuipa mamlaka makubwa kamati hiyo ni kuondoa mantiki ya uwepo wa Bunge lilopewa mamlaka ya kutunga sheria zote za nchi na Katiba ibara ya 63 (3) ( c) na (d ).
Pia alisema Spika Makinda amekuwa wa kwanza kuvunja masharti ya kanuni anazopaswa kuzitilia nguvu kama anavyoelekezwa na kanuni ya 5 (2). Amevunja pia kanuni na hivyo anastahili kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa masharti ya kanuni hizi ili kukidhi masharti ya Ibara ya 84 (7) (d) ya katiba ya kumwondoa madarakani.
Alitoa mfano wa hoja ya dharura iliyotolewa wakati MV Skagit ilipozama Julai 18, 2012 na siku zilipowasilishwa hoja mbili zinazohusiana na mauaji ya kwenye vurugu zinazohusu migogoro baina ya jamii za wakulima na wafugaji na wanyang’anyi wa mali na unyanyasaji wa wafugaji unaofanywa kwenye operesheni tokomeza ujangili.
Katika kuhitimisha taarifa hiyo, Dk Kingwangalla alisema: “Ni maoni yangu binafsi na ya wabunge wengi wanaoniunga mkono kuwa Spika wa Bunge Anne Makinda apumzishwe kazi kwa tuhuma nilizozitaja hapo juu.”