Baraza la Usalama la umoja wa mataifa limeidhinisha kutumwa maelfu ya majeshi ya Afrika na wa Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Hali imeendelea kuwa mbaya nchini humo huku mapigano yakichacha usiku kucha na leo mchama mzima. Takriban watu 80 wameripotiwa kuuawa kwenye mapigano makali mjini Bangui Alhamisi.Mji huo ulivamiwa na wafuasi wa Francois Bozize aliyeng'olewa mamlakani na waasi mwezi Machi hali iliyotumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa.
Mapigano makali ya kurushiana risasi na silaha nzito nzito yalishuhudiwa mapema leo katika mji wa Bangui kabla Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kupeleka majeshi ya kutoka Afrika na Ufaransa.
Mwandishi wa habari wa BBC aliyepo katika mji wa Bangui anasema aliona magari ya kivita yakiendeshwa kupita katika mitaa na kwamba watu wengi bado wamejifungia majumbani mwao.
Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Gerald Araud ameiambia BBC kuwa kuongezwa majeshi ya kimataifa utasaidia hali ya usalama ndani ya wiki chache.
Bwana Araud amesema Majeshi ya Umoja wa Afrika na yale ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kusimamia sheria na utulivu katika mji wa Bangui kabla ya kuangalia usalama katika miji mingine nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati.
0 Comments