Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Hayati Tata Nelson Mandela, Mungu awalaze mahali pema, hakika Afrika na dunia nzima itaendelea kuwakumbuka Daima. Picha na Maktaba 

Pretoria.
 Familia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere itawakilishwa katika mazishi ya Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye atazikwa kesho katika Kijiji cha Qunu, Mthatha Jimbo la Eastern Cape.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana mjini Pretoria zinasema kuwa Mama Maria Nyerere, ambaye ni mjane wa Baba wa taifa, alialikwa kuhudhuria mazishi hayo kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina ya familia hizo mbili.
Hata hivyo, imethibitika kuwa Mama Maria hataweza kuhudhuria mazishi hayo kesho, badala yake amewatuma wawakilishi ambao ni mabinti zake wawili; Anna Nyerere ambaye ni mtoto wa pili na mtoto wake wa saba, Rosemary Nyerere.
Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa sita wa Mwalimu alithibitisha jana kwamba familia yao imealikwa kushiriki mazishi hayo, lakini akaweka wazi kwamba: “Mama hataweza kwenda kuzika, atakwenda baadaye kidogo baada ya mazishi kufanyika.”
Madaraka alisema kwa jinsi afya ya mama yake ilivyo sasa, hataweza kwenda Qunu. “Kwa kawaida mazishi haya ya kitaifa huwa yana mambo na pilika nyingi, kwa hiyo mama ameona asubiri,” alisema.
Kuhusu kifo cha Mandela, Madaraka alisema kwamba kama wanafamilia, wameguswa na msiba huo na kuwa kimewakumbusha uchungu walioupata wakati walipofiwa na baba yao Oktoba 14, 1999.
“Kwa kweli tumeguswa sana na msiba na tunawapa pole sana, tunakumbuka kwamba wakati baba alipofariki, Mama Graca tulikuwa naye, alikuja kabla ya mazishi na alikuwepo kwenye mazishi na baada ya mazishi aliendelea kukaa kwa siku kama saba,” alisema Madaraka na kuongeza:
“Pia tunakumbuka kwamba Mzee Mandela yeye alikuja baadaye mpaka Butiama kutoa pole. Ilikuwa Novemba 26, 1999 kwa hiyo tunaguswa na msiba huu.” Awali, gazeti hili lilidokezwa kwamba watoto hao wa Nyerere walikuwa wamefikia katika Hoteli ya Burgers Park, Pretoria lakini walipotafutwa katika hoteli hiyo wafanyakazi walisema kwamba tayari walikuwa wameondoka.