Rais wa Marekani,Barrack Obama.PICHA|MAKTABA
Wakati Nelson Mandela akihukumiwa mwaka 1964 alisema: “Nimepigana dhidi ya utawala wa kizungu, na nimepigana dhidi ya utawala wa watu weusi. Nimelifanikisha wazo la jamii yenye uhuru na demokrasia ambayo watu wote wanaishi pamoja kwa umoja wakiwa na fursa sawa. Ni wazo ambalo ninataka kuishi nalo na kulitekeleza, lakini kama itanilazimu, nipo tayari kufa.”
Nelson Mandela aliishi maisha yake katika msingi wa kitu alichokiamini, na kukifanya kionekane kwa jamii. Alipata mafanikio zaidi ya ambavyo ilitarajiwa. Leo, amekwenda nyumbani. Tumepoteza mmoja wa watu wenye ushawishi, jasiri na binadamu mwenye utu ambaye kila mmoja wetu angependa kushirikiana naye katika dunia hii. Hayupo pamoja nasi tena.
Kupitia utu wake na nia isiyotikisika ya kujitolea mhanga uhuru wake kwa ajili ya uhuru wa watu wengine, Madiba aliibadilisha Afrika Kusini na sisi sote. Safari yake kuanzia gerezani hadi urais inaelezea kwamba binadamu pamoja na nchi wanaweza kuleta mabadiliko yenye manufaa makubwa.
Nia yake njema ya kukabidhi madaraka na kutoa msamaha kwa wote waliomfunga inatupa mfano ambao kila mmoja anapaswa kujifunza katika ngazi ya kitaifa na hata kwenye maisha binafsi. Kwa sababu alifanya kila kitu kwa furaha na ucheshi, na akiwa na uwezo wa kujikosoa mwenyewe, hivyo zinamfanya aonekane kuwa mtu wa tofauti. Aliwahi kusema: “Mimi siyo mtakatifu, labda kama unamfikiria mtakatifu mtenda dhambi ambaye anaendelea kujaribu.”
Mimi ni miongoni mwa mamilioni ya watu ambao walivutiwa na maisha ya Nelson Mandela. Tukio langu la kwanza la kisiasa nililolifanya ambalo lilihusu sera au siasa lilikuwa ni mgomo dhidi ya ubaguzi wa rangi. Nilijifunza maneno na maandishi yake.
Siku ile ambayo aliachiwa kutoka gerezani ilinipa wazo namna ambavyo watu wanaweza kufanya wanapokuwa wanalindwa na tumaini na siyo hofu. Na kama ilivyo kwa watu wengi duniani kote, siwezi kufikiri kwa mapana maisha yangu yatakuwaje bila mfano ambao Nelson Mandela ameuweka. Kwa kuwa bado ningali hai, nitafanya kila linalowezekana kujifunza kutoka kwake.
Kwa Graca Machel na familia yake, Michelle na mimi mwenyewe tunatoa salamu zetu za maombolezo kwa namna walivyotushirikisha kuhusu Mandela. Ninatumaini kuwa muda walioutumia na Mandela wiki za mwisho zilileta amani na faraja kwa familia yake.
Kwa watu wa Afrika Kusini, tunajifunza kutoka kwa mfano wa kuheshimiwa, kupenda mapatano na uhuru wa kufikiri ambao mmeufanya. Afrika Kusini iliyo na amani, huo ni mfano kwa dunia, na ndiyo urithi wa Madiba kwa taifa alilolipenda.
Kuna uwezekano kwamba hatuwezi kuona tena mambo ambayo Nelson Mandela aliyapenda. Kwa hiyo ni wajibu wetu kuendeleza mfano ambao aliuweka. Kufanya uamuzi usiotokana na chuki, bali upendo; kwa kutambua tofauti ambayo mtu mmoja anaweza kuileta, kuupigania wakati ujao ambao una thamani sawa na sadaka aliyoitoa.
Kwa sasa, kupumzike kidogo na kushukuru kutokana na ukweli kwamba Nelson Mandela aliishi, mtu ambaye aliichukua historia mikononi mwake na kupindisha mazoea ya dunia kuhusu haki. Mungu aibariki historia yake na kumuweka katika amani.