Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane kutokana na tuhuma mbalimbali.
Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri kamili.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kutengua uteuzi wa mawaziri wanne alioufanya siku tisa zilizopita, mawaziri hao walishutumiwa kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Ripoti ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Waliong’olewa katika sakata hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David.
Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane kutokana na tuhuma mbalimbali.
Historia inaonyesha kuwa Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua, huku akiwapandisha naibu mawaziri kuwa mawaziri.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.
Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), na Saada Mkuya na Janet Mbene (wote ni Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha).
Kutokana na utamaduni huo, Dk Asha-Rose Migiro anapewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye baraza jipya la mawaziri, kwani naye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mbunge.
Wabunge ambao wameteuliwa na Rais lakini hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji, James Mbatia na Dk Asha-Rose Migiro.Waliopandishwa
Pia Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa mawaziri.
Amefanya hivyo kwa Dk Nchimbi ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo. Awali alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwingine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo wakati huo ikiongozwa na Shamsa Mwangunga.
Kagasheki pia alipandishwa kutoka naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hadi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Rais Kikwete alipoingia madarakani alimpandisha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Anthony Diallo kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
Mwingine aliyepandishwa ni William Ngeleja, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, baadaye alipandishwa kuwa waziri kamili katika wizara hiyo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk HarrisonMwakyembe aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuitumikia nafasi ya naibu waziri wa Wizara ya Ujenzi.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo baada ya kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Celina Kombani aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baadaye alipandishwa na kupewa Wizara ya Katiba na Sheria. Hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), ofisi aliyopewa kuiongoza tangu mwaka 2012.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Wasomi wanasema
Wakitoa maoni yao juu ya uteuzi wa mawaziri baadhi ya wasomi nchini wameitaka Idara ya Usalama wa Taifa kuhakikisha inapendekeza kwa Rais majina ya watu wazalendo, licha ya kueleza kuwa tatizo la uongozi linaathiriwa na mfumo mzima wa utawala.
Mchambuzi wa masuala ya Maendeleo na Sayansi ya Siasa, Emmanuel Mallya alisema, “Nchi yetu inatakiwa kuwa na viongozi wazalendo na wanaowatumikia wananchi kutoka ndani ya mioyo yao. Kiongozi ambaye hata akiondoka leo ataacha taswira ya namna nzuri ya kuongoza.”
Mallya ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) alisema kuwa pamoja na kuwa na kiongozi mzalendo, taifa linatakiwa kuwa na mfumo mzuri wa utawala: “Idara ya Usalama imshauri vyema Rais katika uteuzi huu.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Anaweza kuteua wapya, au akawapandisha naibu mawaziri kuwa mawaziri. Siwezi kutabiri ufanisi wa mawaziri kwa sasa maana mfumo wetu wa utawala ndiyo tatizo.”
Huku akitolea mfano Wizara ya Nishati na Madini na ile ya Maliasili na Utalii, Profesa Mpangala alisema zimekuwa zikibadilishwa watendaji kila mara, lakini kila anayeingia anaonekana hafai.
Vigezo vinavyoweza kuzingatiwa kuchagua mawaziri
Iwapo Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka, huenda nafasi iliyoachwa wazi na Nchimbi italazimika kujazwa na baadhi ya wabunge kutoka Mkoa wa Ruvuma ambao ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Mhandisi Stella Manyanya, Jenister Mhagama (Peramiho), Vita Kawawa (Namtumbo) au Mhandisi Ramo Makani (Tunduru Kaskazini).
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kuhusiana na uteuzi huo, Manyanya alisema kuwa watu wanaopendekeza jina la waziri huangalia vigezo vingi, siyo tu taaluma ya mtu au utendaji wake wa kazi.
“Watu hao hufanya kazi kwa siri kubwa, hata nilipochaguliwa kuwa Mkuu wa Mkoa sikufahamu hadi dakika ya mwisho,” alisema Manyanya.
Kwa upande wa nafasi iliyoachwa wazi na Kagasheki, wabunge kutoka Kagera wanaotarajiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uwaziri ni Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Deogratius Ntukamazina (Ngara), na Asumpta Mshama (Nkenge).
Nafasi iliyoachwa wazi na Dk David Mathayo, ambaye anatokea jimbo la Same Magharibi, mkoaniKilimanjaro, huenda ikampa Rais Kikwete wakati mgumu kumteua waziri miongoni mwa wabunge wa CCM waliopo mkoani humo kutokana na idadi yao kuwa ndogo.
Kati ya wabunge watano wa majimbo wa CCM waliopo Kilimanjaro, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ndiye pekee ambaye hajawahi kuteuliwa kushika nafasi ya uwaziri.Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe ni Waziri wa Maji, Mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi). Wengine ni Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Naibu mawaziri wanaoweza kupewa uwaziri kamili
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kama Rais ataamua kutumia utamaduni wake wa kupandisha naibu waziri kuwa mawaziri kamili, baadhi ya majina yanayotajwa huenda kuwa mawaziri kamili ni pamoja na
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey Mwanri, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Baadhi ya wabunge ambao majina yao yanatajwa kuwa huenda wakateuliwa kuwa mawaziri ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba na (CCM) na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Mawaziri waliohimili mitikisiko
Pamoja na kuwepo kwa panga pangua ndani ya baraza la mawaziri, wapo baadhi yao ambao wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni SofiaSimba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli. Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Dk Mary Nagu.
Katika baraza la mawaziri lake la kwanza, Rais Jakaya Kikwete alimteua Sofia Simba kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, mwaka 2010 alimhamishia Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ambako yupo hadi sasa.
Akizungumza na gazeti hili juzi kuhusiana na changamoto anazokutana nazo na kwanini amefaulu kudumu muda mrefu, Simba alisema kuwa anafanya kazi katika wizara ambayo haina ushawishi mkubwa kwa jamii, hivyo watu wengi hawapendi kuifuatilia namna inavyofanya kazi.
“Idara ya Maendeleo ya Jamii tunafanya vitu ambavyo havina interest kwa wananchi hasa waandishi wa habari, maana wao wanapenda kusikia habari za wizi na mambo mengine yanayotokea,” alisema Simba.
Aliongeza kwamba amekuwa na bahati ya kufanya kazi na watendaji wenye uwezo mkubwa na kwamba mawaziri walioondoka hivi karibuni waliangushwa na watendaji wao.“Kwa bahati mbaya wenzetu (mawaziri walioondolewa) wamepata watendaji ambao ndiyo hivyo tena,” alisema Simba.
Alipoulizwa kama anadhani ataendelea kuwepo kwenye Baraza la Mawaziri iwapo litafanyiwa marekebisho, Simba alijibu kuwa kila mbunge ni waziri mtarajiwa, hivyo inategemea Rais Kikwete anataka kufanya kazi na nani.
Naye, Profesa Mark Mwandosya mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, mwaka 2010 baada ya kufanyiwa marekebisho safu ya mawaziri aliteuliwa kuongoza Wizara ya Maji hadi mwaka 2012 alipoteuliwa kuwa Waziri asiye na wizara maalumu.
Waziri mwingine aliyefanikiwa kukaa muda mrefu na baraza la mawaziri ni StephenWassira, ambaye mwaka 2005 aliteuliwa kuongoza Wizara ya Maji, kisha mwaka 2008 alihamishwa Tamisemi. Miaka minne baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) nafasi anayoishikilia hadi leo.
Dk Hussein Mwinyi ni miongoni mwa mawaziri waliofanikiwa ‘kucheza’ namba mbalimbali ndani ya baraza la mawaziri bila kutoka nje ya uwanja.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa waziri aliyeshughulikia masuala ya Muungano, mwaka 2008 alipewa kuongoza Wizara ya Ulinzi na mwaka 2012 aliteuliwa kuiongoza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Kwa upande wake Profesa Jumanne Maghembe, mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, nafasi aliyoishika kwa miaka miwili hadi mwaka 2008 alipokabidhiwa mikoba ya kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mwaka 2010 alipewa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maji anayoiongoza hadi hivi sasa.
Katika baraza la kwanza la Kikwete, Dk John Magufuli aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, kabla ya kupewa wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mwaka 2010 alikabidhiwa Wizara ya Ujenzi.
|
0 Comments