Rais Jakaya Kikwete akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuhudhuria maadhimisho ya Miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), jana. Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya Watanzania katika maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania), kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kulihutubia taifa, akiwataka wananchi kuwa na moyo wa kusamehe kama aliokuwa nao Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza Desemba 9, mwaka 1961.
Katika maadhimisho hayo, mbali na karibu asilimia 90 ya hotuba ya Rais Kikwete kumzungumzia marehemu Mandela, aliamuru kusitishwa kwa shamrashamra za ngoma za asili kama ilivyozoeleka na badala yake ilikuwapo halaiki pekee.
“Kutokana na kuomboleza kifo cha Mandela, leo hatutakuwa na watu wa ngoma za asili. Nimeongea na walioandaa sherehe hizi na tumekubaliana kuwa watu wa ngoma watatumbuiza kipindi kingine,” alisema Rais Kikwete.
Mandela alifariki dunia nyumbani kwake Johannesburg, Afrika Kusini baada ya kusumbuliwa na maradhi ya mapafu kwa kipindi kirefu. Anatarajiwa kuzikwa katika kijiji alichokulia cha Qunu Jumapili ijayo.
Katika hotuba yake iliyochukua dakika 25, huku akitumia jina la ‘mtu muungwana’, Rais Kikwete alisema Mandela alikubali kusamehe na kukaa meza moja na wabaya wake.
Alisema licha ya kufungwa gerezani na kuteswa kwa kipindi cha miaka 27, aliporejea uraiani alionyesha moyo wa huruma na kuwasamehe waliomtesa.
“Kwa kawaida siku kama ya leo siyo ya kutoa hotuba, lakini kutokana na tukio kubwa tulilonalo, ningependa niseme machache kuhusu Mandela.
“Mandela alikuwa mtu wa aina yake na itatuchukua miaka mingi duniani kumpata kiongozi kama huyu. Alikuwa muungwana na kuwashangaza wengi kuanzia wale waliomtesa hata wale walioteswa. Alikubali kusamehe na hakutaka kulipiza kisasi.”
“Hapa najua tupo wengi tunaojiandaa kulipa kisasi, tunatakiwa kujifunza kwa Nelson Mandela.
Heshima aliyojijengea leo hii ndiyo inayosababisha mazishi yake kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo kutoka mataifa makubwa,” alisema.
Rais Kikwete alisema Mandela alikuwa kiongozi aliyeamini katika ukweli na wakati wote alipigania haki na uhuru wa watu weusi walionyanyaswa na kuteswa katika ardhi yao na kwamba daima alisimamia ukweli hata kama msimamo wake ulihatarisha maisha yake.Alisema Tanzania na Afrika Kusini zitaendelea kudumisha ushirikiano licha ya viongozi wa kidemokrasia wa mataifa hayo kutangulia mbele ya haki.
“Nataka niwakumbushe kwamba kwa mara ya kwanza Mandela alikuja nchini mwaka 1964 na alikutana na Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikubali kumsaidia kwenye mapambano ya kuikomboa Afrika Kusini. Baada ya hapo alikwenda zake Algeria kupata mbinu za kupambana na makaburu,” alisema Rais Kikwete.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Wengine ni Mawaziri Wakuu wa zamani, John Malecela na Edward Lowassa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Maadhimisho hayo yaliyoanza saa 2:30 asubuhi na kuhudhuriwa na umati mkubwa, yalipambwa kwa gwaride lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Asamehe wafungwa
Katika kuadhimisha siku hiyo, Rais Kikwete amesamehe wafungwa 1,475. Katika sherehe za mwaka jana, alisamehe wafungwa 3,814.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ilisema msamaha huo unawahusu wafungwa wote waliopunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao, wenye magonjwa kama Ukimwi, TB na kansa ambao afya zao ni mbaya na wamethibitishwa na daktari.
Wengine ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, walioingia gerezani na ujauzito pamoja na wenye ulemavu wa mwili na akili.
Msamaha huo haukuwahusisha wafungwa wa dawa za kulevya, rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, wizi, kubaka, kunajisi na kulawiti, unyang’anyi kwa kutumia silaha, waliowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kunyongwa, wanaotumikia adhabu ya kifo na kifungo cha maisha.
Mwinyi, Mkapa wakosekana
Hata hivyo, sherehe hizo hazikuhudhuriwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na haikuweza kufahamika mara moja sababu za kutokuwapo kwao.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na George Njogopa.