Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba akizungumza na waandishi wa Habri jijini Dar esSalaam jana wakati akitoa tamko la kulaani kwa kitendo cha Naibu Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuwanyanyasa na kuwazalilisha Wabunge wa upinzani akiwepo Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameitaka Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa matatizo ya kiuchumi, kwa kuwa hali ilivyo sasa ni mbaya.
Profesa Lipumba ambaye pia ni profesa wa uchumi alisema hivi karibuni Dar es Salaam kuwa hali ya uchumi imezidi kudorora na kusababisha maisha ya wananchi wengi kuwa magumu.
“Vijana wa siku hizi wengi hawana similekushughulika na mambo yanapokwenda sivyo, ajabu ni kwamba wanaofanya mambo hayo yawe magumu wamekuwa wepesi wa kutetea kwa hoja zisizo na msingi kwa masilahi yao binafsi,” alisema.
Akizungumzia maazimio yaliyofikiwa kwenye Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kilichofanyika Desemba 21-22 mwaka huu Dar es Salaam, alisema hatua ya kupandishwa kwa gharama za umeme iliyotangazwa hivi karibuni na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ni miongoni mwa mambo ambayo yanaendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi, jambo ambalo lingeweza kuzuilika kwa shirika hilo kudhibiti wizi wa nishati hiyo.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limetoa wito kwa vyombo vya Dola kuwa na weledi na uadilifu na kuacha kutekeleza amri za wanasiasa zisizojali utawala wa sheria na haki za binadamu ili vipunguze uhasama baina yao na raia.
“Serikali pia isitumie Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kushughulikia masuala ya uvunjifu wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, badala yake kazi hiyo ifanywe na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Nao pia waongezewe uwezo wa kiutendaji,” alisema.
Alisema CUF inaona si vyema kutumia JWTZ kudhibiti vurugu kwa kuwa wanajeshi hao hawana mafunzo ya kukamata wananchi wenye tuhuma za uhalifu isipokuwa wamefundishwa jinsi ya kulinda usalama wa nchi katika mipaka.
|
0 Comments