Mwili wa Mandela ukifikishwa kijijini kwake, utakabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi, ambapo bendera ya taifa itaondolewa  kwenye jeneza na kufunikwa kwa blanketi la kitamaduni la Xhosa kuashiria kurudi kwa mmojawao. PICHA | AFP
Johannesburg. Ratiba inayoonyesha namna siku kumi za maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela atakayezikwa kijijini kwake Qunu, Eastern Cape, imetolewa.
Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma akizungumza na waandishi wa habari juzi, alisema kuwa Desemba 8 itakuwa siku ya sala na kukumbuka mambo aliyoyafanya Mandela.
“Tunawaomba watu wetu wote wakusanyike kwenye kumbi za mikutano, makanisa, misikiti, mahekalu, masinagogi na nyumba zao kwa ajili ya sala na kutafakari kuhusu maisha ya Madiba na mchango wake kwa taifa letu na dunia, “ alisema Zuma.
Kwa mujibu wa CNN, siku hiyo itatumiwa na viongozi wa kitamaduni kukutana, nyumbani kwa Mandela au chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanya sherehe ya kimila ijulikanayo kama ‘kufumba macho.’
Viongozi hao watakuwa ‘wakiongea’ na Mandela na mababu zake wakiwaelezea namna mambo yalivyotokea katika kila hatua.
Inaaminika kuwa baada ya sherehe hiyo, mwili wa Mandela utahifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye hospitali ya jeshi ya Pretoria.
Ibada rasmi ya kumwombea Mandela itafanyika Jumanne, Desemba 10 katika uwanja wa michezo wa FNB wenye uwezo wa kuchukua watu 95,000 uliopo Soweto, mahali ambapo Madiba alionekana hadharani kwa mara ya mwisho alipokwenda kuangalia Kombe la Dunia Julai 2010.
“Kuanzia tarehe 11 hadi 13 Desemba, mwili wa mpendwa wetu Madiba utapelekwa katika majengo ya Muungano, yaliyopo Pretoria, mahali ambako alifanya kazi kama rais wa kwanza katika demokrasia changa baada ya kuapishwa Mei 10, 1994,” alisema.
Mwili wa Mandela utawekwa kwa siku tatu katika majengo hayo ili watu waweze kutoa heshima za mwisho. Siku ya kwanza imetengwa kwa ajili ya watu mashuhuri pekee.
“Katika kipindi chote hicho, ibada za kumwombea zitakuwa zikiendelea kwenye majimbo na mikoa yote,” alisema.
Maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kujitokeza barabarani Desemba 14 kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mithatha kushuhudia wanajeshi wakisafirisha mwili wa Mandela kuelekea Kijiji cha Qunu, mahali atakapozikwa Desemba 15.
Mwili wa Mandela ukifikishwa kijijini kwake, utakabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi, ambapo bendera ya taifa itaondolewa  kwenye jeneza na kufunikwa kwa blanketi la kitamaduni la Xhosa kuashiria kurudi kwa mmojawao.Viongozi wa ANC, machifu na familia ya Mandela wanatarajiwa kukutana usiku kwenye kikao cha faragha kabla ya kufanyika mazishi siku inayofuata.
Katibu Mkuu wa chama cha African National Congress (ANC), Gwede Mantashe alisema wanachama wa chama hicho nchi nzima watafanya ibada ya kumkumbuka Madiba wakati mwili wake utakapokuwa umelazwa kwenye majengo ya Muungano.
“Tumekubaliana kwamba si kila ibada itakuwa na mwanafamilia wa Mandela, huwezi kutegemea familia hiyo iwe katika ibada zote 54 au kuwa katika majimbo yote 9,” alisema Manteshe.
Alisema kuwa ANC yote itahamia Eastern Cape Desemba 14, kabla ya mazishi ya kitaifa na kwamba Zuma kama mwenyekiti wa chama hicho atahudhuria katika ibada yoyote ya kumkumbuka Madiba.
“Lakini hatuwezi kuzuia majukumu yake kama Rais wa Afrika Kusini.” Alisema.
Waziri katika Ofisi ya Rais, Collins Chabane alisema kuwa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa wageni litatangazwa baadaye.
Mandela ambaye alifariki katika nyumba yake mjini Houghton, Johannesburg, Alhamisi usiku wiki iliyopita, akiwa na umri wa miaka 95, anatarajiwa kuzikwa na maelfu ya watu wakiwamo viongozi mbalimbali wakubwa duniani.
Hoteli atakayofikia Obama yajulikana
Rais wa Marekani, Barack Obama na familia yake wanatarajia kulala katika Hoteli ya Radisson Blu iliyopo Sandton, wakatapokwenda kushiriki mazishi ya Mandela Desemba 15, imefahamika.
Itakuwa ni mara ya pili kwa Obama kufikia katika hoteli hiyo, kwani mara ya mwisho alipoitembelea nchi hiyo, alilala chumba namba 2301 katika ghorofa ya 23, wakati wasaidizi wake walichukua vyumba vyote kuanzia ghorofa ya 18 hadi 22.
Kwa mujibu wa gazeti la Independent, walinzi wa Obama wamekwishaondoa mapambo mbalimbali kwenye hoteli hiyo, zikiwamo picha za ukutani, mazulia, vifaa vya vyooni na bafuni.
“Pia wamebadilisha vifaa vyetu vya kuzuia risasi zilivyokuwa madirishani,  wameweka vya kwao,” alisema mfanyakazi ambaye hakutaka kutajwa jina.Polisi kadhaa na mbwa wanatarajiwa kwenda kufanya uchunguzi kwenye jengo hilo.
Ulinzi waimarishwa
Polisi jijini Pretoria jana walilazimika kuimarisha ulinzi kwenye majengo ya Muungano baada ya mamia ya waombolezaji kuvamia eneo hilo wakitaka kutoa salamu zao za mwisho kwa Mandela.
Kikosi cha polisi kililazimika kufunga barabara mbili zinazoingia kwenye majengo hayo ya serikali na kufanya ukaguzi kwenye magari yote yaliyokuwa yameegeshwa eneo hilo.
Waombolezaji waliokuwa wameacha maua na kadi za kumkumbuka Mandela, walizuiwa kuingia ndani ya majengo hayo. Kadi moja ilikuwa imeandikwa na Reitumetse Poo: “Mtu ambaye kila mmoja alimwangalia, mtu mtulivu siku zote, alituweka huru kwa kila kitu.”
Milioni nane wamlilia mitandaoni
Wakati huo huo, mwandishi wetu Elizabeth Edward anaripoti toka Dar es Salaam kuwa msiba wa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini umeonekana kugusa siyo tu Waafrika bali watu wa mataifa mbalimbali  ulimwenguni.
Hilo limethibitishwa na maoni ambayo yamekuwa yakitolewa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na msiba huo ulionekana kutikisa dunia.
Mpaka kufikia jana mtandao wa Twitter ulikuwa na maoni zaidi ya milioni nane yakiwa na neno ‘Mandela’ hiyo ikijumuisha salamu za rambirambi na kueleza namna ambavyo walimfahamu Mandela.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Daily Dispatch la Afrika Kusini, ulibaini tangu kutangazwa kwa taarifa za msiba maoni zaidi 185,000  kwa saa yamekuwa yakitumwa katika mitandao ya kijamii.
Maoni hayo pia yalionekana kwenye  mitandao mingine ya kijamii kama vile Facebook na Instragram katika  lugha mbalimbali kulingana na lugha anayoifahamu  mtumaji.
Mtaalamu wa masuala ya mtandao nchini Afrika Kusini, Gus Silber alisema kuwa taarifa kuhusiana na kifo cha Mandela zimeonekana kutawala zaidi kwenye mtandao kuliko ilivyowahi kutokea kwa matukio mengine.“Maoni yamekuwa mengi mno sidhani hata kama kuna uchaguzi wa Marekani ambao umewahi kuteka hisia za watu na kutawala katika mitandao ya kijamii kama msiba huu,” alisema Silber na kuongeza:
 “Nadhani baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2010 hakujawahi kutokea tukio lingine lililotawala katika mitandao ya kijamii kama msiba wa Madiba.”
Kwa mujibu wa Silber maoni mengi yamekuwa yakizungumzia sifa za shujaa huyo wa Afrika aliyesimama kidete kusaka uhuru wa Afrika Kusini na kupinga utawala wa kibaguzi barani Afrika.
Hoteli Afrika Kusini zajaa
Wakati Afrika Kusini ikifanya maandalizi kwa ajili ya mazishi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela, hoteli zote katika Jimbo la Gauteng zimeshajaa, imefahamika.
Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo jana, Meneja Mkuu wa Corporate Traveller, Eric Sakawsky, alisema kuwa hatua hiyo imetokana na idadi kubwa ya viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani kutaka kuhudhuria msiba wa Mandela.
Sakawsky alisema kuwa: “Kutokana na hali hiyo, kutakuwa na upungufu wa sehemu za malazi Johannesburg na Pretoria.
“Tumepewa taarifa kwamba kutokana na shughuli mbalimbali za Serikali na kidiplomasia, hoteli zote katika Mji wa Gauteng zitashikiliwa kuanzia Desemba 6 hadi 25.”
Aliongeza kuwa kampuni zote za magari ya kukodisha katika mji huo, pia hazitaruhusiwa kutumika kwa watu wengine.
Hata hivyo, alisema kuwa uamuzi huo hautawaathiri wateja ambao walikuwa wameshatoa oda zao au kulipia vyumba kabla ya tangazo hilo.
Vigogo watarajiwa Qunu
Rais wa Marekani, Barack Obama na mkewe, Michelle ni miongoni mwa viongozi wakubwa wanaotarajiwa kwenda Afrika Kusini ‘kumpumzisha’ Madiba.Katika safari yake, Obama anatarajiwa kuambatana na marais wa zamani wa Marekani, George W Bush, Bill Clinton, ambaye alikuwa madarakani wakati Mandela akiapishwa kuwa Rais. Viongozi hao wataambatana na familia zao.
Katibu wa Idara ya Habari Ikulu ya Marekani, Jay Carney alisema Obama atahudhuria kwenye ibada ya kumkumbuka Mandela, lakini hakuwa tayari kutoa taarifa zaidi.
Vyombo vya habari vya Brazil vimesema kuwa Rais wa nchi hiyo, Dilma Rousseff anatarajiwa kwenda Afrika Kusini kutoa salamu zake za mwisho kwa Mandela.