Na Mwandishi wetu
BURUDANI juu ya burudani! Mastaa mbalimbali wa filamu wanatarajiwa kufurika kwa wingi ndani ya Ukumbi wa Dar Live Mbagala-Zakhem jijini Dar, siku ya Krismasi katika tamasha maalumu lililopewa jina la Mtoko wa Mastaa, likiambatana na shoo ya nguvu yenye mchanganyiko wa Bongo Fleva, Hip Hop na Taarabu kutoka kwa wasanii nguli wa miondoko hiyo.
Wema Sepetu.
Siku hiyo, mashabiki watapata nafasi ya kupiga picha mbalimbali na mastaa hao sehemu tofautitofauti ikiwemo kwenye zuria jekundu (red carpet) pamoja na kubadilishana nao mawazo.
Akizungumzia shoo hiyo, Mratibu wa Burudani wa Ukumbi wa Dar Live, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’, alisema kwa upande wa muziki, wasanii watakaopanda stejini kuangusha shoo kali na ya kipekee ni pamoja na Profesa Jay, Joh Makini, huku Kassim Mganga ‘Tajiri wa Mahaba’, akitarajiwa kuangusha shoo kali kwa upande wa Bongo Fleva.

Jackline Wolper.
Aidha, Abby Cool alisema kwa upande wa Taarabu, mfalme wa nyimbo hizo za mwambao, Mzee Yusuf, atalipamba jukwaa kwa staili ya aina yake pamoja na Bendi ya Jahazi Modern Taarabu.
“Siku hiyo kutakuwa na mastaa mbalimbali wa filamu, ambapo mashabiki watapata fursa ya kupiga nao picha sehemu mbalimbali ikiwemo red carpet.
“Hakika itakuwa ni shoo ya aina yake. Kutakuwa na mchanganyiko wa Bongo Fleva, Hip Hop na Taarabu ili kuwaburudisha wadau na wapenzi wa burudani,” alisema Abby Cool.
Mbali na burudani hiyo, Abby Cool alisema kutakuwa na michezo mbalimbali kwa watoto kama kuogelea, bembea za kisasa kabisa pamoja na mazingaombwe kutoka kwa mtaalamu Profesa Karabash.