Matukio mbalimbali yaliyotokea Jumapili kwenye mazishi ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela yamenikumbusha yaliyotokea katika sherehe za miaka 50 tangu kuanzishwa OAU, sasa Umoja wa Afrika (AU).
Katika maadhimisho hayo, Tanzania ilimwagiwa sifa kedekede kutoka kwa wakuu wa nchi mbalimbali walioshiriki, wakiwamo Rais wa Senegal, Mark Sall, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegne na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Rais Zuma alitoa hisia zake kwa Tanzania, akisema wazi kuwa wananchi wa nchi Afrika Kusini hawatausahau mchango wa Tanzania katika kuwakomboa na kuwafikisha walipo sasa. “Tulisaidiwa na nchi nyingi, lakini Tanzania ilitusaidia kwa namna ya kipekee.”
Sifa hizo ziliwekewa uzito katika hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kwenye mazishi, alipoamua kueleza kwa uwazi historia ya Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini na Afrika kwa jumla.
Awali, ilipofanyika ibada ya kumbukumbu ya Mandela ambapo viongozi mbalimbali zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali duniani walishiriki, Watanzania hawakuelewa kuona mchango wa Tanzania hauelezwi wazi katika tukio hilo muhimu wala kupewa fursa ya kuhutubia, lakini bila shaka nyoyo zao zilisuuzika baadaye Jumapili, fursa hiyo ilipopatikana siku ya mazishi.
Kauli ya Prof Mpangala
Miongoni mwa walioweka wazi dukuduku lao ni Profesa Gaudence Mpangala wa Kitengo cha Sayansi ya Jamii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akisema Tanzania ilitakiwa kupewa nafasi ya kuzungumza lolote kutokana na ukaribu wa nchi hizo.
Anasema Tanzania ni moja ya nchi duniani zenye historia kubwa na ujenzi wa taifa la Afrika Kusini.
“Na baada ya kutoka gerezani mwaka 1990, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza Mandela kuitembelea kwa lengo la kutoa shukrani zake, tukampatia na heshima ya jina lake kuitwa barabara muhimu, Mandela Road,” anasema Profesa Mpangala na kuongeza;
Sasa sijui ni utaratibu gani uliotumika kuangalia vigezo vya kuhutubia, kwa sababu siku zote rafiki yako wa karibu ndiye anayestahili nafasi ya kuzungumza siku ya msiba wako,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Usu Mallya anasema kutokana na mazingira hayo, kuna kila sababu ya Watanzania kujiuliza kwa sasa, iwapo thamani iliyokuwapo katika harakati za ukombozi bado inatambuliwa.
Anaongeza kuwa ni muhimu kukumbuka kwamba Tanzania ilikuwa kitovu cha harakati za ukombozi na kituo cha kuandaa fikra mbadala kwa ajili ya kutumika katika harakati za kuleta mabadiliko kwa ndani na nchi nyingine za Afrika.Kwa upande wake Wakili wa Kujitegemea na Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Maria Kashonda anasema mazingira hayo yasiwakatishe tamaa Watanzania kwani haiwezi kuondoa heshima iliyojengeka miongoni mwa mataifa hayo.
Maria anasema mbali na Tanzania kutoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa taifa hilo, jamii haitakiwi kuwa na unyonge wa kutohusishwa kuhutubia katika msiba huo.
“Ni kweli inashangaza lakini tusionekane wanyonge  kwa sababu ya hali hiyo tu, hatuwezi kujua walitumia vigezo gani lakini sisi kama Watanzania ndiyo tunafahamu mchango na uhusiano uliopo katika historia ya ukombozi,” anasema Maria.
Kauli hii inaungwa mkono na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta), Nicolas Mgaya akisema haoni tatizo lolote katika mazingira hayo.
Anasema kutokana na mazingira yalivyokuwapo, haikuwa rahisi kupata nafasi ya kushiriki kwa viongozi wengi wa Afrika.
“Siamini kama kukosa nafasi ya kuzungumza kwa Tanzania inaweza kuwa kigezo cha kutothamaniwa mchango wetu, ila kutokana na muda, idadi kubwa ya marais basi imetokea hali hiyo,” anasema Mgaya.
Baada ya nafasi ya kuhutubia kupatikana na ikatumiwa vizuri, wananchi mbalimbali, waliochangia katika mitandao ya kijamii, wamepongeza kwa historia hiyo iliyofichika kuwekwa wazi na kufahamika katika tukio lililokuwa linatazamwa na dunia nzima.
Mchango wa Tanzania
Uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini ulianza kabla ya miaka ya 1960 ikiwa mwanzo wa harakati za kuondoa utawala wa mkoloni barani Afrika.
Baada ya juhudi za kudai uhuru kwa njia ya amani kushindikana, Mzee Mandela aliamua kutafuta mbinu na njia mbadala za kutafuta ukombozi wa taifa hilo kupitia mchango wa mataifa ya Afrika.
Taarifa kutoka mtandao wa chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini, zinaonyesha namna uongozi wa juu wa chama hicho ulipoamua kuhamia Tanganyika baada ya serikali dhalimu ya makaburu wa Afrika Kusini kukipiga marufuku chama hicho.