Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe PICHA|MAKTABA
Singida, Mwanza na Arusha. Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha zimenusurika kuteketea baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya vyumba vyake jana alfajiri.
Wakati hayo yakitokea, msuguano ndani ya chama hicho umeendelea kushika kasi baada ya jana, Mwenyekiti wake Mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu kujiuzulu akipinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kwamba walipata taarifa za kuungua kwa ofisi hizo zilizopo eneo la Ngarenaro saa mbili asubuhi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema chumba cha kompyuta ambacho kina kumbukumbu za wanachama wote Kanda ya Kaskazini kimeathirika.
“Hii ni hujuma dhidi ya Chadema; watu hawa walipanda juu ya ukuta na kuingia ndani kupitia kwenye dari kisha kuchoma moto ofisi,” alisema Golugwa.
Alisema vyumba viwili ndivyo, vimeungua kabisa na kwa bahati nzuri moto ulishindwa kusambaa na kuzimika baada ya umeme kuzimwa. Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Wilaya ya Arusha, Happiness Chale ambaye aliwahi kushuhudia tukio hilo alisema, mhudumu wa ofisi hiyo, Jenipha Mwacha alibaini moto huo baada ya kusambaa na kufika katika maliwato. Alisema kwa kawaida ofisi hiyo inalindwa na walinzi wa Red Brigade.
Polisi walifika mapema eneo hilo na kuweka uzio ili kuzuia watu kuingia katika ofisi hizo pamoja na kuanza uchunguzi wa tukio hilo.
Wakati polisi wakiwa katika ofisi hizo, viongozi wa Chadema Mkoa na Wilaya ya Arusha walikuwa wakitoa maelezo polisi kuhusiana na tukio hilo.
Huko Singida, Kitundu amejiuzulu nafasi hiyo jana huku akieleza kuwa chama hicho kinakiuka misingi ya demokrasia.
Uamuzi wa Kitundu umekuja siku nne tu, tangu Mwenyekiti wa Chadema mkoani Lindi, Ally Chitanda naye kujiondoa katika nafasi hiyo akieleza kuchoshwa na uamuzi wa kikanda na kikabila unaoendelea ndani ya chama hicho.Katika taarifa yake ya jana, Kitundu ambaye pia ni muasisi na Chadema mkoani Singida, alisema: “Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya Uenyekiti wa Mkoa wa Singida, ambayo nimeitumikia kwa muda mrefu kutokana na kukiukwa kwa demokrasia ya kweli ndani ya chama,” alisema na kuongeza:
“Binafsi ni mtu wa kwanza kujiunga na Chadema hapa Singida na mtu wa 300 kujiunga na chama hiki kitaifa. Hiyo ni heshima kubwa kwangu na sipo tayari kuipoteza kwa kukubali kuwa sehemu ya udhalilishaji huu wa demokrasia uliopitiliza.”
Alipinga hatua hiyo ya Kamati Kuu ya Chadema akisema ni kinyume na mambo ambayo chama hicho kinayahubiri kwa umma... “Si vyema nikaendelea kupingana na dhamira yangu inayonituma kuwa mwanademokrasia wa kweli.”
Awali, akizungumza na waandishi wa habari mjini Singida, Kitundu alisema baada ya kupata taarifa za Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto na wenzake, alimtumia ujumbe mfupi wa maneno Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimweleza: “Uamuzi mliofanya ni sawa na mtu kujenga nyumba ya tope wakati mvua kali ikinyesha.”
Alisema mwenyekiti wake hakuwahi kumjibu. Mbowe hakupatikana jana kujibu madai hayo kwani yuko nje ya nchi.
Alisema baada ya kufanya kikao na wenyeviti wa Chadema katika wilaya za Mkoa wa Singida, wamefikia uamuzi wa kulaani, kupinga na kukemea uamuzi Kamati Kuu ya chama aliyoyaita kuwa ni ya kipuuzi yaliyojaa chuki, hofu na wasiwasi mwingi.
Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Singida, Patrick Msuta alikiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa Kitundu na kusema: “Kama alikuwa na tatizo, angekatia rufani suala hilo katika ngazi husika.”
“Uamuzi wake ni kama kutengeneza mgogoro na katika mgogoro una kujenga au kubomoa. Sasa uamuzi wake hauwezi kubomoa chama, kwani Chadema kuna watu wazuri wenye uwezo wa kukijenga chama. Chadema hakuna ilichopoteza kwa uamuzi wake.
“Alichokifanya ni kama ametumia demokrasia yake kupinga uamuzi wa Kamati Kuu na ametekeleza... lakini juzi tu hapa, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa mtu ambaye hawezi siasa aache, akae kando akalime, mimi nadhani huyu anatekeleza kauli ya Rais,” alisema Msuta.
Msuta, baadaye alisema kuwa uongozi wa Chadema mkoani humo hauhusiki na yaliyozungumzwa na Kitundu: “Huo ni uamuzi wake yeye mwenyewe, hakuna anayehusika na uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti.”
Chadema Mwanza watoa tamko
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Mwanza, Yunusi Chilongozi amesema chama chake kitawachukulia hatua wote waliohusika kutoa tamko la kuwapiga marufuku viongozi wa kitaifa, Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbrod Slaa na Mbowe kufika mkoani humo.Chilongozi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Chadema, kimechoka kuchafuliwa na kundi la vijana ambao wamekuwa wakitumika kwa madhumuni na malengo yasiyofahamika na sasa kitawashtaki mahakamani.
“Tuko katika maandalizi ya mapokezi ya viongozi wetu kichama mkoani Mwanza na tunalaani kauli ya Robert Gwanchele anayejiita Mwenyekiti wa Matawi ya Chadema Mkoa wa Mwanza ikiwazuia viongozi wa juu wa chama hicho kutokanyaga Mwanza.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 17 inatoa uhuru wa kila Mtanzania kutembea sehemu yoyote ya nchi ilimradi havunji sheria za nchi na waliotoa tamko la kuwazuia viongozi wao wamevunja sheria za nchi,” alisema Chilongozi.
Slaa aanzia Shinyanga leo
Dk Slaa, leo anaanza ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ambako atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa Dk Slaa anatarajia kuanza ziara yake wilayani Kahama na kesho yake ataendelea na ziara hiyo mkoani Kigoma.
Hatua hiyo, imekuja siku chache baada ya viongozi wa Mkoa wa Kigoma kumtaka Katibu huyo kuahirishwa ziara hiyo kutokana na sababu zilizodaiwa kuwa za kiusalama.
Imeandikwa na Mussa Juma, Gasper Andrew na Fredrick Katulanda.
|
0 Comments