ILIKUWA ni safari ndefu, iliyosheheni misukosuko, kwa nguvu za Mwenyezi Mungu tumefanikiwa kuvuka milima na mabonde na sasa tumerejea tena mtaani, tukiwa na sura na muonekano mpya. Si kwamba tumelegeza vishikizo vyetu, bali tumezidi kukaza gidamu za viatu tulivyovaa katika kuhakikisha tunawashibisha Watanzania kile walichokikosa kwa muda wa siku 90, ambao tulikuwa kifungoni.
Sio lengo letu kuanza kubainisha kwa kina habari tulizozichapisha hadi Serikali ikaamua kuzitumia kama rungu la kutuadhibu. Inawezekana tulipotoka, hata hivyo hatukustahili adhabu kubwa ya namna ile.
Ni utumiaji wa nguvu ya madaraka usioelezeka kwa mujibu wa taratibu za kisheria hususan ikizingitiwa nchi hii ni ya kidemokrasia inayozingatia utawala wa kisheria kwa kuheshimu vyombo vya kisheria vilivyowekwa kama vile mahakama.
Si nia yetu kuanza kumsaka mchawi aliyeamua kujitolea mhanga kwa kutoa uamuzi usiokuwa na mantiki au tija kwa jamii, bali tulishangazwa kuona amri ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu ambayo dunia ilikuwa ikiyafuatilia.
Kulifungia gazeti wakati ule haikuwa dawa ya kutibu majeraha yanayoendelea kulikumba taifa, kama haya ya kuwa na mawaziri mizigo, vyombo vya usalama kutumia nguvu ya kijeshi vibaya kuwapiga raia wema kwenye Operesheni Tokomeza, ambayo imesababisha kulitingisha Taifa.
Hatua ya mawaziri wanne kuvuliwa nyadhifa zao, si jambo dogo, ni jambo zito ambalo linachafua taswira ya Baraza la Mawaziri na Serikali kwa ujumla.
Hatua ya Serikali kulifungia gazeti hili kwa kipindi cha siku 90, si tu imeharibu sifa nzuri ya Tanzaniakwenye masuala ya haki na usawa, bali pia imemuweka Rais Kikwete kwenye wakati mgumu kimataifa, ambapo huenda baadhi ya mataifa rafiki wameanza kupata hofu juu ya uhuru wa habari nchini.
Ukweli ni kwamba uhuru wa vyombo vya habari, unaweza kusaidia kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kujenga misingi ya uwajibikaji wa viongozi wa Serikali na sekta ya umma kwa wananchi wao na hivyo kuendeleza amani na utulivu wa kweli na kushawishi uwekezaji wa wafanyabiashara na wajasiriamali wa ndani na nje.
Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), unathibitisha kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaambatana na maendeleo ya uchumi, kutokomeza umasikini na kuwepo kwa huduma bora za jamii ikiwemo elimu, afya na lishe bora.
Uhuru wa vyombo vya habari sio jambo la anasa la kusubiri mpaka nchi itakapokuwa imeendelea. Ni msingi muhimu wa kuleta maendeleo kwa wote. Vyombo vya habari ni muhimu katika mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa. Vyombo vya habari vilivyo huru ni medani ya mijadala ya sera na maoni mbalimbali na vinasaidia kufikia uamuzi wa pamoja na maridhiano ya kitaifa. Vyombo vya habari vinafuatilia utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali. Ni nyezo ya kuelimisha na kutoa taarifa zinazosaidia kukuza biashara, kuelewa fursa za kiuchumi zilizopo na mabadiliko ya teknolojia.
Jambo la kushukuru ni kwamba, nchi iko kwenye mchakato wa kupata Katiba Mpya. Kifungu cha 30 cha Rasimu ya Katiba Mpya kinazungumzia Uhuru wa habari na vyombo vya habari, kifungu kidogo cha 30(2) kinaeleza kuwa “Vyombo vya habari vitakuwa huru na vile vile vitakuwa na haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa wanazopata”. Kwa mujibu wa kifungu hiki ni wazi kinatoa uhuru wa vyombo vya habari, ambao ndio kilio cha wengi.
Hata hivyo, kifungu kidogo cha 30(4) kina dalili za kufifisha uhuru unaotakiwa na wengi kwa kueleza “Masharti ya Ibara hii yatalazimika kuzingatia masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa ajili hiyo na kwa madhumuni ya kulinda usalama wa Taifa, amani, maadili ya umma, haki, staha na uhuru wa watu wengine.”
Kwa muktadha huu, ni wazi kwamba kifungu hiki kinaweza kutumiwa vibaya katika kuendeleza sheria za ukandamizaji wa vyombo vya habari.
Isitoshe vyombo vya habari siyo jambo la muungano. Ni muhimu wakati wa kujadili rasimu ya Katiba Mpya, uhuru wa vyombo vya habari uwe wazi na uingizwe katika Katiba za Tanganyika na Zanzibar.
Endapo suala hili litaachwa, kifungu hiki kitaipa mamlaka Serikali kuwa mlalamikaji, muendesha mashtaka na jaji wa kutoa hukumu. Haki haiwezi kutendeka katika hali hii.
Kwa mujibu wa taarifa ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, ni wazi sheria hii inapinga kifungu cha 19, taarifa hiyo inaeleza “Kila mmoja ana haki na uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na maoni kwa njia yoyote bila kujali mipaka.”
Tunarejea mtaani leo tukiwa chini ya sheria kandamizi za magazeti, ni budi sasa Watanzania kwa ujumla tuungane katika kuzipinga sheria zote kandamizi.
Inatia ukakasi kuona baadhi ya taasisi ziko juu ya sheria hata kama zinavunja sheria na ukweli unaposemwa kunaibuka hoja za uchochezi kama zilivyoelekezwa kwenye gazeti hili na kukumbana na adhabu kali ya namna ile.
Hebu tuliangalie kwa kina suala la baadhi ya wanajeshi na polisi kupiga na kufanyia matendo ya kidhalimu Watanzania wenzao wakati wa Operesheni Tokomeza ambayo imeitia doa jekundu Serikali.
Tunaamini Serikali kupitia Idara ya Habari Maelezo, ilitekeleza uamuzi ule kwa sababu ambazo inazijua, hata hivyo tulikubaliana na adhabu ile na kwamba tutasimamia weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.
Hatukuwahi kuwa na nia ovu ya kuwajengea chuki Watanzania na Serikali yao, tumekuwa mstari wa mbele kusema ukweli, na ukweli utakuwa kwenye viganja vyetu na midomo yetu daima.
Ukweli uliowazi ni kwamba, hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (Vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea kwa pamoja wameumia.
Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao.
Hivyo hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika, nao pia wameumia. Hasara ambayo kampuni imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali haielezeki.
Tunataka kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, ni magazeti makini yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, lakini tumekuwa makini mno katika kuhakikisha tunalinda maslahi ya nchi na wananchi wake.
Adiha pindi inapotokea tukafanya makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka, kwa lengo la kupunguza maumivu kwa yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni kulazimisha uongozi uchukue taratibu za kisheria juu yake.
Kampuni yetu imejiwekea taratibu na sera ambazo kila mwandishi, mhariri na mfanyakazi yeyote wa kampuni hii huzifuata ili kutekeleza majukumu yake kwa weledi.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Kwa sababu tunaona kuwa ni sheria ambayo inatoa mwanya kwa kiongozi wa wanahabari kutumia rungu lake bila kujali wala kufuata misingi ya Katiba ambayo ni baba au mama wa sheria zote nchini.
Hata hivyo, pamoja na hayo yote tunapenda kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa ujumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni.
Wametuunga mkono tulipohamishia nguvu zetu kwenye gazeti la RAI na tunaamini wataendelea kuwa nasi katika kipindi hiki tunachorejea mtaani, tunaahidi kuwapatia habari nzito na za uhakika.
Tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti ambayo yalionekana kuonewa.
Tunaamini hatua ya kurejea leo na wakati huu wa msimu wa sikukuu, ni ishara tosha kwamba tumerudi kwa ajili ya kuukomboa uhuru wa habari kutoka kwenye makucha ya sheria kandamizi.
0 Comments