Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwandishi wa makala haya kwa miezi kadhaa, umebaini kuwa vitendo vichafu vimesababisha baadhi yao kuathirika kisaikolojia hivyo kujikuta wakiona jambo hilo ni la kawaida na hulifurahia.
Watoto hao hufanyiwa vitendo hivyo hasa kipindi cha masika ambapo mvua huwa zinanyesha, maeneo ambayo hupendelea kulala nyakati hizo kwenye majumba ambayo ujenzi wake haujamalizika (Mapagala) huwa yanavuja maji ya mvua hivyo hulazimika kuyazikimbia kujisalimisha popote.
Wapo watoto wawili tayari tumewatenga katika kundi letu kwa tabia ya kupenda kulawitiwa, sasa kama wapo wengine tukiwafahamu nao tunawatenga hata wakipata matatizo hatuwezi kuwasaidia” mtoto mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jose (siyo jina lake halisi).
Naye mtoto aitwaye Juma anasema kuwa kinachowaponza watoto wengine ni tamaa na sio hifadhi ya kulala pekee kwani wapo watoto ambao wamezitoroka familia zao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na kukimbilia mitaani kufanya kazi ya kuombaomba ambapo wamekuwa wakidanganyika kwa vyakula kama Chips na pombe katika baa za usiku.
“Sisi wengine tupo huku mitaani kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kipato duni cha familia zetu, malezi mabaya kama vile kulelewa na kina mama wa kambo ambao ni chanzo matatizo kwa sehemu kubwa lakini sio sababu ya kukubali kulawitiwa.
Ila wapo wale wanaopenda pombe na chips ndio wanajikuta wakishawishiwa na sio tu na walinzi lakini pia hata baadhi ya watu ambao hutumia kisingizio cha ulevi wa pombe ili kufanya vitendo hivyo,” anasema mtoto Maiko (siyo jina lake halisi).Walinzi
Baadhi ya walinzi walihojiwa kwa nyakati tofauti na mwandishi wa makala haya walikiri kwamba wapo wenzao wamekuwa na tabia ya kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto hao.
“Ni kweli wapo wenzetu wana tabia hii hasa mtaaa wa Nyerere road (barabara ya kuelekea mkoani) na kuna tukio la mauaji liliwahi kutokea ambapo kuna mtu alikuwa mlinzi anamlawiti mtoto usiku wa manane akamshushia kipigo hadi kumsabishia kifo” anasema mlinzi mmoja anayelinda mtaa wa Kiwelu ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Hata hivyo, mlinzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Peter alisema kwamba yeye binafsi hajawahi kusikia kama kuna baadhi ya walinzi wanafanya vitendo hivyo na watoto ila anachofahamu ni walinzi kuwahifadhi watoto hao kwa kuwapa eneo la kulala kwenye vibaraza vya waduka wanayolinda hali ambayo huwasaidia pia kiulinzi.
Ongezeko la watoto hao na mikakati ya kuwadhibiti
Afisa maendeleo ya Jamii Manispaa ya Sumbawanga, James Biseko anasema hivi sasa manispaa hiyo ina watoto wa mitaani 6872 ambapo kati ya hao 3268 ni wavulana na wasichana ni 3604 takwimu zilizopatikana baada ya utafiti uliofanywa kati ya uongozi Manispaa hiyo na Shirika la Pact - Tanzania.
Shirika hilo lilishirikiana na Manispaa hiyo kutafuta takwimu hizo wakati wakianza kutekeleza mradi wa pamoja tuwalee unaolenga kumtaka mwana jamii kutunza na kusaidia watoto hao.
Aidha, uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi mjini Sumbawanga, umebaini kuwa ongezeko la watoto wa mitaani ni kubwa na linasababishwa na hali ya umasikini wa kipato unaozikabili familia nyingi.
Hali hiyo inawalazimu wazazi kuzikimbia familia zao hivyo watoto kulelewa na kina bibi wasio na uwezo kiuchumi na kuwatumia watoto hao kama sehemu ya kujipatia kipato cha siku kwa kupita mitaani kuomba fedha.
Anaeleza kuwa baada ya watoto hao kuzoea maisha ya kuomba mitaani hulazimika kutorudi kwa walezi wao (bibi) zao, hivyo hubaki mijini wakiendelea na maisha ya kuomba omba.
Anaeleza kwamba sababu nyingine ni migogoro ya kifamilia na malezi ya wazazi wa kambo.Pia tamaa ya baadhi ya watoto kupenda kukimbilia mjini wakifikiri maisha ni rahisi.
Kwa upande wake, Deo Mlwafi ambaye ni mratibu wa mradi wa pamoja - unaotekelezwa na Pact - Tanzania kwa kushirikiana na Shideph+ Mkoa wa Rukwa anasema kuwa wao jukumu ni kuijengea uwezo jamii kupitia kamati za mitaa ili kamati hizo ziweze kuwasaidia watoto hao.Kuhusu Maambukizi ya ukimwi.
Makamu mwenyekiti wa Shidepha+ taifa, Godfrey Mwikala anaeleza kuwa watoto hao wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Ukimwi kwa kuwa wamekuwa wakishiriki ngono isiyo salama.
“Si watoto wa kike wala wa kiume wote wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kuwa wanashiriki ngono zembe, hawana elimu yoyote.
Nafikiri ipo haja ya kuwepo kwa mradi mwingine ya kuwafikia moja kwa moja watoto hawa kuwahifadhi katika vituo maalumu, kuelimisha kuhusu athari ngono zembe, kuwapima afya ili kuona namna ya kuwasaidia maana mradi wa Pact - Tanzania unalenga kuwaisaidia lakini kupitia ngazi ya jamii tu” anasema.
Mipango na Mikakati ya Serikali.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imekuwa na mipango na mikakati ya kuhakikisha kwamba watoto wote wanastawi na kuwa na maisha bora kutokana na kupatikana kwa haki zao za msingi ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushiriki katika mambo yanayowahusu bila ubaguzi wa hali yoyote.
Hiyo ni sehemu ya mipango na mikakati ya Serikali ambayo ipo kwenye maandishi, pasipo utekelezaji wa aina yoyote ile ndio maana ongezeko la watoto wa mitaani ni kubwa, na hakuna wenye kuchukua hatua si Serikali kuu, za mikoa wala wilaya huku taasisi zisizo za kiserikali zilizoanzishwa kwa ajili ya kusaidia kupunguza tatizo hilo zimekuwa zikiishia kujinufaisha zenyewe.
Baadhi ya wananchi wanashauri Serikali kushirikiana na familia ili kuhakikisha wanakuwa na maisha bora, tofauti na ilivyo sasa, kwani kuna idadi kubwa ya watoto wa mitaani.
Mkazi wa Sumbawanga, Julian Francis anasema wakati umefika kwa Serikali kuwa na mkakati thabiti katika kutokomeza vitendo hivyo vichafu; polisi wanatakiwa kufuatilia hilo.
0 Comments