Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema maandalizi ya mechi hiyo ya aina yake yamekamilika.
Wambura alisema vikosi vya ulinzi na usalama katika mechi ya leo vimekamilika kila idara na kwamba Barabara ya Taifa inayoanzia Keko-Maghorofani hadi Barabara ya Mandela, itafungwa kuanzia saa 12 asubuhi kupisha hekaheka za mtifuano huo.
Alisema magari hayataruhusiwa kuegeshwa kuanzia eneo la Baa ya Minazini hadi msikiti unaotazamana na Uwanja wa Uhuru, hivyo magari yote yataegeshwa nje ya Uwanja wa Ndani wa Taifa – kando ya Barabara ya Mandela.
“Magari yatakayoruhusiwa kuingia maeneo hayo na hata ndani ya Uwanja wa Taifa ni yatakayokuwa na stika zilizotolewa na TFF. Tunawaomba wadau na mashabiki wa soka kuheshimu na kutii maagizo ya vikosi vya ulinzi,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa milango ya kuingilia uwanjani itakuwa wazi kuanzia saa sita mchana ambapo baada ya mauzo ya tiketi ya jana, zoezi hilo litaendelea leo nje ya uwanja huo kabla ya mechi ili kuwapa mashabiki fursa ya kukata na kuingia moja kwa moja.
Pambano la leo linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wanaohitaji sio tu kuona nyota wapya waliosajiliwa na klabu hizo, pia kujua ‘nani jembe’ ndani ya uwanja kwani kwa nje ya uwanja, Yanga ni kama imeshinda kutokana na kuwa kwenye mazingira mazuri kisaikolojia.
Nje ya uwanja, Nani Mtani Jembe ilihusisha vita baina ya mashabiki wa kila klabu ‘kupora’ mamilioni ya mwingine kupitia shindano la kinywaji cha Kilimanjaro Premium Lager ambapo Simba ilizidiwa na Yanga kwa kiasi kikubwa cha pesa.
Ukiondoa shangwe ya mashabiki wa Yanga kumpata mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi akitokea SC Villa ya Uganda na Juma Kaseja, Simba leo itakuwa na makipa waliowahi kudaka Jangwani kwa vipindi tofauti, Ivo Mapunda na Yaw Berko.
Nyuma ya majina hayo makubwa, Yanga ilinasa saini ya kiungo Hassan Dilunga kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, wakati Simba iliwasainisha kwa mpigo kiungo mchezeshaji Awadh Juma Issa kutoka Mtibwa Sugarya Morogoro na Ally Badru Ally kutoka Canal Suez ya Misri.
Kila timu ilishajichimbia kambini kunoa makucha kuelekea pambano hilo ili kusawazisha makosa yaliyowafanya watani hao kutoka sare ya 3-3 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Oktoba 20.
Uwepo wa nyota wapya kwa kila upande ambao watashirikiana na wakali wengine, unalifanya pambano la leo liwe lenye mvuto wa aina yake ambapo kiingilio cha chini ni sh 5,000 kwa viti vya kijani.
Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, kiingilio ni sh 7,000; viti vya rangi ya chungwa sh 10,000; VIP C ni sh 15,000; VIP B sh 20,000 huku VIP A sh 40,000.
Kwa upande wa waamuzi, kati atasimama Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles wa Dodoma huku Israel Nkongo wa Dar es Salaam akiwa mezani. Kazi ya kutathimini utendaji wa waamuzi wote itakuwa chini ya Soud Abdi wa Arusha.
MECHI TANGU 2010
Rekodi ya watani hawa inaonyesha kuwa mechi ya leo ni ya tisa tangu mwaka 2010 na katika mechi nane, Yanga imeshinda tatu, Simba mbili na wamekwenda sare tatu.
Aprili 18, 2010: Simba 4, Yanga 3
Oktoba 16, 2010: Yanga 1, Simba 0
Machi 5, 2011: Yanga 1, Simba 1
Oktoba 29, 2011: Yanga 1, Simba 0
Mei 6, 2012: Simba 5, Yanga 0
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1
Mei 18, 2013: Yanga 2, Simba 0
Oktoba 20, 2013: Simba 3, Yanga 3
0 Comments