Stori: Makongoro Oging’
WATOTO wawili wakazi wa Kijiji cha Ngombanya, Kata ya Kimbiji wilayani Temeke jijini Dar esSalaam, Alhamisi ya wiki iliyopita saa 9 alasiri walilipuliwa na bomu na kupoteza maisha.
Licha ya bomu hilo kuua watoto hao, mwenzao mmoja Shaban Hassan,5, aliponea chupuchupu.
Waliopoteza maisha ni Yohana Vicent,10, na William Jeremia,8, na inadaiwa kuwa watoto hao walilipukiwa na bomu hilo wakati wanatoka kufukuza nyani shambani.
Katika mahojiano na gazeti hili kaka wa marehemu Yohana aliyejitambulisha kwa jina la Venance Silungwe alikuwa na haya ya kueleza kuhusina na tukio:
“Maeneo hayo lilipotokea tukio kuna mashamba ya mihogo ambapo watoto hao walikuwa wakiwafukuza nyani.
“Wakiwa wanarudi waliona hilo bomu ambapo walifikiria kuwa ni kitu cha kuchezea, hivyo kuamua kulichukua na kulichezea ndipo likawalipukia.
“William alifariki hapohapo wakati Yohana alikutwa hai lakini akiwa amejeruhiwa kichwa upande wa kulia na vidole vitatu vya mkono wa kulia vilikatika na shingoni kulikuwa na jeraha kama vile alichomwa na kitu chenye ncha kali, alifia njiani akiwa anapelekwa hospitali.
“Baada ya tukio hilo kutokea mtoto Shabani ambaye hakujeruhiwa alijaribu kuwaita wenzake kwa majina, alipoona wamenyamaza aliamua kwenda kwa wazazi wa marehemu na kuwaeleza.
“Wazazi walifuatana naye hadi eneo la tukio ambapo waliwakuta wamejeruhiwa vibaya, William alikuwa amekwishafariki dunia na Yohana alitapakaa damu.
“Maiti za watoto hao zimehifadhiwa katika Zahanati ya Kimbiji na tunatarajia kuzika Jumatatu (jana).”
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, SACP Engelbert Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilo. “Tukio hilo limetokea na tunaendelea kufanya uchunguzi,” alisema kamanda huyo.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameliomba Jeshi la Wananchi, kulifanyia ukaguzi eneo hilo walilokuwa wakilitumia kwa mazoezi.
0 Comments