|
Mkuu wa Jeshi la Polisi aliyemaliza muda wake, Said Mwema akimkabidhi kadi Naibu IGP, Abdulrahman Kaniki baada ya kuapishwa Ikulu Dar es Salaam jana. Kushoto ni IGP mpya, Ernest Mangu.Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam. Baada ya kuapishwa jana kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu amesema ataanza kazi yake kwa kupambana na uhalifu wa aina zote pamoja na ajali za barabarani.
Akizungumza katika Viwanja vya Ikulu jana baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, IGP Mangu alisema: “Nitakabiliana na uhalifu kwani uhalifu bado ni tatizo kubwa, nitaangalia mfumo uliopo na kuubadilisha ili kupunguza au kumaliza kabisa uhalifu.”
Pia Mangu alisema, jeshi la polisi litatumia rasilimali zote ilizonazo ili kuhakikisha uhalifu unapungua pamoja na ajali za barabarani ambazo alisema zinaathiri maisha ya watu na mali zao.
Mbali ya IGP Mangu kuapishwa jana, Msaidizi wake, Abdulrahman Kaniki naye aliapishwa kushika wadhifa huo mpya katika jeshi hilo.
IGP Mangu alisema anafahamu kuwa kazi yake ina changamoto nyingi lakini amejipanga na atajitahidi kukabiliana nazo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na mawaziri mbalimbali pamoja na wakuu wa majeshi. Waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira.
Kwa upande wake, Naibu IGP, Kaniki alisema amepokea uteuzi uliofanywa na Rais kwa mshtuko mkubwa kwani ni jambo ambalo hakulitegemea. Hata hivyo, alisema ataifanya kazi yake kwa weledi na usasa.
“Nilishtuka lakini kwa kuwa hii ni kazi yangu na niko ndani ya Jeshi la Polisi, basi nitaifanya kwa weledi na utashi wangu wote,” alisema
Alisema Watanzania watarajie huduma bora kutoka katika jeshi hilo na ushirikiano wa kina kwa wananchi na watu wa kada nyingine.
Naibu IGP, Kaniki pia alisema atatumia polisi wa ngazi zote kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika ili kupunguza malalamiko.
IGP Mstaafu, Said Mwema alisema ataendelea kumpa ushirikiano wa kutosha mkuu huyo mpya wa Jeshi la Polisi na kuwataka wananchi kumpa ushirikiano zaidi.
“Kwanza namshukuru Rais kwa uteuzi wake lakini ningependa ushirikiano uendelezwe kwa vyombo, asasi, taasisi na kwa raia wote kama ilivyokuwa awali,” alisema
|
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wake, Mwema alisema zipo tafiti mbalimbali za kisayansi zilizofanywa na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zinazohusu mafanikio ya kutumia polisi jamii na kuhusu utendaji wa jeshi hilo.
Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya Chadema imewapongeza wakuu hao na kuwataka kuliboresha Jeshi la Polisi ili lifanye kazi kwa kuzingatia haki za binadamu, sheria za nchi na weledi.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare alisema jana katika taarifa yake kuwa umma wa Watanzania umekuwa mashuhuda wa namna ambavyo jeshi hilo linavyotumika kwa manufaa ya kisiasa na baadhi ya viongozi walioko serikalini.
“Kwa sababu ya ‘kukubali’ kutumika huko kisiasa, wakati mwingine tumeshuhudia jeshi likiacha kuwajibika na kutumikia wananchi badala yake limekuwa likilinda masilahi ya CCM na viongozi wake dhidi ya washindani wao wa kisiasa hasa Chadema,” alisema.
Baadhi ya askari polisi wa Mkoa wa Manyara, wamempongeza Mkuu mpya wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo na wamemuasa ajitahidi kurudisha nidhamu.
Wakizungumza jana polisi hao walisema aliyekuwa IGP, Said Mwema alijitahidi kulisogeza jeshi hilo kuwa karibu na jamii hivyo kumtaka IGP Mangu aendeleze jambo hilo na kusimamia nidhamu iliyotetereka.
Askari hao waliogoma kutaja majina yao walisema wana imani kubwa na IGP Mangu na kuahidi kumpa ushirikiano ili kuhakikisha jukumu la kusimamia usalama kwa jamii linatimizwa ipasavyo.
*Nyongeza na Joseph Lyimo, Babati.
0 Comments