Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu akizungumza na Maofisa, Wakaguzi , Askari na watumishi raia wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Vikosi vya Jeshi la Polisi (hawapo pichani) katika kikao chake cha kwanza na watendaji hao baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.Kikao hicho kilifanyika jana katika Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Ostarbay jijini Dar es Salaam.(Kushoto) ni Naibu IGP Abdulrahman Kaniki na (kulia) ni Kamishna wa fedha na Usafirishaji wa watu na vifaa Clodwing Mtweve.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu akizungumza na Maofisa, Wakaguzi , Askari na watumishi raia wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Vikosi vya Jeshi la Polisi (hawapo pichani) katika kikao chake cha kwanza na watendaji hao baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.Kikao hicho kilifanyika jana katika Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Ostarbay jijini Dar es Salaam.(Kushoto) ni Naibu IGP Abdulrahman Kaniki, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja na Kamishna wa Kanda Maalumu Suleman Kova (kulia) ni Kamishna wa fedha na Usafirishaji wa watu na vifaa Clodwing Mtweve, DCI Issaya Mngulu na Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa.(Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi).



Na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.



Maofisa na Askari Polisi kote nchini wametakiwa kuendelea kufanya  kazi kwa kufuata misingi na maadili ya kazi za Polisi ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii jambo ambalo litafanya mapambano ya uhalifu na wahalifu kufanikiwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.



Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu wakati alipokuwa akizungumza na Maofisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi raia ndani ya jeshi la Polisi kutoka Makao makuu ya Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Vikosi vya Polisi,  kikao ambacho ni cha kwanza kuzungumza na Askari tangu ateuliwe na Mh.Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.



Alisema kazi za Polisi zinafanywa kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa hivyo kila Askari akifuata misingi hiyo na ushirikiano wa pamoja ukiimarishwa mapambano dhidi ya uhalifu yatafanikiwa.



 “Wananchi wanaimani kubwa na sisi hivyo ili tuweze kuboresha uhusiano na ushirikiano uliopo kati yetu na jamii hatuna budi kutoa huduma bora bila upendeleo” Alisema IGP Mangu.



Kwa Upande wake Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Abdulrahman Kaniki alisema muundo mpya wa utawala ndani ya Jeshi la Polisi wa kuwa na Kamisheni mpya lengo lake ni kuboresha utendaji wa kazi za Polisi hivyo Watendaji wa Jeshi la Polisi hawana budi kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.



Alisema lengo la Muundo huo ni muendelezo wa utekelezaji wa Maboresho ya Jeshi la Polisi yanayoendelea kutekelezwa ambayo yanahitaji kufanya kazi kwa weledi, usasa na Polisi Jamii ambapo katika kipindi cha utawala wao wataendelea kuyatekeleza.





Naye Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa alisema atahakikisha elimu ya Polisi jamii inawafikia Wananchi wote kwa kasi kubwa ili kuendelea kuboresha uhusiano uliopo kati ya Wananchi na Jeshi la Polisi ambapo atahakikisha Askari Kata na Wakaguzi wa Tarafa wanafanya kazi kwa ukaribu na wananchi ili kutokomeza uhalifu kuanzia ngazi ya familia.