Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman akizungumza kwenye mkutano na waaandishi wa habari  jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Msajili wa Mahakama, Ignas Kitusi. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam.
Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuharakisha mchakato wake wa kuandaa ripoti inayohusu migogoro ya ardhi nchini ili kutoa nafasi ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ardhi.
Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati ambao maeneo mbalimbali nchini yamekumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha wananchi kupoteza mali,mifugo,makazi na wengine kuuawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu sherehe ya Siku ya Sheria Nchini itakayofanyika Februari 3, mwaka huu, Jaji Chande amesema, “Ukiondoa idadi kubwa ya kesi za jinai, zinazofuata wa wingi ni kesi za migogoro ya ardhi, hasa za madai, mfano Mahakama Kuu ya Tanzania pekee kuna kesi za ardhi zaidi ya 6,000.”
Alisema asilimia 60 ya kesi hizo zinatoka kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.“Mfumo wa kutatua kesi za ardhi uko chini ya mamlaka tatu. Ngazi ya chini kabisa ni Baraza la Ardhi la Kijiji ambalo lipo chini ya Serikali za Mitaa na Halmashauri. Pili, ni Baraza la Kata,” alisema na kuongeza;
“Na tatu ni Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ambalo mamlaka yake ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Baada ya hapo ndiyo kinafuata Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu” alisema.
Alisema tatizo lililopo sasa ni kwamba ili uweze kutatua migogoro ya ardhi ni lazima uangalie kesi husika ipo katika ngazi gani na kusisitiza kuwa migogoro mingi ipo katika ngazi za chini ambazo zipo katika mamlaka nyingine.
“Hivi sasa mfumo wa migogoro ya ardhi na mashauri ya ardhi unaangaliwa upya na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo imetembelea mikoa yote nchini na kukutana na wadau wote ikiwamo, mahakama, Wizara ya Ardhi, wananchi na wanasheria hivyo ripoti hiyo ikitolewa itasaidia kuboresha sheria,” alisema.
Mahakama za mwanzo
Akizungumzia mahakama za mwanzo, Jaji Chande alisema, “Tanzania tuna mahakama za mwanzo 960 lakini zinazofanya kazi ni 803, kati ya hizo zinazofanya kazi mahakama 487 ndiyo zina mahakimu wa kudumu na nyingine 316 hutoa huduma kwa kutembelewa na mahakimu mara moja au mbili kwa wiki kutokana na mahakimu kutoishi maeneo hayo.”
Alisema kwa sasa kuna uhaba wa majengo zaidi ya 296 ya mahakama za mwanzo, kwamba kuna majengo 157 ya mahakama za mwanzo ambayo hayafanyi kazi kwa sababu ya uchakavu.
Alisema mahakama hizo zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuwapo katika majengo chakavu na nyingine zikiwa ndani ya majengo yanayomilikiwa na taasisi mbalimbali na Serikali, jambo ambalo alisema linazifanya mahakama hizo kuonekana kutokuwa huru.
Alisema miundombinu ya mahakama nyingi ni mibovu na kutolewa mfano mahakama za mwanzo zilizopo katika Wilaya za Bagamoyo, Mkuranga na Kisarawe mkoani Pwani kuwa hazina umeme na kusisitiza kuwa hali hiyo inachangia kuchelewa kutolewa kwa hukumu na haki kwa wananchi.Hata hivyo, Jaji Chande aliipongeza Serikali kwa kuongeza Bajeti ya Maendeleo ya Mahakama kutoka Sh17.8 bilioni mwaka 2012/13 mpaka Sh42.7 bilioni.
“Tunafungua mwaka mpya wa mahakama na kati ya hiyo bajeti tumepata Sh5.5 bilioni tu. Tutaendelea na malengo tuliyojiwekea ya kujenga mahakama za mwanzo 25 na kukarabati nyingine 10. Lakini kwa kiwango hiki cha fedha tulichopata ujenzi utakuwa mgumu,” alisema Jaji Chande.
Mahakama kuchomwa moto
Akizungumzia tabia ya wananchi kuchoma moto mahakama za mwanzo, alisema jambohilo linawanyima haki watu wenye kesi zao mahakamani na pia linachelewesha haki kutendeka.
“Tangu mwaka 2012 hadi sasa zimechomwa moto mahakama za mwanzo nne, mbili za mkoani Mtwara, moja mkoani Lindi na nyingine Njombe. Mahakama hizi zilikuwa na kesi nyingi na anayeathirika ni wananchi wenyewe kwani ushahidi unapotea na walioko rumande wataendelea kusota.”
Alisema mahakama za mwanzo zote nchini mwaka jana zilipokea kesi 29,507 na kuamua kesi 27,747, “Tatizo la mahakama za mwanzo ni zile kesi ambazo kila mwaka zinatakiwa kusogezwa mbele, mwaka jana kulikuwa na kesi 15,533 na mwaka huu Januari kuna kesi 15,303, idadi ya mrundikano wa kesi umebakia palepale.”
Operesheni Tokomeza
Akizungumzia kesi za watu waliokamatwa katika Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanza Oktoba 4 mpaka Novemba Mosi mwaka jana, ambayo ilisitishwa kwa muda kutokana na kukumbwa na kasoro katika utekelezaji wake, alisema mahakimu waliotoa hukumu ya baadhi ya kesi hizo hawakuwa miongozi wa vikosi vilivyokuwa vikiongoza operesheni hiyo.
“Watuhumiwa wengi walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika kipindi hicho mahakama ilipokea zaidi ya kesi 516 lakini zilizomalizika ni 188. Kesi hizi zimesikilizwa kwa mamlaka ambayo imepewa mahakama na zilisikilizwa mahakamani siyo kwenye misitu” alisema
Kesi za muda mrefu
Alisema mahakama imeandaa mipango ya kupunguza wingi wa kesi zinazosikilizwa kwa muda mrefu, “Kesi kusikilizwa kwa muda mrefu inategemea ipo katika mahakama ipi. Tumeanza kufanya tathmini ya kesi zote, pia Mahakama Kuu kuna vikao maalum vimefanyika kuondoa kesi hizo na tutahakikisha tunazipa kipaumbele kesi za muda mrefu kuliko kesi mpya.”