Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jenister Mhagama kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania, vitalazimika kufanya mabadiliko katika safu zake za uongozi kutokana na athari zilizosababishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.
Juzi, Ikulu ilitangaza mabadiliko katika baraza hilo ambayo yaliwaweka kando mawaziri na manaibu waziri watano, huku sura kumi mpya zikiingia, mabadiliko ambayo yameacha nafasi mbili wazi katika sekretarieti ya CCM na nafasi nne katika uongozi wa Bunge.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa jana ni waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya CCM; Dk Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, wakati Dk Migiro ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alisema jana kuwa viongozi wa sekretarieti ya CCM wanapoteuliwa kushika nafasi nyingine za Serikali, wanalazimika kuziacha nyadhifa zao katika chama.
Nape alisema kwa maana hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete atalazimika kuteua watu wa kuziba nafasi za Dk Migiro na Nchemba. “Huu ni utaratibu tuliojiwekea katika chama kwamba viongozi wa sekretarieti hawatafanya kazi mbili za chama na Serikali, kwa hiyo viongozi hawa pia wataziacha nafasi za chama,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema utaratibu huo hauwagusi wenyeviti wa chama hicho wa mikoa, ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ama manaibu waziri kwani uenyekiti si nafasi ya utendaji.
Katika uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wakati Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Hawa wanaweza kuendelea na nyadhifa zao za uenyeviti katika chama, huku wakiwa na nyadhifa serikalini, hii haina athari kwa sababu siyo watendaji wakuu wa chama,” alisema Nape.
Bunge pia litalazimika kuchukua hatua za kuziba nafasi zilizoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge pia Kiongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Jenister Mhagama ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Mahmoud Mgimwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na sasa ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.Naibu Spika, Job Ndugai alisema nafasi zilizoachwa wazi na wabunge hao zitazibwa kwa kuchagua wenyeviti wengine kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
“Mapema sana kamati za kudumu za Bunge zitakutana kabla ya Bunge la Katiba, nafasi ambazo zimeachwa wazi na walioteuliwa kuwa mawaziri zitazibwa kwa sababu kamati husika watachagua wenyeviti wao,” alisema Ndugai.
Kuhusu mawaziri walioachwa katika mabadiliko hayo, Ndugai alisema wao wanarejea kuwa wajumbe wa kamati.
“Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati, kwa hiyo tutawapanga kwenye kamati mbalimbali na hawazuiwi kuchaguliwa kuwa wenyeviti ikiwa watapangwa kwenye kamati ambazo wenyeviti wao wamechaguliwa kuwa mawaziri,” alisema Ndugai.
Mawaziri walioachwa kwenye uteuzi huo ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye, Dk Terezya Huvisa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mazingira) na Benedict Ole-Nangoro, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine ni Gregory Teu, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Philipo Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Viongozi hao wanaungana na wenzao wanneambao uwaziri wao ulitenguliwa na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Bunge kuhusu utekelezaji wa operesheni tokomeza ujangili.
Hao ni pamoja na waliokuwa Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
|
0 Comments