Picha juu na chini ni magari ya kuzolea taka ngumu ya kampuni mbalimbali yakiwa kwenye foleni ya kuingia Dampo la Pugu Kinyamwezi ambalo miundo mbinu yake ni mibovu na kupelekea zoezi hilo kuchukua zaidi ya siku 4 mpaka kufanikisha kufikia eneo maalum la kumwagia taka ngumu.
.Ni kutokana na kukwama kwa magari ya taka kwenye Dampo la Pugu
.Siku ya tatu sasa magari ya taka yamekwama
Na.Mwandishi wetu, MOblog
MIUNDOMBINU mibovu katika Dampo kuu la jiji la Dar es Salaam Pugu Kinyamwezi imesababisha magari makubwa ya kuzoa na kumwaga taka kukwama kwa muda wa siku tatu na kupunguza ufanisi wa kuzoa taka katika mkoa wa Dar es Salaam, MOblog inaripoti.
Mtoa taarifa wetu ambaye hakutaka kutajwa kwenye blogu hii, amesema kwamba uongozi wa Dampo Pugu umeshidwa kuweka utaratibu mzuri na kukarabati miundombinu ya dampo kwa muda mrefu na kusababisha msongamano mkubwa wakati wa kwenda kumwaga taka katika sehemu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari wa MOblog jana asubuhi, mtoa taarifa (Jina linahifadhiwa) amesema kwa muda wa wiki mbili sasa umwagaji wa taka katika dampo hilo siyo mzuri kabisa na inaweza kufika miezi kadhaa tangu dampo hilo lianze kuelemewa na uchafu kutoka kila kona ya jiji la Dar es Salaam.
“hali ni mbaya katika dampo la pugu kwa miezi kadhaa sasa na uongozi wa dampo wameshidwa kufanya kazi kwa tija na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa dampo katika jiji la Dar es Salaam,’ amesema mtoa taarifa
Amesema magari makubwa aina ya (Bulldozers) hayawafanyi kazi kabisa na kusababisha kukwama kwa kazi ya kumwaga taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi na msongamano mkubwa wa magari.
Mtoa taarifa anasema kuwa kutokana na matatizo hayo katika dampo la Pugu imesababisha baadhi ya taka kuoza kabisa na kuleta harufu kali kwa wakazi wa karibu wa dampo hilo na tishio la magonjwa ya mlipuko ni kubwa.
“kutokana na tatizo hili katika dampo la hapa Pugu hali za kiafya kwa wakazi wa karibu wa eneo ni ya hatari na magonjwa ya mlipuko yako mbioni kutokea,” aliongeza.
Pichani juu na chini hii ndio hali halisi ya muonekana wa eneo la Dampo la Pugu Kinyamwezi. Kwa hali hii kweli jamani hata hayo magari ya kuzoa taka yaliyopewa zabuni ya kukusanya taka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam yatadumu kweli....???
Hivi karibuni waandishi wa habari ikiwemo blog hii walitembelea eneo la dampo na kufanya mahojiano na badhi ya madereva, Devera wa gari la Kampuni ya usafi ya Green Waste Pro ltd Bw. Ramadhani Sufi alisema adha wanayoipata ni pamoja na kulala siku mbili na gari lenye mizigo ya taka katika mazingira ambayo hawawezi kula kitu kwa hofu ya kupata magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.
‘tunawaomba viongozi wa jiji kurekebisha hali hii ili waweze kutuepusha na magonjwa hatarishi kutokana na uchafu unaorundikana mahali pamoja kuanzia kwenye dampo hadi kwenye magari,” alisema.
Kwa upande wake Dereva Rajab Kavuzi wa kampuni ya Tirima Enterprises, amefafanua kuwa hali hiyo inasababisha kuwachafulia jina la kampuni yao na kuonekana kama hawafanyi kazi kumbe tatizo lipo kwenye utaratibu mzima wa Manispaa na suala la miundo mbinu.
Kwa upande dereva mwingine Bw. Likongo wa Eco Protection alisema kero ya kwenye dampo la taka lililopo maeneo ya Pugu Kinyamwezi ni za muda mrefu ambapo taka zimerundikana hadi barabarani na njia hazipitiki hata Magreda ya kuzoa hayana pakupita.
Gari la kampuni ya Tirima Enterprises likipita kwa shida kuelekea eneo maalum la kumwagia taka ngumu.
MOblog ilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Afya Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Dar es Salaam Bw. Membe Protus Membe ambaye aliahidi kupambana na tatizo la mrundikano wa magari ya taka yaliyokwama katika eneo la Dampo kutokana na ubovu wa miundo mbinu ya barabara unaopelekea kukwamisha zoezi la ukusanyaji taka katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar na kusababisha mrundikano wa taka nyingi kwa muda wa siku tatu.
Lakini mpaka sasa hali iko hivyo hivyo na imechukua takribani miezi sita tangu atoe ahadi hiyo ya kutatua kero na ubovu wa miundombinu kuelekea dampo la Pugu Kinyamwezi.
0 Comments