Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid.PICHA|MAKTABA
Mbeya. 
Mfanyakazi wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, EugeneVurugu amemtisha Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kuwa ikitokea amefariki dunia akiwa mkoani Mbeya, basi maiti yake italazwa kwenye sakafu hospitalini hapo.
Akizungumza kwenye mkutano wa wafanyakazi na naibu waziri huyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Vurugu alisema kitengo hicho kimezidiwa na wingi wa maiti zinazopelekwa hospitalini hapo.
Alisema kitengo hicho cha kina majokofu sita tu na hulazimika kuhifadhi miili kwa zamu ili angalau maiti zisiharibike.
“Hata wewe Waziri ukifa leo, hakuna pa kukuweka.
Utawekwa sakafuni kusubiri maiti nyingine zipoe halafu utaingizwa ndani kwa kuingizwa maiti mbili kwenye eneo la mtu mmoja,’’ alisema Vurugu.
Aliiomba Serikali ifanye haraka kuboresha kitengo hicho ili kuepusha tatizo la kuoza kwa miili ya marehemu.
Kumekuwa na malalamiko kuhusu uchache wa majokofu ya kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo na baadhi ya watumishi walisema hali kuwa mbaya zaidi inapotokea ajali ambayo inasababisha vifo vya watu wengi kwa wakati mmoja.
Vurugu alidokeza pia kuwapo kwa tatizo katika Idara ya Mifupa ya hospitali hiyo, akisema wakazi wengi wanaofika hapo kwa matatizo hayo anawaona wakiondoka kwenda Hospitali za Peramiho ya Ruvuma na Ikonda ya Makete huku wengine wakienda kwa waganga wa jadi kuunga mifupa yao.
Vurugu alizungumza baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Humphrey Kiwelu kusoma taarifa ya utendaji mbele ya Naibu Waziri iliyoonyesha hali iko shwari baada ya kudai kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa kiutendaji na katika utoaji huduma kwa wagonjwa.
Dk Kiwelu alisema hospitali yake ina mafanikio makubwa yakiwamo ya kuwa na maabara ambayo imekubalika katika kiwango cha kimataifa na kwamba majibu yanayotoka kwenye maabara hiyo kwa sasa yanakubalika hata Uingereza na Marekani.
Hata hivyo, alisema hospitali hiyo haina mashine ya CT Scan licha ya kuiomba kutoka serikalini tangu 2003.
Akijibu hoja mbalimbali za wafanyakazi, Dk Rashid aliwataka viongozi kujipanga na kuchangua vipaumbele kutokana na mafanikio mazuri yanayoonekana hospitalini hapo.
Alisema kwa kuwa hospitali hiyo imeongeza mapato ya ndani kutoka Sh60 milioni hadi Sh300 milioni kwa mwezi, ipo haja ya kutumia fedha hizo kuiboresha kwa kuangalia vitendea kazi zaidi na masilahi ya watumishi wote.