Mke wa aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu William Mgimwa, Jeni(katikati) akifuta machozi jijini Dar es Salaam jana,baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere. Picha na Michael Jamson
Dar es Salaam.
Vilio, simanzi na majonzi, vilitawala jana katika Uwanja za Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, wakati mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Dk William Mgimwa, aliyefariki dunia Afrika Kusini, ulipowasili nchini.
Mamia ya wananchi wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali na wanasiasa, jana walijitokeza uwanjani hapo kuanzia saa 4.30 asubuhi na ilipofika saa 7.45 mchana, ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), iliyobeba mwili huo ilitua uwanjani hapo.
Mjane wa marehemu, Jane Mgimwa akiambatana na watoto wake walishuka kutoka ndani ya ndege hiyo na kupokewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Baada ya mwili huo kuwasili , msafara wa magari ulianza kuelekea nyumbani kwa marehemu Mikocheni B Mtaa wa Ruvu, jijini Dar es Salaam ambapo ibada fupi ya Misa Takatifu ilifanyika na baadaye mwili wa Dk Mgimwa ulipelekwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kuhifadhiwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, Rais Jakaya Kikwete ndiye atakayewaongoza viongozi wa Serikali na wananchi kutoa heshima zao za mwisho kabla mwili haujapelekwa kijijini kwa marehemu, Magunga mkoani Iringa kesho.
Marehemu Dk Mgimwa, alifariki dunia Januari Mosi mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, iliyoko mjini Pretoria, alikokwenda kwa matibabu, zaidi ya mwezi mmoja na nusu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari, Januari 2 mwaka huu Waziri Lukuvi alisema, Serikali itaweka wazi chanzo cha kifo wakati wa kumuaga marehemu kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Hatuwezi kusema leo (Alhamisi, Januari 2 mwaka huu), hapa kwa sababu siyo busara. Hatujapokea hata taarifa ya daktari, nafikiri siku tutakayokuwa tukimuaga kwenye Viwanja vya Karimjee, ndipo tutapata nafasi ya kueleza hilo,” Lukuvi alinukuliwa akisema.
Baada ya shughuli ya kuaga mwili huo Viwanja vya Karimjee, utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini Magunga, kupitia Iringa mjini ili kuwapa nafasi wananchi kutoa heshima za mwisho, kisha kwenda kijijini ambako mwili huo utalala, kabla ya maziko yatakayofanyika kesho.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema kuwa marehemu Dk Mgimwa atakumbukwa kwa utendaji kazi wake uliotukuka, ambapo kwa muda mfupi aliweza kuijengea heshima Wizara ya Fedha iliyokuwa imepoteza imani kwa wananchi.
Siku nne baada ya taarifa ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa mama yake mzazi, Consolata Mgovano amesema kuwa hakupata taarifa kwamba mtoto wake alikuwa amelazwa hospitalini Afrika Kusini.Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga, Tarafa ya Kiponzero, Wilaya ya Iringa Vijijini jana, mama huyo alisema hakupata taarifa ya ugonjwa wa mtoto wake hadi alipovumishiwa kuwa amefariki kwenye taarifa iliyosambaa kwenye vyombo vya habari.
“Mimi mama yake mzazi, sikuwahi kufahamu, wala kupata taarifa kama mtoto wangu anaumwa na amepelekwa kutibiwa. Wala sikuwahi kufahamu anasumbuliwa na ugonjwa gani, badala yake siku za nyuma nilipata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa amefariki, lakini taarifa hizo hazikuwa na ukweli,” alisema Consolata.
Alisema taarifa hizo zilimsumbua kwani hakujua tatizo lililosababisha mtoto wake kupoteza maisha.
Mama huyo alisema Marehemu Mgimwa ndiye mwanawe wa kwanza kati ya watoto wanane aliozaa.
“William ndiye aliyekuwa tegemeo langu kubwa, kwa sababu alikuwa anaisaidia familiapamoja na kuwasomesha watoto hawa wa marehemu ndugu zake. Sasa hivi sijui ni naniatakayewasaidia na kuwaendeleza katika kielimu,” alisema mama huyo.
Naye dada wa marehemu, Rosemary Mgimwa alisema kuwa kaka yao alikuwa nguzo ya familia hivyo, amewaachia pengo kubwa na hawajui wataliziba vipi.
Habari ya nyongeza na Berdina Majinge, Iringa.
|
0 Comments