Mrembo wa Redds Miss Kanda ya Mashariki , Diana Laizer , ambaye ni Miss Morogoro 2013 akimkabidhi zawadi ya vyakula Mkurugenzi wa Kituo cha Amani cha watu wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo ,
Padri Beatus Sewando ( kulia) wakati alipotembelea Kituo hicho siku ya
kwanza ya mwaka mpya 2014 akiwa na mshindi wa tatu wa Miss Morogoro,
Muzne Abduly pamoja na Mratibu wa Miss Kanda ya Mashariki , Alex Nikitas ili kuwafariji na kusherekea kwa kula chakula nao.( Picha na John Nditi).
|
Picha ya pamoja
======== ====== =========
REDDS MISS KANDA YA MASHARIKI AMBAYE PIA NI MISS MORO 2013 ASIFIWA ALIVYOJITOA KUSAIDIA WATU WENYE ULEMAVU WA VIUNGO NA MTINDIO WA UBONGO KITUO CHA AMANI.
Na John Nditi, Morogoro
KITUO cha Amani kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro na kinachowahudumia Watu wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo, kutoka sehemu mbalimbali mkoani hapa kimepongeza Redds Miss Kanda ya Mashariki , Diana Laizer , kutokana na kuonesha upendo na kulijali kundi la watu wa aina hiyo kwa kutoa msaada wa vyakula.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Padri Beatus Sewando , siku ya kwanza ya mwaka mpya 2014, kwa Miss Kanda ya Mashariki ambaye pia ni Miss Morogoro 2013.
Mrembo huyo ambaye kwa sasa ni Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) siku hiyo alikitembelea Kituo hicho akiwa na mshindi wa tatu Miss Morogoro, Muzne Abduly , pamoja na Mratibu wa Miss Kanda ya Mashariki, Alex Nikitas ambapo alitumia siku hiyo kula na kucheza nao burdani za ngoma.
Mkurugenzi wa Kituo hicho alisema , watoto wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo wanayo mahitaji mengi ukiwemo kuwaonesha upendo na wanapotembelewa na wageni hasa nyakati za sikukuu na kupatiwa zawadi wanapata faraja kubwa kwa kujiona nao ni sehemu ya jamii.
“ Binafsi yangu nikiwa Mkurugenzi wa Kituo hiki , walengwa na wazazi wao tumefurahi na tumefarijika kwa uamuzi wako kututemebela siku ya mwanzo ya kuanza mwaka huu wa 2014 , umetuletea zawadi ya vyakula” alisema na kuongeza.
“ Japo wewe mwenyewe umesema ni kidogo , lakini kwetu sisi tunakiona ni kikubwa , watoto wamefurahi , kutoa ni moyo na si utajiri , kikubwa umejitoa kujakushinda nasi leo hii” alisema Padri Sewando.
Hata hivyo alisema , kituo hicho cha Amani kina watoto 42 wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo na hakina ufadhili wa n je na wadani , kinawategemea watu wenye kujitoa na kitendo cha Miss Kanda ya Mashariki kukitembelea na kutoa zawadi ya vyakula ndiyo ufadhili wenyewe.
Pamoja na hayo alisisitiza kwa kusema “ Kituo hakina ufadhili na nina waomba wote wanaoshinda kuwa Miss Morogoro waige mfano wa Miss Diana , ambaye amejitoa na kuutumia muda wake kusaidia jamii isiyojiweza” alisema na kusisitiza kuwa.
“ Jambo hili ni kubwa na linayapa hadhi mashindano haya ambayo jamii yetu siku zote imekuwa na fikra potufu ya kuwa Ma Miss ni wapenda starehe na anasa, lakini sivyo ilivyo miaka ya hivi sasa ” alibainisha.
Naye Redds Miss Kanda ya Mashariki, alisema kuwa , moja ya majukumu yake ni kusaidia jamii hasa makundi ya watoto yatima na wenye ulemavu sambamba na wanaishi katika mazingira magumu , wakiwemo wa Kituo hicho.
Hivyo alisema, kwa kutambua jukumu hilo, siku hiyo ya mwaka mpya aliamua kukitembelea Kituo hicho na kutoa msaada wa vyakula ,kula nao na kuburudia kwa pamoja ili kuonesha upendo.
Hivyo alitoa wito kwa washiriki wengine wa Urembo wajitokeza kusaidia makundi kama hayo kile kidogo wanachokuwa nacho kwani wao pia ni sehemu ya jamii inayohitaji kutunzwa kiafya , kielimu na kijamii. |
0 Comments