Rais wa Uganda Yoweri Museveni (kushoto), Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete (wa pili kulia) na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein wakipokea saluti wakati wa garide la maadhimisho, Unguja, jana.
Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania itakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopitishwa na Bunge.
Akihutubia taifa katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja jana, Dk Shein alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetimiza wajibu wake na imefanya kazi kubwa na kukabidhi ripoti kwa Rais Jakaya Kikwete.
Dk Shein alitoa kauli hiyo huku vyama vya CCM na CUF ambavyo vimeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) vikitofautiana kuhusu mapendekezo ya kuwa na muungano wa Serikali tatu yaliyotolewa katika  Rasimu ya Katiba hiyo.
Wakati CCM ikipinga mfumo wa Muungano wa Serikali tatu na kutaja kuwa mfumo huo ni hatarishi na unaweza kuvunja muungano uliopo, CUF imeunga mkono mapendekezo hayo na kueleza  kuwa muundo huo ndiyo utakaomaliza kero za Muungano.
“Hatua zilizobakia nazo zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo hatimaye tuweze kupata Katiba Mpya itakayoliongoza Taifa letu kuimarisha Muungano wetu,” alisema Dk Shein.
Rais huyo wa Zanzibar alisema ni jambo la faraja kuona Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliweza kukamilisha kazi yake kwa muda mwafaka na kwamba wajumbe wake, pamoja na Rais Kikwete wanastahili pongezi kwa kusimama imara katika kusimamia mchakato huo.
Aliahidi kuwa SMZ itaendelea kushirikiana na Serikali ya Muungano katika kuendeleza na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya pande mbili na kuwataka wananchi kulitumia Bunge la Katiba kutoa maoni yao kwa kupitia wabunge na wawakilishi kabla ya hatua ya mwisho ya kura ya maoni kufanyika.
Hali ya Kisiasa Z’bar
Dk Shein alisema Serikali ya Muungano na SMZ ziko katika mikono salama na kila upande utaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya katiba, haki za binadamu na utawala bora ili kulinda amani, utulivu, mali na maisha ya watu.
Hata hivyo alisema hatua hiyo itafikiwa ikiwa viongozi, wanasiasa, dini, Serikali na viongozi katika jamii watatii sheria na kutekeleza wajibu kwa kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa.
Dk Shein alisema Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalifanyika ikiwa ni hatua ya wananchi kupinga vitendo vya kudharauliwa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kutokuheshimiwa katika nchi yao na ukombozi huo ulitekelezwa na Chama cha ASP kilichoanzishwa Februari 5 mwaka 1957.
“Leo tunapoadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi, hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu, waasisi wa ASP walioongozwa na Hayati Mzee Abeid Karume, tutawakumbuka kwa ushujaa wao na jitihada zao za kupigania haki, kuleta usawa na kuleta maelewano,” alisema Dk Shein.Leo mapumziko
Dk Shein na Rais Jakaya Kikwete wametangaza kuwa leo itakuwa ni mapumziko kwa Watanzania wote ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Wakati Dk Shein akitangaza uamuzi huo kwa ajili ya watu wa Zanzibar, pia Rais Kikwete aliyekuwepo Jukwaa Kuu alimnong’oneza kwa kumweleza kuwa watu wa Bara nao watapumzika.
Baadaye ilitolewa taarifa rasmi na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ofisi ya Rais iliyoeleza kuwa Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo ili kutoa fursa kwa Watanzania wote kusherehekea mapinduzi hayo kutimiza miaka 50.
Makomandoo, mbwa
Kati ya vitu vilivyonogesha sherehe hizo ni kikosi cha makomandoo kilichoonyesha umahiri wake katika utendaji kazi hasa kuonyesha ukakamavu pamoja na kikosi cha mbwa, ambacho hutumia mbwa katika kusaka wahalifu.
Makomandoo waliingia kwa staili ya aina yake na walishangaza umati kwa mmoja kuvunjiwa matofali mawili kifuani, kupigwa na ubao kichwani na ubao kuvunjika, kuruka urefu wa futi 10 na kufikia chini kwa staili ya msamba.
Mbwa wa polisi nao walikuwa kivutio, walionyesha umahiri kwa kufichua mkoba uliokuwa na hashishi kati ya mikoba minne iliyowekwa uwanjani hapo.
Ndege za kijeshi, magari ya deraya, vifaru vya aina mbalimbali vilipita mbele ya wananchi waliokuwa wakishangilia.
Kilichovutia zaidi ni kikosi maalumu cha Jeshi la Tarbush ambacho kilivalia kaptura na kofia ya kitunga (tarbush) yenye rangi nyekundu na uzi mweusi na kamanda wa kikosi hicho alivutia zaidi wakati akitoa amri na kuwaadhibu askari wake waliokwenda kinyume na maelekezo yake. Rangi mbalimbali vilipamba uwanja hasa kwa vijana wa halaiki waliokuwa wamevalia mavazi ya rangi za njano, kijani na nyeusi ikiwa ni rangi za Bendera ya Zanzibar na mapambo mbalimbali.
Kigeni katika shughuli hiyo ni vijana wadogo walioingia katika uwanja huo wakijipanga kwenye gwaride, wakiwa wamebeba mfano wa bunduki na kufanya maonyesho yanayofanana na ya kijeshi.
Museveni na mafuta, gesi
Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliungana na Rais wa Comoro na mwakilishi wa China kutoa salamu katika sherehe hizo.
Akitoa salaam zake, Rais Museven aligoma na kuzungumza Kiingereza akisema hayupoLondon hivyo hawezi kuzungumza Kiingereza.
Katika hotuba yake, Rais huyo alisema: “Tusigombane kwa sababu ya utajiri wa mafuta na gesi tunayoyavumbua kwenye nchi zetu kwani binadamu ndiyo utajiri mkubwa kuliko kitu chochote.”
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah na Salma Said, Zanzibar na Raymond Kaminyoge, Dar