Rais Kikwete.
Nichukue pia fursa hii kuwapa pole Watanzania wenzangu kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wetu wa Fedha, Dr. William Mgimwa aliyefariki akiwa Afrika Kusini Jumatano iliyopita baada ya kuwa ameugua kwa muda mrefu kidogo. Ni pigo kwetu kama taifa, kwani tumeondokewa na mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kuaminiwa na Rais hadi kukabidhiwa ofisi nyeti kabisa ya nchi yetu.
Hatuna tunachoweza kufanya, isipokuwa ni kumuombea sana kwa Mungu ili roho yake ipate pumziko la amani. Ingawa ni msiba wa kitaifa, naomba kwa namna ya pekee kabisa, niwape pole wanafamilia wote katika wakati huu mgumu na Mwenyezi Mungu awape nguvu.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa nipasue jipu langu la leo. Wote tunakumbuka kwamba hivi karibuni, mawaziri wanne waliondolewa katika nafasi zao kufuatia ripoti ya Bunge juu ya makosa yaliyotokea wakati wa utekelezaji wa Oparesheni Tokomeza Ujangili, iliyokuwa na lengo la kuwalinda Tembo, Faru na wanyama wengine wa porini wanaowindwa sana na wawindaji haramu.
Baada ya mawaziri hao kuondoka ofisini, watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao, juu ya nani anastahili kushika nafasi hii na nani anatakiwa kuungana na wengine walioondolewa. Katika hali ya kusikitisha, baadhi ya watu wanaripotiwa kumshawishi Rais kwa namna wanavyojua wao, ili mradi tu nao wafikiriwe kupewa nafasi ya uwaziri, ambayo Rais anatarajia kutangaza hivi karibuni.
Nijaribu kushauri tu kwamba huu ni wakati wa kumuacha Rais Jakaya Kikwete afanye uamuzi wake mwenyewe, juu ya nani anafaa kushika nafasi gani. Ni wakati wa kuendelea kuamini kuwa kiongozi huyu ni makini, anajua mahitaji ya nchi na anafahamu vyema matarajio waliyonayo Watanzania.
Kuanza kumtajia majina ya watu ni kuingilia majukumu yake na wakati mwingine inaweza hata kumchanganya, akajikuta amefanya uteuzi utakaokuja kulalamikiwa baadaye. Miaka yake nane akiwa Ikulu, imetosha sana kujua aina ya watu anaotaka kufanya nao kazi. Wengine wanajipendekeza wakijua kabisa hawana uwezo wa kufanya kazi.
Wapo ambao aliwaamini, lakini baadaye wakamwangusha. Wapo waliopigiwa debe wapewe nafasi, lakini mwishowe waliharibu. Hii ndiyo imesababisha kuwe na malalamiko kutoka kwa baadhi ya Watanzania kuwa Rais anafanya uteuzi wake kirafiki badala ya uwezo wa kazi, jambo ambalo siyo sahihi.
Rais anahitaji timu imara ili amalize vizuri miaka yake miwili iliyobaki, ambayo pia ina changamoto nyingi pengine kuliko hata hii aliyokaa madarakani. Tukumbuke, huu ni mwaka ambao taifa litapata katiba mpya, jambo ambalo linahitaji sana umakini wa mkuu wa nchi.
Katika muda wake ofisini, tumeshuhudia jinsi gani alivyojitahidi kuboresha timu yake kila wakati, ilimradi tu aweze kufikia malengo yaliyowekwa. Ingawa kuna baadhi ya watu wanabeza, lakini ukweli ni kwamba taifa limepiga hatua kubwa katika maendeleo wakati wa uongozi wa awamu hii ya nne.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
|
0 Comments