Makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.PICHA|MAKTABA 
Arusha. Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kimeifikisha mahakamani Serikali ya Burundi kwa madai ya kukiuka haki za msingi za kujipatia kipato halali Wakili Isidore Rufyikiri aliyepigwa marufuku kufanya shughuli za uwakili nchini humo.
Shauri hilo namba 3 la mwaka 2014, lilisikilizwa jana na jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), mdaiwa wa kwanza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Burundi hakufika mahakamani.
Mdaiwa wa pili katika shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji hao wakiongozwa na Jaji Isaac Lenaola wa Kenya akisaidiana na Jaji Faustine Ntezil wa Rwanda na John Mkwawa wa Tanzania, ni ofisi ya Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), anayewakilishwa na Wakili wa Jumuiya, Wilbert Kahwa.
Licha ya maombi mengine, Wakili Richard Onsongo kutoka Kampuni ya Uwakili ya Onsongo & Company ya nchini Kenya anayeiwakilisha EALS, aliomba mahakama kutoa amri ya kusitisha uamuzi wa Serikali ya Burundi kumzuia Wakili Rufyikiri kufanya kazi ya uwakili nchini humo.
Wakili Onsongo aliomba Mahakama kutoa amri ya upande mmoja bila Mwansheria Mkuu wa Burundi kuwasilishwa, kuondoa zuio la kutotoka nje ya Burundi alilowekewa Wakili Rufyikiri na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini humo.
Kabla ya kunyang’anywa leseni ya uwakili na kupigwa marufuku kutoka nje ya mipaka ya Burundi, Wakili Rufyikiri alikuwa ni Rais wa Chama cha Wanasheria nchini humo.
Wakili Kahwa aliomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo akidai hayakidhi mahitaji ya kisheria ya pande zote kupewa taarifa na muda wa kutosha kujibu hoja, huku akiieleza mahakama kuwa mdaiwa wa pili, Katibu Mkuu wa EAC alipokea hati ya mashtaka Februari 22 mwaka huu, siku tano kabla ya shauri kusikilizwa.
Hata hivyo, Jopo la majaji halikukubaliana na hoja hiyo kwa kueleza kuwa amri ya kuzitaka pande husika kufika mbele ya mahakama jana ilitolewa na mahakama yenyewe Februari 19, mwaka huu kutokana na dharura ya maombi na hoja zilizowasilishwa mbele yake na wadai.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama ilitoa muda wa siku 15 hadi Aprili 14, mwaka huu kwa upande wa wadaiwa kuwasilisha hoja zao kujibu maombi ya wadai ambao nao watayajibu ndani ya siku 21 kabla ya shauri hilo kusikilizwa Aprili 4, mwaka huu.
Mahakama hiyo imekuwa ikipokea kesi mbalimbali kutoka kwa raia wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
Tayari, aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzani kupitia Chadema, Anthony Komu amewasilisha maombi kupinga utaratibu unaotumiwa na Bunge la Tanzania kupata wabunge wa EAC.
Pia, baadhi ya wabunge kutoka Kenya waliwahi kuwasilisha kesi kupinga utaratibu uliotumika kupata wabunge, mahakama hiyo iliwapa ushindi baada ya kuridhika taratibu kukiukwa.