Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akimtambulisha mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa, Godfrey William Mgimwa jana. Picha na Bashir Nkoromo
Dar es Salaam.
Wakati Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM ikimpitisha Godfrey Mgimwa (32) kuwa mgombea wa chama hicho Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa, Kamati Kuu ya Chadema inakutana keshokutwa kuteua jina la mgombea wake.
Mgimwa ni mtoto aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliyefariki Januari Mosi mwaka huu, Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema jana kuwa jina hilo lilipitishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Ikulu chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.
“Kwa hiyo tunatangaza rasmi kwamba Godrey Mgimwa ndiye mgombea wa chama chetu Jimbo la Kalenga,” alisema Nape.
Kabla Kamati Kuu haijampitisha, Mgimwa wiki iliyopita alishinda kura za maoni kwa kupata 342, huku mshindi wa pili Jackson Kiswaga akipata kura 170, watatu ni Hafsa Mtasiwa aliyeambulia kura 42.
Tayari Tume ya Uchaguzi imepanga Machi 16, mwaka huu kuwa siku ya uchaguzi Jimbo la Kalenga.
huku kampeni zikifanyika kuanzia Februari 19 hadi Machi 15.
Akifafanua, Nape alisema wana CCM wana imani na mgombea huyo kuwa atashinda kwa kishindo na kulichukua jimbo hilo.
Naye Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema mbali na CC kufanya uteuzi, pia itapokea ya uchaguzi wa madiwani uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Makene alisema pia kuwa Kanda mbalimbali kulikofanyika uchaguzi huo, zilipewa jukumu moja la kuhakikisha mambo yanakwenda vema, lakini kutokana na matokeo yaliyopatikana, kila Kanda inatakiwa kuandika ripoti ya uchaguzi huo kabla ya CC kutoa kauli rasmi ya kufanyika uchaguzi huo.
Akijibu shutuma kwamba, jimbo hilo linarithishwa kifamilia, Nape alisema chama hicho hakiwezi kumnyima mwanachama yeyote haki ya kuwania kwa sababu tu wazazi wake waliwahi kuwa viongozi.“CCM haiwezi kumzuia Godfey kuwania eti kwa sababu ni mtoto wa marehemu Dk Mgimwa, yeye ana haki ya kuwania kama watu wengine tunachoangalia ni uwezo wake na hilo limeonyeshwa baada ya wananchi wa Kalenga kumpa ushindi wa kishindo,” alisema.
Alivionya vyama vya upinzani kwamba muda wa kampeni ukifika kufanya mikutano ya kistaarabu kwa sababu chama hicho hakitavumilia vurugu.
Aliwapiga kijembe Chadema kuwa wanatakiwa kuandaa Chopa nyingi zaidi ili ziweze kuwazungusha katika kata 13 ilizopo kwenye Jimbo hilo ili wajaribu bahati yao.
Naye Mgimwa akizungumza, aliishukuru Kamati Kuu kwa kumpitisha kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo.
“Natoa shukurani zangu za dhati kwa Kamati Kuu kunipitisha kugombea ubunge, sitawaangusha,” alisema Mgimwa ambaye anafanya kazi katika Benki ya Stanbic.
Kamati Kuu jana jioni iliendelea na kikao chake ikiwa ni maandalizi ya Kikao cha Kamati ya Maadili kitakachokaa kesho mjini Dodoma.
Kikao hicho kinatarajia kuwahoji baadhi ya vigogo wa chama hicho waliokiuka maadili ikiwemo kutangaza kugombea urais kinyume na taratibu za chama hicho.
|
0 Comments