Wanachama wa Chadema wakikimbia huku wakiwa wamembeba Mbunge wa Iringa Mjini, Mchugaji Peter Msigwa mara baada ya kupatiwa dhamana na Mahakama ya Wilaya ya Iringa jana. Picha na Said Ngamilo
Iringa.
 Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kufanyiwa hujuma, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa amekuwa mbunge wa pili kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kujeruhi.
Msigwa alifikishwa jana katika Mahakama yaWilaya ya Iringa akidaiwa kutenda kosa hilo juzi kwa kumjeruhi kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Kaita kwenye mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa udiwani wa Chadema katika Kata ya Nduli, Ayub Mwenda.
Juzi, katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mbunge wa Maswa Mashariki, SylvesterKasulumbayi na wenzake 15, walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuwajeruhi wafuasi watano wa CCM katika kampeni za udiwani na kulazwa rumande. Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alijisalimisha polisi kutokana na taarifa za kutafutwa kwake kutokana na tuhuma zinazohusiana na uharibifu wa mali katika kampeni za udiwani. Aliachiwa baadae.
Mashtaka ya Msigwa
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo GodfreyIsaya, Wakili wa Serikali, Elizaberth Swai alidai kuwa mnamo Februari 5 mwaka huu katika Kata ya Nduli, Msigwa alimjeruhi Kaita kinyume cha sheria sura ya 12 ya mwaka 2002 kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu.
Mchungaji Msigwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni iliyowekwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Lilian Msomba.
Chadema walia na polisi
Kutokana na matukio hayo, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chadema, Kigaila Bensonaliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa kuwatia nguvuni wale wote ambao wanahusika na vitendo kuwajeruhi wanachama wao badala ya kupindisha ukweli.
Akizungumzia vurugu zinazoendelea katika kampeni za kuwania udiwani kwenye kata 27, Kigaila alisema uongozi wa CCM na Polisi kwa pamoja wanajua kinachotokea lakini wanakifumbia macho.
“Watu wetu wanajeruhiwa, wanakamatwa wanawekwa mahabusu na tunapotoa taarifa polisi hazichukuliwi hatua. Inakuaje watu wanaoumiza watu wetu hawakamatwi? Polisi wanatakiwa kuzingatia sheria na kanuni kwa wote,” alisema Benson.
Kasulumbayi apata dhamana
Mahakama ya Wilaya ya Kahama jana mchana ilimwachia kwa dhamana Kasulumbayi aliyekuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za kuwacharanga mapanga wafuasi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama.Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Gadiel Mariki katika uamuzi wake mdogo kwenye kesi iliyokuwa ikimkabili mbunge huyo na wenzake, alitupilia mbali cheti cha kiapo cha kuzuia dhamana, kwa madai kiliandikwa bila kufuata taratibu za kisheria.
Mariki alisema cheti hakikuonyesha taarifa yamajeruhi watatu ambao hali zao ni mbaya imetolewa na nani na nafasi ya mkurugenzi wa kiapo haikutiwa saini wala kuonyesha ni kiapo cha dini gani.
Mara baada ya kutupa kiapo hicho, dhamana ilibaki wazi kwa watuhumiwa wote 13 kwa masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, mmojawapo akiwa na hati ya vielelezo vya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua Sh10 milioni.
Hata hivyo, Kasulumbayi pekee ndiye aliyetimiza masharti na kufanikiwa kupata hati ya nyumba iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Kahama, Juma Protas. Watuhumiwa wengine 12 wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Buselesele, ChristianKagoma walirudishwa rumande.
Lema ajisalimisha
Kwa upande wake, Lema, alijisalimisha polisi baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Arusha, Gillis Mrotto akitakiwa kufika kwa mahojiano.
Lema alifika polisi jana mchana akiongozana na viongozi na wafuasi kadhaa wa Chadema Wilaya ya Arusha ambapo alipokewa na Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Faustine Mafwere kabla ya kukabidhiwa kwa askari mwenye cheo cha Mkaguzi kwa ajili ya mahojiano.
Hata hivyo, mbunge huyo alipinga kuhojiwa hadi atakapokuwapo wakili wake, Method Kimomogoro ambaye hakuweza kupatikana.
Baada ya majadiliano na uongozi wa polisi, walifikia mwafaka wa Lema kutakiwa kufika kituoni hapo Jumanne Februari 11, mwaka huu akiwa na wakili wake ili achukuliwe maelezo.
Akizungumza baada ya kuachiwa, Lema alisema polisi walimjulisha kuwa anatakiwa kuhojiwa kuhusiana na kosa la uharibifu wa mali na matukio ya kampeni zinazoendelea Kata ya Sombetini, jijini Arusha.
“Sijajua mlalamikaji, lakini polisi wameniambia kuna magari mawili ya abiria (Toyota Hiace), yanadaiwa kuvunjwa vioo na wafuasi wa Chadema wanaodaiwa waliongozwa na mimi,” alisema Lema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kuwa baada ya upelelezi, jeshi hilo litakabidhi majalada ya tuhuma hizo ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uamuzi zaidi.Alisema pamoja na suala la Lema, jeshi hilo linakamilisha upelelezi kwenye majalada mengine yaliyofunguliwa kuhusiana na matukio yanayotokea Sombetini katika kampeni.