Aliwahi kuzipamba kurasa za Jarida la Forbesmwaka 2011 akiwa ni miongoni mwa wanawake tisa wa kiafrika wanaoongoza kwa utajiri. Siyo hivyo tu, bali ana cheo kikubwa akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji, wa Benki ya Dunia(WB).
Ni Dk Mamphela Ramphele, mwenye umri wa miaka 66 ambaye hivi karibuni alitangaza kuwania nafasi ya urais nchini humo, kwenye uchaguzi ambao utafanyika miezi minne ijayo nchini Africa Kusini.
Ramphele amedhamiria kuwa mwanamke wa kwanza nchini humo kuwania urais na pia kuutaja utajiri wake ambao ni randi 55 milioni (Dola za Marekani 5.5milioni).
Uchaguzi wa Rais na wabunge ambao unatarajiwa kufanyika Aprili au Mei mwaka huu, ni wa kwanza baada ya kifo cha Rais mstaafu Nelson Mandela.
Ramphele, ambaye ni mwanasiasa mkongwe, mhadhiri na mhudumu wa afya, mwenye mafanikio makubwa na Mkurugenzi wa sekta nyeti ya uchimbaji wa madini, alikaririwa akisema maamuzi yaliyofanywa na chama chake ya kumchagua kuwa mgombea wa urais ni yenye tija kwa Waafrika wa Kusini.
“Nimefarijika na kukubali mwaliko huu wa chama cha Democratic Alliance,(DA) kuwa mgombea wa urais kwa mwaka 2014,” alisema Dk Ramphele.
Ramphele alizaliwa jimbo la Bochum, Kaskazini mwa Transvaal,(hivi sasa Limpopo). Alimaliza elimu ya sekondari, Setotolwane, mwaka 1966 na akajiunga na kozi fupi ya tiba kwenye chuo kikuu cha Kaskazini.
Mama yake, Rangoato Rahab, na baba yake Pitsi Eliphaz Ramphele walikuwa walimu wa shule ya msingi. Mwaka 1944 baba yake alipandishwa cheo na kuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Stephanus Hofmeyer.
Akiwa Chuo Kikuu, Ramphele alianza kuvutiwa na siasa za wanafunzi na ubaguzi wa rangi na hapo alikuwa mwanzilishi wa Chama cha Watu Weusi(BCM). Muungano huo wa wanafunzi kupinga ubaguzi wa rangi ulikuwa chanzo cha kukutana na Steve Biko, miongoni mwa wanasiasa wakongwe wa Afrika Kusini. Urafiki kati ya Ramphele na Biko, ulikua na kuzua mapenzi ambayo yaliwapa zawadi ya watoto wawili, Lerato Biko, (aliyezaliwa mwaka 1974) na Hlumelo Biko(1978). Hata hivyo, Lerato alifariki baada ya kuugua nimonia.
Mwaka 1955 Ramphele alishuhudia mgogoro kati ya mbaguzi wa rangi, Dominee na watu wa Kijiji cha Kranspoort jambo ambalo liliamsha ari yake ya kuwa mwanasiasa.
Miaka ya 1970 na kuendelea, Ramphele aliendelea na shughuli za kisiasa akiwa bega kwa bega na Steven Biko, Barney Pityana pamoja na wanafunzi wengine wanaharakati wa chuo cha tiba. Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi la chama kabla ya kupata cheti chake cha Chuo Kikuu.Alipata nusu ajira katika Hospitali ya Mfalme Edward wa nane na baadaye alihamia Hospitali ya Livingstone, Port Elizabeth.
Mwaka 1974, Ramphele aliendeleza harakati zake ambapo alikuwa akiwahamasisha watu wajiunge kwenye miradi ya kijamii. Akijumuisha na elimu yake ya tiba, alikuwa pia mkurugenzi wa Mpango wa Wanajamii Weusi(BCP) Mashariki ambako Biko alipigiwa marufuku kuonekana.
Agosti mwaka 1976, Ramphele aliwekwa kizuizini chini ya sheria namba 10 ya ugaidi akiwa ni mtu wa kwanza kuwekwa kizuizini kwa sheria hiyo mpya.
Mwaka 1977, Ramphele alizuiwa asitoke maeneo ya Tzaneen, Kaskazini mwa Transvaal ambako alibaki hadi mwaka 1984. Hata hivyo, muumini mmoja wa kanisa la kijijini hapo aliwaandaa watawa wawili, wa Kiafrika, ambao walimtoa mafichoni na kumtafutia nyumba kwenye Lenyenye, Tzaneen ingawa aliendelea kufuatiliwa na polisi.
Akiwa hapo, alipata msaada wa hati ya kusafiria kutoka kwa Mbunge wa Chama cha PP, Helen Suzman ambayo aliitumia kusafiria kwenda nchi za nje kujinoa kielimu na kisiasa.
Mwaka 1983 alimaliza shahada yake ya kwanza ya Mawasliano kwenye Uongozi kutoka Chuo Kikuu cha UNISA ambako alijiunga tangu mwaka 1975. Alimaliza pia Diploma ya Afya ya Umma Chuo Kikuu cha Witwatersand.
Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa msaidizi wa masuala ya utafiri chuo Kikuu cha Cape Town, na mwaka 1996 wakati huo huo aliteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho akiwa ni mwanamke wa kwanza mwafrika kushika nafasi hiyo kwenye Vyuo Vikuu vya Afrika Kusini.
Mwaka 2000, Ramphele alikuwa miongoni mwa Wakurugenzi wakuu wanne wa Benki ya Dunia akiwa na majukumu ya kuangalia shughuli zinazofanywa na benki hiyo. Ni mwafrika Kusini wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Pamoja na nafasi nyeti ya WB, Ramphele aliwahi kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mo Ibrahim ambayo inashughulikia utawala bora na uongozi Afrika.
Mwaka 2013, alionyesha dalili za kurejea kwenye siasa za nchini Afrika Kusni akiachia ngazi kwenye nafasi yake ya Uenyekiti wa Gold Fields. Februari 18, 2013 alitanganza kuanzisha chama kipya cha siasa, kilichopewa jina la Agang(maana yake ni Jenga) ambacho kilipanga kukipa changamoto chama cha ANC, kinachotawala nchini humo.
Hata hivyo, kuingia kwa Ramphele kwenye siasa kumepokelewa kwa changamoto na ukosoaji mwingi kutoka kwa wachambuzi wa masuala ya siasa. Wakosoaji hao walidai kuwa amekuwa akitoa taswira mbaya kwa marehemu Biko katika mikutano yake ya siasa.Kujiunga na kuteuliwa kwa Ramphele na chama cha DA kama mgombea wa Urais kunatajwa kuwa ni sehemu ya mapinduzi ya chama hicho ambacho kina wazungu wengi kukusanya kura za watu weusi.
Tathmini ya hivi karibuni imeonyesha kuwa, Chama cha ABCM kimeshuka kwa asilimia 53 na Chama cha DA kimepanda kwa asilimia 18. Wakati huo huo, mwanachama mkongwe wa ANC, Julius Malema, alikihama chama hicho na kuunda chama kipya cha Economic Freedom Fighter.
|
0 Comments