Stori: Shakoor Jongo
STAA wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja amejikuta katika hali mbaya kufuatia kunyweshwa sumu na mtu ambaye hakuweza kufahamika mara moja.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumapili iliyopita maeneo ya Tegeta jijini Dar katika Klabu ya Seventy One ambayo alikwenda kujiachia na marafiki zake.Chanzo cha uhakika, kilipenyeza habari kuwa, Kajala alinyweshwa sumu hiyo kupitia kwenye glasi ambayo aliwekewa juisi ambapo haikuweza kufahamika mara moja kuwa aliwekewa kabla au baada ya mhudumu kumpa huduma.
“Unajua mambo ya klabu tena, kila mtu alikuwa bize na mambo yake, hivyo hatukuweza kugundua mara moja kuwa nani alihusika, lakini tulishangaa ghafla Kajala alijisikia vibaya hivyo marafiki zake wa karibu walimkimbiza nyumbani kwao kisha hospitali,” kilisema chanzo hicho.Baada ya paparazi wetu kuzinyaka habari hizo, Jumanne iliyopita (juzi) alimtafuta Kajala ambaye alikuwa amejipumzisha nyumbani kwa njia ya simu, akaeleza kwa shindashinda jinsi tukio hilo lilivyokuwa:
“Ilikuwa Jumapili usiku, nilikuwa nimekaa na washkaji zangu pale klabu akiwemo Mubenga, sasa niliagiza juisi pale nikaanza kunywa, funda la kwanza…la pili nikaanza kujisikia vibaya.
“Nilisikia kama kichefuchefu, nikatoka nje ambapo hali ilizidi kuwa mbaya. Marafiki wakashauri nirudishwe nyumbani, nako hali ikazidi kuwa mbaya.

“Wakanipeleka hospitali ambapo madaktari waliponipima walinambia nimekunywa kitu chenye sumu hivyo wakanipa dawa za kuondoa sumu mwilini na nashukuru Mungu, naendelea vizuri.”
Alipoulizwa kama ana ufahamu wowote juu ya aliyehusika na kama anaweza kumchukulia hatua zozote, Kajala alisema anamuachia Mungu kwani anaendelea vizuri.
“Mimi nashukuru bado napumua, siwezi kujua aliyefanya hivyo alikuwa na dhumuni baya kwangu au iliingia kwa bahati mbaya, naendelea vizuri,” alisema.